Na Mwajuma Juma
KAMATI ya Kombe la Mapinduzi Zanzibar imepanga ratiba ya makundi kwa timu za soka zitakazoshiriki michuano hiyo huku timu za Zanzibar zikiwa bado hazijajuulikana.
Kwa mujibu wa msemaji wa Kamati hiyo Farouk Karim alisema kuwa juzi kamati ilikkutana na kupokea majina ya timu zitakazoshiriki lakini cha kushangaza timu kutoka Zanzibar zikiwa hazijaorodheshwa.
Alisema kuwa katika kikao hicho kamati hiyo imepanga kwa makundi ratiba ya michuano hiyo ambayo yamegawiwa katika makundi matatu huku makundi mawili yakicheza katika kituo cha Unguja na moja kituo cha Pemba.
Alisema kuwa kundi A litaundwa na timu za Yanga, Azam, Tusker na timu moja kutoka Unguja, wakati kundi B likiunduwa na timu za Simba, KCC ya Uganda, Gormahia na moja kutoka Unguja.
Kwa upande wa kundi C ambalo kituo chake kitakuwa Pemba litaundwa na timu za Mbeya City, URA ya Uganda na timu moja kutoka Unguja.
Hata hivyo akizungumzia kuhusu hoja ya kutopeleka majina ya timu za Zanzibar Rais wa ZFA Taifa Ravia Idarous amesema kuwa wao kama ZFA hawajapeleka majina ya timu zozote.
Alisema kuwa kamati ilichokifanya walikuwa wakiwambia ZFA kuhusumajina ya timu wanazotaka kuialika kazi ambayo ilifanywa na ZFA lakini kuhusu kupeleka timu hilo wao hawalijui.
‘Mimi katika kikao hicho nilikuwepo lakini sisi kama ZFA hatujapeleka majina ya timu hizo timu wanazijuwa wenyewe”, alisema.
Hata hivyo alisema kuwa ZFA inatarajia kukutana siku ya Alkhamis wakati wa saa 5:00 asubuhi ili kuzungumzia juu ya timu ambazo zitashiriki michuano hiyo.
Michuano hiyo ambayo inatarajiwa kuanza Januari 2 mwakani kwa mujibu wa kamati ya Mapinduzi itashirikisha timu 12.