Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Maoni ya kamati kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya wizara ya kazi, uwezeshaji wananchi kiucumi na ushirika

$
0
0

HOTUBA YA  MWENYEKITI WA KAMATI YA MIFUGO,UTALII,UWEZESHAJI NA HABARI YA BARAZA LA WAWAKILISHI, ZANZIBAR KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA KAZI,UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI NA USHIRIKA KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014.


Utangulizi.

Mheshimiwa spika, awali ya yote, nachukua fursa hii muhimu kumshukuru Mwenyezimungu kwa neema zake zisizo na ukomo kwetu ikiwa ni pamoja na kutujaalia uhai na afya njema kiasi kwamba tumemudu kukutana hapa leo, ili kujadili mambo mbali mbali yenye manufaa kwetu  binafsi na kwa wananchi wetu kwa ujumla.Kwa hakika kama si taufiki na rehma za Mwenyezimungu juu yetu basi huenda muda huu tusingekuwa hapa tukipitia Bajeti za Wizara za Serikali.

Mheshimiwa Spika, Pili napenda kuendeleza shukrani zangu za dhati kwako binafsi kwa kuniruhusu nitowe mchango kwa niaba ya Kamati ya Mifugo, Utalii,Uwezeshaji na Habari na pia kwa niaba ya wananchi wa jimbo la Bumbwini. Aidha,naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Raisi wa ZANZIBAR na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa heshima na busara zake za kuiongoza Nchi yetu ya Zanzibar,kwa kuheshimu Utawala Bora.

Mheshimiwa Spika, naomba pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Watendaji wake wote wakiongozwa na Katibu Mkuu kwa kujitahidi kutekeleza malengo na majukumu yao kwa bidii kubwa katika kipindi cha mwaka 2012/2013,lakini pia kwa mashirikiano yao mazuri waliyotupa wakati Kamati ilipokua ikitekeleza kazi zake za kawaida.

Mheshimiwa Spika, nitakuwa mtovu wa fadhila nisipowapongeza wajumbe wote wa Kamati ya Kudumu ya Mifugo, Utalii,Uwezeshaji na Habari ya Baraza la Wawakilishi  kwa imani yao kubwa juu yangu iliyowapelekea kunichagua mimi kuwa ndio mwenyekiti wao na pia kwa ushirikiano wao mkubwa waliouonesha wakati wote ambao Kamati ilipofanya kazi za ufuatiliaji, ikiwa ni pamoja na kuihoji Serikali na kutoa  maoni yao kwa lengo la kuimarisha utendaji na kukuza uwajibikaji katika Serikali.


Mheshimiwa Spika, naomba kuwatambua Wajumbe hao kwa kuwataja kama ifuatavyo:-

1.       Mhe. Mlinde Mabrouk Juma                           -        Mwenyekiti

2.       Mhe. Abdalla Mohammed Ali                        -          Makamo Mwenyekiti

3.       Mhe. Asha Bakar Makame                             -          Mjumbe

4.       Mhe. Mussa Ali Hassan                                  -         Mjumbe

5.       Mhe. Kazija Khamis Kona                              -          Mjumbe

6.       Mhe. Amina Iddi Mabrou                     -        Mjumbe

7.       Mhe. Asaa Othman Hamad                            -         Mjumbe

8.       Mhe. Mohammedraza Hassanali Mohammedali  Mjumbe

9.       Ndg. Maryam Hussein Rajab                             Katibu

10.      Ndg. Abubakar Mahmoud Iddi                         -Katibu

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo napenda sasa nitoe maoni ya Kamati ya Kudumu ya Kamati ya Mifugo, Utalii,Uwezeshaji na Habari kuhusu makadirio  ya mapato na Matumizi ya Wizara hii kwa mwaka wa fedha 2013/2014 kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika,Wizara ya Kazi,Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika inajukumu la kusimamia na kuratibu utekelezaji wa sheria za kazi, programu za uendelezaji wa miradi,  uwezeshaji wa miradi na uwezeshaji wananchi kiuchumi hususan wananchi wenye kipato cha chini ili kuwapunguzia makali ya umasikini pamoja na kusimamia maendeleo ya ushirika.

Mheshimiwa Spika, Kamati inaipongeza Wizara hii kwa juhudi na jitihada wanazozichukua katika kutekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na kufanikiwa kuwatoa watoto 398 katika ajira mbaya kutoka katika maeneo tofauti ndani ya Zanzibar na kuwarudisha Skuli ikiwa  ni pamoja na kuwapatia vifaa mbali mbali kama viatu,madaftari na Sare za Skuli ili waweze kubakia maskulini kwalengo la kupata elimu ambayo itawasaidia katika maisha yao.

