Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Hoja ya Mwakilishi Mgeni Hassan Juma dhidi ya vitendo vya udhalilishaji wa watoto Zanzibar

$
0
0

HOJA YA MJUMBE WA BARAZA LA WAWAKILISHI LA ZANZIBAR KULIOMBA BARAZA LA WAWAKILISHI LA ZANZIBAR KUTOA MAAZIMIO DHIDI YA VITENDO VYA UDHALILISHAJI WA WATOTO ZANZIBAR (CHINI YA KANUNI YA 27(1) (n), 27(3), 49(1),  50 YA KANUNI A BARAZA LA WAWAKILISHI, TOLEO LA 2012)


MAELEZO YA HOJA


KWA KUWA, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa na dhamira ya dhati ya kuwalinda watoto wa Zanzibar  kwa kuchukua hatua mbali mbali ikiwemo ya kuwa na Sheria namba 6 ya 2011na kuhakikisha kupatikana kwa  haki zao ikiwa ni pamoja na kuwapatia elimu bora, makaazi,  mavazi, chakula na kuwalinda dhidi ya aina zote za udhalilishaji.


NA KWA KUWA, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeridhia mikataba inayohusiana na haki za watoto duniani, ambayo Zanzibar  inahusika katika utekelezaji wa mikataba hiyo ili kuona azma ya kuwalinda watoto inafikiwa.


NA KWA KUWA, Kumekuwepo na ongezeko kubwa la kesi za udhallilishaji wa watoto, ikiwa ni pamoja na kesi za ubakaji na ulawiti hapa nchini


NA KWA KUWA kwa mujibu wa takwimu za Mahakama Kuu ya Zanzibar inaonesha kuwa katika mwaka wa 2010 kesi zipatazo 48 zilifunguliwa, ambapo kesi  35 zilitolewa maamuzi, kesi 13 zinaendelea kusikilizwa, na katika kesi zilizotolewa maamuzi ni kesi 2 tu ambazo washtakiwa wake walipatikana na hatia na kuhukumiwa adhabu ya kifungo na 7 kulipa faini na kesi 28 washtakiwa wake wameachiwa huru;


NA KWA KUWA, Kwa mwaka 2011 kesi 74 zilifunguliwa ambapo ni pamoja na kesi 18 za kuingiliwa kinyume na maumbile na kesi 56 za ubakaji,  kesi zinazoendelea ni 38 na kesi 36 zimetolewa maamuzi na kati ya hizo zilizotolewa maamuzi ni kesi 2 tu ambazo washtakiwa wake walitiwa hatiani na kupewa adhabu ya kifungo na 2 kulipa faini, na kesi 32 washtakiwa wake wameachiwa huru;


NA KWA KUWA, Kwa mwaka 2012 kesi 72 zilifunguliwa zinazojumuisha kesi 10 za kuingilia kinyume cha maumbile, na kesi 62 za ubakaji ambapo  kesi 61 zinaendelea kusikilizwa, na kesi 11 zimetolewa maamuzi ambapo kati ya hizo kesi 2 washtakiwa wake wametiwa hatiani na kupewa adhabu na 1 kulipa faini, na kesi 8 washtakiwa wake wameachiwa huru;

NA KWAKUWA kwa mujibu wa takwimu za tafiti zilizofanywa na taasisi mbali mbali zikiwemo asasi za kiraia zinaonyesha kuwa kesi nyingi zaidi zimekuwa zikiriporipotiwa polisi lakini zimeshindwa kufikishwa mahakamani kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo ya kukosekana ushahidi;


NA KWAKUWA , mbali na takwimu za mahakama kutoonesha hali halisi ya matukio mengi ya udhalilishaji wa watoto hapa Zanzibar, bado inaonyesha kuwa tatizo hilo ni kubwa sana nchini.


NA KWA KUWA , kesi nyingi zinazofikishwa mahakamani zimeshindwa kuthibitishwa kutokana na sababu mbali mbali na hivyo kupelekea washitakiwa wengi kuachiwa huru na hatimae kupelekea kuongezeka kwa vitendo hivyo vya udhalilishaji kwa watoto wetu.


NA KWA KUWA, Serikali inapaswa kuchukua hatua madhubuti ili kuwalinda watoto hao dhidi ya udhalilishaji na pale inapotokea watoto hao kufanyiwa vitendo hivyo vya udhalilishaji, kuhakikisha wahusika wa vitendo hivyo wanachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa Sheria ili kukomesha kabisa vitendo vya udhalilishaji kwa watoto wetu.


