CAIRO, Misri
JESHI nchini Misri limeipindua serikali iliyochaguliwa kidemokrasia ya Rais Mohammed Morsi, mwaka mmoja tu tokea achaguliwe.
Mkuu wa Majeshi Jenerali, Abdul Fattah al-Sisi alisema Morsi, amekosa kutimiza mahitaji ya watu.
Hatua hiyo inakuja baada ya siku nyingi ya maandamano dhidi ya rais Morsi.
Waandamanaji walimtuhumu yeye na chama chake kwa kusukuma ajenda ya kiisilamu kwa taifa hilo na kukosa kusuluhisha matatizo ya kiuchumi yanayolikumba taifa hilo.
Chama cha Muslim Brotherhood kimesema kuwa Morsi pamoja na washauri wake wako chini ya kifungo cha nyumbani na hawana mawasiliano ya nje.
Hapo awali mkuu wa majeshi alisema katiba ya nchi hiyo imeahirishwa na kwamba Jaji Mkuu wa taifa hilo atachukuwa mamlaka ya rais.
Maelfu ya Wamisri wanaopinga utawala wa Morsi wanaendelea kusherehekea,huku kukiwa na taarifa kwamba jeshi limeanza kuwakamata viongozi wa juu wa chama cha udugu wa Kiislamu na wasiwasi ikiwa hatua hiyo italeta muafaka wa kisiasa.
Rais Morsi alichaguliwa kihalali baada ya kuondolewa madarakani Rais wa zamani wa nchi hiyo, Hussein Mubarak.
Kwa siku nzima ya juzi watu walikuwa wakisubiri kwa hamu muda wa mwisho aliopewa Rais Morsi na jeshi, na jioni yake maelfu ya wapinzani wa kiongozi huyo walizidi kumiminika kwenye viwanja vya Tahrir na kasri ya rais.
Hali ilikuwa ya amani zaidi kuliko ilivyokuwa katika siku za hivi karibuni.
Pale waziri wa ulinzi alipoanza kutoa hotuba yake iliyongojewa kwa hamu na kwa muda mrefu, umma ulipiga kelele za “amani!amani!”, lakini dakika chache baadaye umma huo ukaripuka kwa vifijo na nderemo na uwanja wa Tahriri ukageuka mara moja kuwa uwanja wa tamasha.
Fashifashi zikatanda anga, na watu wakavaana huku wakifuta machozi ya furaha.
“Nina furaha ya kunichania nguo hapa, kuona kwamba Wamisri wa kila tabaka wapo uwanjani. Mtu anaweza kusema kwamba huku ni kuachiliwa uhuru wetu kutoka gerezani mwa wenye siasa kali. Udugu wa Kiislamu wamesababisha matatizo mengi sana,” alisema Sharif, Profesa wa chuo kikuu cha Cairo.
Sharif alisisitiza kwamba wote ni Wamisri na sio Waislamu au Wakristo, kwamba kwa miaka 7000 wamekuwa wakinywa maji mamoja na wakivuta hewa moja.
Lakini kando ya furaha hizo kubwa, watu hao waliopeperusha bendera kulipongeza jeshi kwa kumuondoa Mursi, bado wana maswali kadhaa ya kujijibu.
Jeshi, upinzani, wawakilishi wa kanisa la Koptik na wa dini ya kiislamu,walisema wamekubaliana kwamba Mkuu wa mahakama ya katiba awe rais wa kipindi cha mpito, lakini utaratibu mzima kuelekea uchaguzi mpya bado hauko wazi.
Pia haifahamiki hatima ya Rais Morsi na wenzake wa kundi la Udugu wa Kiislamu, ambao taarifa zinasema wanashikiliwa na jeshi.
Lakini Morsi alikuwa rais wa kwanza kuingia madarakani kupitia uchaguzi wa kidemokrasia, akishinda zaidi ya asilimia 50 ya kura, na hivyo uhalali na nguvu zake haziwezi kupuuziwa kisiasa na hata kisheria.
Bado haifahamiki ikiwa wafuasi wa Udugu wa Kiislamu, ambao waliripuka kwa ghadhabu wakati mkuu wa majeshi,alipokuwa akitangaza mapinduzi yake usiku wa kuamkia jana, watajiunga na kipindi cha mpito, ama nao wataendelea kuandamana na hivyo kuikwamisha tena nchi hiyo kisiasa.
Kwa vyovyote vile, bado mambo hayajesha kwenye taifa hilo kongwe kaskazini mwa Afrika
Washirika wa Morsi wameliitaka tangazo hilo la al Sisi kama mapinduzi dhidi ya utawala halali wa nchi na kwamba watapinga kwa nguvu zote hata ikiwezekana kugharimu maisha yao.
Rais Obama amesema ana wasiwasi mkubwa kuhusiana na matukio yaliyopo nchini Misri huku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Kimoon akitaka kuwe na utulivu.