Na Rehema Mohamed, Pemba
WANANCHI 16,656 wa Zanzibar wamefaidika na mikopo kwa vyama vya ushirika wenye thamani ya shilingi bilioni 1.27, kupitia Idara ya mikopo iliyo chini ya Wizara ya Uwezeshaji kuanzia mwaka 2000-2013.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mratibu Idara ya Mikopo Pemba, Nd. Humud Rashid Khamis, alisema fedha hizo zilitolewa kwa wilaya zote 10 kwa lengo la kuwakwamua wananchi na umaskini.
Kati ya fedha hizo, alisema tayari shilingi milioni 900.93, zimerejeshwa.Akizungumzia mafanikio ya wajasiriamali hao, Mratibu huyo alisema ni pamoja na kujipatia fedha za kujiendeleza kimaisha na kurejesha mikopo katika Idara.
Alisema, vikundi vilivyofaidika na mkopo huo ni vile vinavyojishughulisha na kilimo, bustani za mboga mboga, ufugaji, miradi midogo, viwanda, biashara za kusindika matunda, sabuni za dawa, vifaa vya utalii, saluni, vyakula, ufumani wa vikavu na samani.
Hata hivyo, alisema Idara inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo wanavikundi kutolipa mikopo yao kwa wakati, uhaba wa fedha na riba inayolalamikiwa na wanavikundi.
Aliwataka wanajamii kujikusanya na kuazisha vikundi vya ushirika ili kujikwamua na dimbwi la umaskini