Na Othman Ame OMPR
Walimu Wakuu wa Skuli za Sekondari Nchini wanawajibu wa kuendelea kushirikiana zaidi na wazazi katika kuhakikisha ufaulu mkubwa wa wanafunzi unaongezeka zaidi kwa kuzingatia na kutumia akili zao.
Ushirikiano huo unaweza kufikia lengo kubwa iwapo utakwenda sambamba na upatikanaji wa uongozi ulio makini wa Kamati za maskuli katika maeneo mbali mbali hapa nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati akiufungua Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Jumuiya ya Walimu wakuu wa Skuli za Sekondari Zanzibar unaofanyika katika Ukumbi wa Skuli ya Sekondari ya Lumumba Mjini Zanzibar.
Balozi Seif alisema jambo kubwa liliopo hivi sasa katika kuona wanafunzi wengi wanafanikiwa katika muelekeo wa kitaaluma ni kujaribu kutumiwa mbinu za pamoja baina ya pande hizo mbili na namna ya udhibiti wa matumizi mabovu ya mitandao ya mawasiliano ya Kompyuta ambayo hufanywa na wanafunzi walio wengi Nchini.
Alifahamisha kwamba wanafunzi wa karne hii wamebahatika kupata nafasi nzuri ya kusoma kupitia mitandao hiyo ya Kompyuta lakini wengi kati yao hutumia fursa hiyo kwa kuangalia michezo na filam zilizo nje ya Maadili jambo ambalo huzorotesha kiwango chao cha ufaulu kwenye mitihani yao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaomba walimu Wakuu hao kusimamia vyema majukumu ya kazi zao za kila siku kwa walimu na wanafunzi wao kwa lengo la kunyanyua kiwango cha elimu kitakachokidhi mahitaji ya sasa ya sayansi na Teknolojia Duniani.
Alifahamisha kwamba Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 kutimia miaka 50 yanakwenda sambamba na miaka 50 tokea kutangazwa kwa elimu bila ya malipo hapa Zanzibar.
Alisema katika kuthamini uzito wa Mapinduzi hayo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar ipo katika utekelezaji wa sera mpya ya elimu ya mwaka 2006.
Balozi Seif alieleza kwamba lengo la sera hiyo ni kuweza kukabiliana na kasi ya maendeleo iliyopo ulimwenguni hivi sasa, mabadiliko ya Teknolojia kimazingira na kiakili katika kumuandaa vyema mtoto.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibart aliwapongeza Walimu Wakuu wa Skuli za Sekondari Zanzibar kwa uamuzi wao wa kuanzisha jumuiya hiyo na kutoa wito kwa skuli binafsi ambazo bado hazijajiunga kushirikiana na jumuiya hiyo ili kusaidiana kupata nguvu za pamoja zitakazosaidia kutatua baadhi ya changamoto zinazowakabili.
“ Skuli binafsi pia zinapaswa kupongezwa kwa mchango unazotoa wa kuiunga mkono Serikali kutoa elimu bora bila ya ubaguzi. Skuli hizi zimeisaidia sana Serikali kuwapatia ajira Raia wa Nchi hii pamoja na kuipunguzia mzigo mkubwa Serikali wa mrundikano wa wanafunzi katika skuli nyingi Nchini “ Alisema Balozi Seif.
Katika kuunga mkono jitihada za Walimu Wakuu hao wa Skuli za Sekondari Zanzibar za Kuunda Jumuiya yao Balozi Seif alichangia shilingi Laki 500,000/- kusaidia mkutano huo pamoja na kuahidi kusaidia Kompyuta moja na Mashine moja ya Foko Kopi kwa ajili ya Ofisi ya Jumuiya hiyo.
Aidha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaeleza wana jumuiya hiyo kwamba atawasiliana na Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji, Nishati na Madini katika kuangalia uwezekano wa kuipatia Jumuiya hiyo eneo la kujenga Ofisi yake pamoja na kupatiwa hati miliki za maeneo yote ya Skuli za Serikali.
Akisoma Risala ya Wanajumiya hiyo ya Walimu Wakuu wa Skuli za Sekondari Zanzibar Katibu wa Jumuiya Hiyo Maalim Fadhil Hamada Mshamba alisema lengo la kuanzishwa kwa jumuiya hiyo ni kuwaunganisha walimu wa Serikalina
Binafsi ili kuwa na sauti moja katika kuwafinyaga vyema watoto kielimu.
Maalim Fadhil alisema wanajumiya hiyo hivi sasa wanajivunia mafanikio makubwa waliyoyapata tokea kuanzishwa kwake mwaka 2009 ikiwa ni pamoja na kurejea kwa nidhamu katika maskuli mengi nchini, utunzaji wa mazingira pamoja na taaluma ya kuepuka taathira mbaya za ajira kwa watoto.
Katibu Mkuu huyo wa Jumuiya ya Walimu Wakuu wa Skuli za Sekondari Zanzibar alizitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili sekta ya elimu kuwa ni pamoja na uchakavu wa baadhi ya majengo ya Skuli, upungufu wa samani, ukosefu wa vyombo vya usafiri kwa walimu Wakuu pamoja na uvamizi wa maeneo ya Maskuli kwa kujengwa nyumba za kudumu za watu binafsi.
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Bibi Mwanaid Saleh alisema Wizara hiyo inaendelea na tathmini ya kupanga vigezo mbali mbali vitakavyotoa fursa kwa walimu kupanda daraja kwa mujibu wa Taaluma wanazozipata.
Mada mbali mbali zinajadiliwa katika Mkutano huo wa Siku Tatu wa Jumuiya ya Walimu Wakuu wa Skuli za Sekondari Zanzibar ukihitimishwa na uchaguzi Mkuu wa kuwachaguwa Viongozi wake wapya.
Miongoni mwa mada zitakazojadiliwa katika Mkutano huo kuwa ni pamoja Maendeleo na mafanikio ya elimu katika miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Utekelezaji wa Sera ya Elimu ya mwaka 2006 pamoja na changamoto zake, pamoja na Utawala wa Mwalimu Mkuu na utekelezaji wa majukumu .
Nyengine ni Mchango wa Skuli Binafsi katika kuleta maendeleo ya Elimu Zanzibar, usimamizi wa Mwalimu Mkuu katika somo la Hesabu pamoja na muelekeo Mpya wa tathmini ya mwanafunzi ndani ya Zanzibar.
Mkutano Mkuu huo wa Jumuiya ya Walimu Wakuu wa Skuli za Sekondari Zanzibar umepata baraka ya kuhudhuriwa pia na baadhi ya Viongozi wa Jumuiya ya Walimu Wakuu wa Skuli za Sekondari Tanzania Bara { TAHOSSA }.
Ujumbe wa mwaka huu wa Mkutano huo wa Jumuiya ya Walimu Wakuu wa Skuli za Sekondari Zanzibar { JUWASEZA } ni Muelekeo mpya wa Tathmini ya Mwanafunzi Zanzibar.