Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Nape Nnauye akimtambulisha mgombea wa nafasi ya uwakilishi wa jimbo la Kiembesamaki Ndugu Mahmoud Thabit Kombo mara baada ya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kumteua kuwa mgombea wa nafasi uwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki kwa tiketi ya CCM. Picha na Adam H. Mzee
Na Mwinyi Sadallah
Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imemteua Mahmoud Thabit Kombo, kuwa mgombea wa kiti cha uwakilishi katika Jimbo la Kiembesamaki.
Jimbo hilo limekuwa wazi baada ya aliyekuwa mwakilishi wake, Mansoor Yussuf Himid, kufukuzwa uanachama kwa madai ya kwenda kinyume na maadili na sera za CCM.
Akitangaza uamuzi huo jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema: “Kamati Kuu imemteua Mahmoud kuwa mgombea wa CCM. Ni mgombea aliyekidhi vigezo, ana uwezo wa kutosha, hodari, muumini wa Muungano na mtetezi wa Mapinduzi ya Zanzibar.”
Akizungumza mara baada ya uteuzi huo, Kombo alisema anashukuru jina lake kupitishwa na kwamba anaamini CCM itashinda.
“Nafikiri sina ubora wa kuwapita wenzangu ila kura zangu zimetosha. Nitaungana na kushirikiana nao katika kukitafutia ushindi chama chetu. Tunajenga nyumba moja hatutagombania fimbo,” alisema Mahmoud ambaye ni mtoto wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa kwanza wa ASP, hayati Thabit Kombo Jecha.
Wengine waliokuwa wakiwania kuteuliwa ni Suleiman Haroub Pandu, aliyeshika nafasi ya pili katika kura ya maoni na Mwanaasha Abdallah, aliyeshika nafasi ya tatu.
Wote watatu jana asubuhi walionekana wakiingia kwenye Jengo la CCM Kisiwandui wakati kikao hicho kikiendelea.
Nape alisema mgombea huyo anatarajiwa kuchukua fomu katika Ofisi za Tume ya Uchaguzi Zanzibar(ZEC) leo.
Kampeni za uchaguzi huo mdogo zinatarajiwa kuzinduliwa Januari 22 mwaka huu na mgeni rasmi anatazamiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Mohamed Gharib Bilal na kufungwa Februari mosi na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Balozi Seif Ali Idd.
Wakati huohuo, Nape alisema msimamo wa sera ya CCM wa kutetea muundo wa Muungano wa Serikali mbili bado unaendelea.
Alisema licha ya rasimu ya pili ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kupendekeza Serikali tatu, msimamo wa CCM uko pale pale.
Nape alisema msimamo wa kuwa na muundo wa serikali mbili ulitokana na sera ya chama hicho na kwamba hadi sasa hakuna kikao chochote cha kikatiba kilichokaa na kubadili msimamo huo unaopingana na mapendekezo ya tume.
Chanzo : Mwananchi