Na Salum Vuai, MAELEZO
WANANCHI wa Zanzibar wanatarajiwa kunufaika na huduma za uchunguzi na matibabu ya meno zitakazoendeshwa na taasisi ya Zanzibar Help Foundation kwa ushirikiano na hoteli ya Doubletree By Hilton ya Dar es Salaam na hoteli ya Al Beit Al Salaam ya Zanzibar.
Huduma hizo zinatarajiwa kuwa za siku tatu kuanzia Disemba 5 hadi 7, mwaka huu zikiendeshwa katika kambi itakayokuwepo katika jengo la 'Zanzibar Help Foundation Practice', Vuga mkabala na tawi la CCM.
Huduma hizo zitakazoanza saa 2:30 asubuhi, zitaendeshwa na madkatari bungwa kutoka 'Zanzibar Help Foundation' na hospitali ya Aga Khan ya Dar es Salaam, na zitaolewa bila ya malipo yoyote.
Akizungumza na waandishi wa habari katika hoteli ya Al Beit Al Salaam, Mratibu wa kambi hiyo, Ali Jivraji ambaye ni mwanafunzi wa 'International School of Tanganyika' mwenye umri wa miaka 15, amesema kwa kutambua kwamba watu wengi wanasumbuliwa na meno, ameamua kuendesha kambi hiyo.
Alisema katika siku ya kwanza, huduma hizo zitatolewa kwa watoto wadogo, na siku mbili za mwisho zitakuwa kwa watu wazima na vijana.
Alifahamisha kuwa, lengo la kambi hiyo, ni kuwasaidia watu wenye matatizo ya meno kupata tiba hasa ikizingatiwa kuwa, gharama za matibabu hayo ni kubwa na kwamba wananchi wengi hawawezi kuzimudu kutokana na uhaba wa kipato chao.
"Dhamira yangu ni kuwafanya watu kufahamu umuhimu wa afya ya meno kwa kuwakutanisha na madaktari wataalamu watakaowasaidia kuondokana na matatizo waliyonayo," alieleza.
"Ili tuishi, tunapaswa kula, na ili tule chakula chenye afya ni muhimu sana tuwe na meno yenye afya pia," aliongeza Jivraji.
Aliishukuru Wizara ya Afya Zanzibar na taasisi zote zilizofanikisha kufanyika kwa kambi hiyo, na kuwahimiza wananchi wenye matatizo ya meno kujitokeza kwa wingi, akisema hiyo n fursa adhimu ambayo hawapaswi kuikosa.
Naye Mkurugenzi wa Zanzibar Help Foundation Dk. Feroz Jafferji, alisema taasisi yake imekuwa ikitoa huduma mbalimbali za kiafya hasa katika maeneo ya vijijini kwa miaka miwili na nusu sasa.
Alisema mkakati wa baadae ni kuhakikisha wanafika katika maeneo mengi zaidi ikiwemo Pemba, pamoja na kupata gari la kutoa huduma za meno (mobile dental clinic) ili kurahisisha kazi hiyo.