NA KWA KUWA, hali halisi ilivyo sasa hasa katika uendeshaji wa mashtaka ya wanaotuhumiwa kufanya udhalilishaji wa watoto inaonyesha kuwa bado tunashindwa kulikabili tatizo hili na hivyo wahusika wengi wa vitendo hivyo kuendelea na vitendo hivyo bila ya kupatikana na hatia kutokana na udhaifu wa mfumo mzima wa utoaji haki katika kesi za aina hii.


NA KWA KUWA, endapo hatua madhubuti hazitachukuliwa katika suala hili, watoto wengi wanaweza kuathirika kiafya na kisaikolojia na hivyo kuathiri maendeleo ya watoto hao na pia kuwafanya waathirika wa matukio haya ya udhalilishaji watoto kupoteza imani na mfumo mzima wa utoaji haki.


HIVYO BASI


Mimi, Mgeni Hassan Juma, Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi nafasi za wanawake, chini ya kanuni ya 27(1) (n) 27(3), 49 (1) na kanuni ya 50 ya kanuni za kudumu za Baraza la Wawakilishi toleo la 2012, naliomba                              Baraza hili tukufu, kwa kutumia mamlaka liliyo nayo liridhie kupitishwa maazimio yafuatayo:-


1.     Kuitaka Serikali ianzishe Mkakati wa Kitaifa wa Kupambana na Kutokomeza Udhalilishaji wa watoto utakaojumuisha Wawakilishi wa makundi mbali mbali katika jamii wakiwemo viongozi wa dini, polisi, makundi ya wanasheria, asasi za kiraia, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Wakuu wa Wilaya, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali na Wizara nyengine zinazohusika;


2.     Kwamba katika bajeti ya Serikali ya mwaka 2014/2015 na bajeti zitakazofuata, Mkakati wa kupambana na kutokomeza udhalilishaji wa Watoto uwe ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ili hatua za kupambana na udhalilishaji wa watoto zinazohitaji rasilimali fedha ziweze kutekelezeka bila ya vikwazo;


3.     Kwamba miongoni mwa majukumu ya msingi ya Mkakati wa Kupambana na Kutokomeza Udhalilishaji wa Watoto yazingatie utoaji wa taaluma kwa jamii kwa ujumla kuhusu namna ya kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya udhalilishaji na pia namna ya kushughulikia matukio ya udhalilishaji watoto pale yanapojitokeza;


4.     Kwamba kutokana na udhaifu ulioonekana katika kushughulikia kesi za udhalilishaji watoto, Serikali ianzishe utaratibu wa mafunzo ya pamoja ndani na nje ya nchi katika vipindi maalum kwa wahusika wanaosimamia mfumo wa utoaji haki katika kesi za watoto wakiwemo mahakimu, waendesha mashtaka, polisi, madaktari na makarani wa mahkama ili kuyajengea uwezo makundi hayo katika kushughulikia kesi za udhalilishaji watoto na pia kuleta uratibu wa pamoja (coordination) miongoni mwa taasisi hizo;


5.     Kwamba Serikali iingize katika mitaala ya elimu hasa katika ngazi ya elimu ya awali na elimu ya msingi, suala la udhalilishaji watoto na namna ya kujikinga dhidi ya udhalilishaji huo;


6.     Serikali iwekeze rasilimali zaidi ili kuziimarisha Mahakama za Watoto kwa kuweka idadi ya kutosha ya Mahakimu wa kudumu wa mahakama hizo, majengo, samani na mambo mengine yatakayofanya kesi hizo zisikilizwe katika muda mfupi na kwa kuzingatia haki;


7.     Serikali ifanye mapitio ya Sheria ya Mtoto na sheria nyengine zinazosimamia uendeshaji wa kesi za udhalilishaji wa mtoto ili kuleta tija katika uendeshaji wa kesi hizo ikiwemo kuweka muda maalum ambapo kesi hizo za udhalilishaji  zitapaswa kuwa zimemalizika;


8.     Katika kurahisisha upelelezi wa kesi za udhalilishaji wa watoto, serikali ihakikishe ndani ya kipindi kifupi kijacho, mashine ya uchunguzi wa vinasaba (DNA) inapatikana hapa Zanzibar;


9.     Kwamba Serikali ilete kila mwaka katika Baraza la Wawakilishi, ripoti ya hatua zinazochukuliwa katika kulikabili tatizo la udhalilishaji wa watoto itakayoonyesha hatua zilizochukuliwa katika kuzuia tatizo hilo na matokeo yake na pale matukio ya udhalilishaji yalipojitokeza, hatua zilizochukuliwa na matokeo ya hatua hizo;




Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.






………………………….

Mgeni Hasan Juma,

Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi,

Zanzibar.



Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>