Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Hamis Mdee akipima afya yake kwenye banda ya NHIF katika maonesho ya maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi Zanzibar.
Mwakilisho wa NHIF Zanzibar Ismail Kangeta (Katikati) akitoa elimu ya umuhimu na namna ya kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya katika maonesho hayo.
Ofisa Elimu kwa Umma wa NHIF, Grace Michael akifafanua jambo kwa wananchi waliofika katika banda la Mfuko huo.
Wananchi wakiendelea kupata huduma ya kupima afya zao ikiwemo uzito na hatimaye kupata elimu ya kujikinga na maradhi yasiyoambukiza.
…………………………………………………………………
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
MAMIA ya wananchi wa Zanzibar wamezipongeza huduma zinazotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya katika maonesho ya maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi yanayoendelea visiwani hapa.
Kutokana na hali hiyo, banda la Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) limekuwa kivutio kwa wananchi waliofika kwenye maonyesho hayo ambao mbali na kupata elimu ya umuhimu wa kujiunga na huduma za Mfuko huo, lakini walipata fursa ya kupima afya zao bure na kupata ushauri wa kitaalam wa namna ya kujikinga na maradhi yasiyoambukiza.
Akizungumza bandani hapo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Hamis Mdee alitoa mwito kwa wananchi wa Zanzibar kutumia fursa hiyo kupima afya zao lakini pia kuchukua uamuzi wa kujiunga na NHIF ili wanufaike na mafao yanayotolewa na Mfuko huo.
“NHIF ina mtandao mkubwa wa vituo vya kutolea huduma ambao unamwezesha mwanachama wetu kupata huduma popote pale alipo na kwa sasa tumejitahidi kusogeza huduma kwa wanachama wetu na wananchi kwa ujumla hivyo kwa Zanzibar ni vyema mkaitumia vyema fursa hii,” alisema Bw. Mdee.
Naye Ofisa Uhakiki Ubora wa NHIF Dk. Ally Mvita alitaja huduma zinazotolewa hapo kuwa ni kupima urefu, uzito, kisukari na shinikizo la damu.
Kwa mujibu wa Dk. Mvita kila mwananchi anayekubali kwa hiyari kupima hupewa ushauri na wataalam namna sahihi za kujikinga ili kukwepa maradhi hayo.
Baadhi ya wananchi waliofika kwenye banda hilo waliupongeza uongozi na watoa huduma wa mfuko huo kwa kutambua umuhimu wa Zanzibar kwa kusogeza huduma za mfuko huo visiwani humo.
Asha Ali Said mkazi wa Bububu alisema alipongeza kwa huduma za vipimo vinavyotolewa kwenye maonesho hayo kwa kuwa vinawasaidia wananchi kujua afya zao mapema kabla ya kupata maradhi.
Ali Shaaban Mohamed, hakusita kutoa mwito kwa wananchi wengine kufika bandani hapo na kutumia fursa hiyo ambayo ina manufaa kwao.
Katika maonyesho hayo yaliyozinduliwa visiwani hapa na Rais Dk. Ali Mohamed Shein yanashirikisha wizara, taasisi, mashirika na idara mbalimbali za serikali.