Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akisalimiana na Balozi wa India Nchini Tanzania Debnath Shaw,alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo asubuhi.[Picha na
Ramadhan Othman,Ikulu.]Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, akizungumza na Balozi wa India Nchini Tanzania Debnath Shaw,alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo asubuhi.[Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]
Na Said Ameir, Ikulu
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo amekutana na Balozi wa India nchini Mheshimiwa Debnath Shaw ambapo walizungumzia masuala mbalimbali ya Uhusiano na Ushirikiano kati ya Zanzibar na India.
Katika mazungumzo hayo Dk. Shein alisifu uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliodumu karne nyingi kati wa wananchi wa Zanzibar na watu wa India na kueleza kuwa nchi hizo zina kila sababu ya kuimarisha ushirikiano huo.
“wananchi wa Zanzibar na India tumekuwa katika ushirikiano kwa karne nyingi yafaa kuendelea kubadilishana uzoefu wetu katika hatua za maendeleo tulizofikia” Alisema Dk. Shein.
Kwa hiyo alimueleza Balozi Shaw kuwa Zanzibar ingependa kuona ushirikiano zaidi katika maeneo ya elimu na afya ambayo pande hizo zimekuwa zikishirikiana kwa muda mrefu lakini pia kupanua maeneo mapya ya ushirikiano ikiwemo kilimo na viwanda vya kusarifu mazao ya kilimo.
Aliyataja maeneo kuwa ni pamoja na uwekezaji katika sekta zote ikiwemo ya afya pamoja na sekta ya utalii ambapo Zanzibar ingependa kuona watalii wengi zaidi kutoka nchi za Asia wakiwemo toka India wanatembelea Zanzibar na Tanzania kwa jumla.
Kwa upande wake Balozi Debnath Shaw alimueleza Rais kuwa kupanua maeneo mapya ya ushirikiano ni muhimu katika kuimarisha ushirikiano kati ya India na Zanzibar.
Aliahidi kuyashauri makampuni ya biashara ya utalii nchini mwake kuingiza Zanzibar katika mipango ya safari za watalii wanaotembelea Afrika Mashariki.