Amesema Mtume Swalla Allaahu ‘Alayhi Wasallam katika mojawapo ya hadith Qudsiy kwamba, Allaah Subhaanahu Wata’ala amesema kuwaambia Malaika wake:
إذا هم عبدي بسيئة فلا تكتبوها عليه، فإن عملها فاكتبوها سيئة، وإذا هم بحسنة فلم يعملها فاكتبوها حسنة، فإن عملها فاكتبوها عشرا. |
Akiazimia mja wangu kufanya jambo baya, basi msiliandike dhidi yake. Akilifanya basi mliandike kama ni baya moja. Na akiazimia kufanya jambo jema lakini hakulifanya basi mliandike kama ni jema moja. Na akilifanya mliandike kama ni mema kumi. Muslim
Ndugu yangu katika imani, Umma wa kiislam umejaaliwa neema laitani kama tungelizitambuwa neema hizi umma huu ungelikuwa ni wa kupigiwa mfano.
Neema ya kupewa fursa na Muumba ya kutulipa kwa kunuia au kuazimia tu kufanya jambo jema si neema ndogo.
Neema ya kupewa fursa ya kutoandikwa dhambi zetu ikiwa tumeazimia tu kabla ya kuzitenda si neema ndogo.
Neema ya kulipwa mara kumi kwa jema moja tulilolitenda sio neema ndogo.
Ndugu yangu katika imani wapi katika ulimwengu huu uliotuzunguka utapata neema hizi?