JUKAMKUM/BR/1/VOL.1/62 Date: 18/12/2013
RISALA FUPI KWA MGENI RASMI
MAKARIBISHO
MH: MGENI RASMI
Kwa niaba ya wanachama, Viongozi na Vijana kwa pamoja tunatoa shukrani zetu za dhati kwako, kwa kuamua kuja kuitembelea Jumuiya inayotoa Elimu kwa jamii kuhusu Athari za Madawa ya Kulevya, Ukimwi, Mimba katika umri mdogo (JUKAMKUM).
Tunaamini kuwa unazo shughuli nyingi za Kitaifa ambazo zina umuhimu mkubwa, lakini umeamua kuzibakisha hadi baadaye, tunasema ahsante sana na karibu JUKAMKUM.
MH: MGENI RASMI,
Fursa hii tulikuwa tunaisubiri kwa hamu kubwa na leo tumeipata, tunaamini ndani ya nyoyo zetu kuwa Jumuiya hii inatambulika na itaendelea kutambulika ndani ya nchi na nje ya nchi, pia itapata baraka zenye kheri, tunakuombea dua kwa Mwenyezi Mungu akupe kila la kheri, akuepushe na matatizo yote ya dunia wewe pamoja na familia yako yote Ameeen.
MH: MGENI RASMI,
Jumuiya hii imeanzishwa 08/06/2002 na kupata usajili 20/08/2008 kwa hati ya usajili namba 579, afisi ya Jumuiya ipo hapa Pemba katika Wilaya ya Chake Chake.
MH: MGENI RASMI:
Kila jambo linakuwa na sababu ya kuwepo kwake, hivyo lengo la jumuiya hii ni kama ifuatavyo:
1. Kupunguza utumiaji na athari za dawa za kulevya.
2. Kupunguza kasi ya maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi na ukimwi wenyewe
3. Kupunguza tatizo la watoto wa kike kupata mimba katika umri mdogo au zisizo tarajiwa.
4. Kupambana na maradhi nyemelezi ikiwemo TB.
MWELEKEO WA JUMUIYA:
ND. MGENI RASMI.
Jumuiya inashirikiana na itashirikiana na taasisi husika za Serikali na zisizo za kiserikali katika kupunguza ongezeko la utumiaji wa dawa za kulevya, maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi na ukimwi, pamoja na watoto wa kike waepuke kupata mimba katika umri mdogo.
MAFANIKIO:
Tulipata ruzuku ndogo kutoka The Foundation for Civil Society Tanzania Bara, ambapo ruzuku hii ilitumika kwa kuwapa elimu Vijana 80 wanaotumia dawa ili kujitambua.
Baada ya mafunzo hayo, vijana 15 waliamua kuacha kutumia dawa na sasa wanaelimisha wenzao waache kutumia dawa hizo.
Jumuiya ilianzisha Dropping Center kwa ajili ya kuwaelimisha vijana namna ya kujielewa na kujua wako wapi na wanahitaji kufika wapi na baada ya kuelewa dhana nzima ya kuwepo kwao duniani na kuwa wako ambao wanawategemea, tumeweza kuanzisha (Soba house) sehemu ambayo vijana hubakia humo kwa muda wa miezi mitatu mpaka mine ili kuweza kupata mafunzo ya jinsi ya kubadilisha tabia, kukabiliana na changamoto za hamu ya dawa ili kuweza kurejea kama mwanzo. Kwa sasa JUKAMKUM ina soba house tatu mbili zikiwa Wilaya ya Chake chake na moja Wilaya ya Mkoani.
Jumuiya imepata tunzo ya kuwa asasi bora kupitia The foundation for Civil society kwa mwaka 2012/2013.
Jumuiya inapata mashirikiano ya karibu sana na Viongozi wa Wilaya, Jamii husika na maafisa Wadhamini wa Wizara mbalimbali.
CHANGAMOTO ZA JUMUIYA:
1. Jumuiya imekabiliwa na tatizo la nyenzo zikiwemo fedha ambapo vijana waliopo wanahitaji kupata huduma za lazima kama , kula, kulala na matibabu ambapo baadhi ya wazee wanaweza kusaidia gharama lakini wengine hawamudu.
2. Majengo ambayo tunatumia kama soba house ni majengo ya kukodi, muda wa kodi umekaribia kumaliza na Jumuiya haina uwezo wa kumudu kwani gharama zake ni kubwa. Kwa hili tunaomba kwako kama Mzee utuangalie kwani jengo hili ambalo leo tupo hapa kodi yake inamalizika mwezi huu wa Disemba na mpaka sasa hatuna chanzo cha kuweza kupata gharama za kulipia kodi ya mwaka unaofuata.
3. Pamoja na kuwasaidia vijana katika kukabiliana na tatizo la utumiaji wa dawa za kulevya JUKAMKUM mpaka sasa haina mradi wa kuwaendeleza vijana wakaweza kuwa na angalau chanzo kidogo cha mapato.
JUKAMKUM inapenda kuchukua fursa hii kuomba kupatiwa nyenzo kwa ajili ya uanzishaji wa mradi wa ufugaji wa kuku na mbuzi kwa vijana walio katika vituo vyetu ambao kwa kiasi fulani mapato yake yanaweza kutumika kusaidia huduma za soba na kuwawezesha vijana kupata uzoefu wa ufugaji ambao wanaweza kuutumia katika jamii watakapotoka katika vituo hivi.
ND. MGENI RASMI:
Kwa kumalizia tunatoa tena shukurani zetu kwako na kwa wale wote ambao mmefika hapa kututembelea. Mwenyezi Mungu awajaalie afya njema na pia awarudishe salama nyumbani na katika ziara zenu nyengine ili kuendeleza mbele Taifa letu kwa ujumla.
Ahsanteni sana .