Na Abdi Shamnah
SERIKALI ya Oman imeombwa kuangalia uwezekano wa kuyafanyia matengenezo maeneo ya kihistoria, ikiwa ni hatua za kuendeleza ushirikiano uliopo kati yake na Zanzibar .
Ombi hilo limetolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Mhe. Said Ali Mbarouk, wakati alipofanya mazungumzo na ujumbe wa Taasisi ya Sayansi na Utamaduni ya Mfalme Qaboos wa Oman , ulioongozwa na Katibu Mkuu wake, Habib Al Riyami.
Alisema mbali na uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya wananchi wa nchi hizo, lakini pia kuna maingiliano ya karibu katika tamaduni zao.
Alisema majengo kadhaa yanayohusisha tamaduni kati ya watu wa mataifa hayo, yamechakaa na mengine kubaki magofu, hivyo aliuomba ujumbe huo kuangalia uwezekano wa kuyafanyia matengenezo, ili kuuenzi utamaduni.
Alisema majengo hayo yana umuhimu mkubwa kwa Zanzibar , kwani mbali na kuenzi hisitoria ya tamaduni ya watu wa nchi mbili hizo, lakini pia hutoa mchango mkubwa katika nyanja ya utalii.
Aliyataja baadhi ya majengo hayo kuwa ni pamoja na Beit el Ajaibu, Kasri la Mfalme, mahamuni ya Mtoni, Kizimbani na Msikiti chooko ulioko Chwaka Tumbe.
Nae Katibu Mkuu wa taasisi hiyo, Habib Al Riyami, aliahidi kuendeleza ushirikiano wa muda mrefu uliopo katika nchi hizo, kwa faida na maslahi ya watu wake.
Alisema Oman itaendelea na juhudi za kuimarisha uhusiano uliopo kupitia nyanja mbali mbali za kiutamaduni na kijamii.