Mheshimiwa Spika, Mpango huu umetayarishwa kwa lengo la kuwapa watoto haki yao ya kusoma ili waweze kufanya kazi zenye tija pindi watakapomaliza masomo yao. Kutokana na juhudi hizo Kamati inawashauri Wazazi ambao bado wanawaruhusu watoto wao kufanya kazi zisizoeleweka waache mara moja tabia hiyo kwani hicho ni kitendo kibaya ambacho  kinawanyima watoto haki zao za msingi za kuishi katika Nchi yao.

Mheshimiwa Spika, Hii ni Wizara mpya kwahivyo kuna umuhimu kwa kupewa kipaumbele na Serikali hasa ukizingatia kazi za Wizara hii ni kutoka nje zaidi na sio kubakia Ofisini kwa hivyo vifaa kama Honda,Vespa na magari kwa lengo la kuzidisha ufanisi wa Wizara hii.Mheshimiwa Spika, Kamati imesikitishwa mno na fungu lililotengwa kwa ajili ya ununuzi wa Mashine na Zana kwa Afisi Kuu ya Wizara iliyoko Pemba kwa mwaka huu wa fedha ambalo ni jumla ya shilingi ya Kitanzania  11,650,00/=.

Mheshimiwa Spika, Wizara hii kazi zake nyingi ni za kupeleka huduma kwa Wananchi,kwa mnasabaha huu basi usafiri ni kitu cha lazima kwa watendaji wa Wizara hii ila cha kushangaza kasma nambari 311203 ambayo imewekewa shilingi 5,000,000 ambayo ndio ya ununuzi wa vyombo vya maringi mawili haiwezi kukidhi mahitaji ya Wizara hii, pesa ambazo hata Honda moja huwezi kulinunua. Hivyo tunaishauri Serikali kuengeza pesa katika fungu hili ili Wizara iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi kama ilivyojipangia.

Mheshimiwa Spika,Tunaishukuru Wizara kwa kuendelea kuratibu vyema mfuko wa Zakka ambao lengo lake ni kuwanasua kiuchumi Wananchi hususan wale wenye kipato cha chini ili kuwapunguzia makali ya umasikini kwalengo la kuleta maendeleo katika nchi yetu. Mheshimiwa Spika pamoja na hayo Kamati inaishauri Wizara kuzidi kutoa elimu kuhusiana na fedha hizo za Zakaa maana kumejitokeza tatizo kwa baadhi ya Wananchi kutorudisha fedha hizo wakati katika nchi hii kuna wananchi wengi ambao wanazitegemea pesa hizo ili wenzao watakaporudisha halafu wapewe wao. Mheshimiwa Spika Kamati pia inaishauri Wizara iwe inatoa pesa hizo kwa vikundi vichache ili wapate pesa nyingi kuliko kutoa pesa chache kwa vikundi vingi hatimae pesa zinaliwa bila ya kufanyika lolote na pia Kamati inashauri Ofisi ya Wakfu isimamie zoezi hili kwavile ni wazoefu na sio Wizara.

Mheshimiwa Spika,Kamati inaishauri  Wizara ya Kazi,Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika kujenga tabia ya kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi pindi inapotembelea wajasiriamali wake kwani kumejitokeza tatizo la wajasiriamali wingi hususani wale wanaojishughulisha na kazi za ufugaji wa Samaki kutofahamu kuwa kuna wataalamu wa kizalendo ambao wanapatikana hapa Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, Kamati pia imeridhishwa na kiwango cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya kutumika katika Idara uendelezaji na Uratibu wa Programu za Uwezeshaji wananchi kiuchumi. Mheshimiwa Spika naomba ieleweke kwamba miongoni mwa malengo ya  Idara hii ni kujenga Utamaduni wa ujasiriamali na kuimarisha uwezo wa wajasiriamali hususan vijana katika Wilaya 10 za  Zanzibar.Kwa kiwango hicho cha fedha walichoekewa wataweza  kutimiza malengo yao kwa ufanisi. Hatahivyo Kamati inashauri Wizara ya Fedha kujenga tabia ya kuingiza fedha kwa wakati ili Idara iweze kutekeleza vyema shughuli zake kiufanisi na kwa muda iliyojipangia.

Mheshimiwa Spika, Kamati inaipongeza Idara ya Mikopo kwa malengo mazuri waliyojiwekea kwa mwaka wa fedha 2013/2014 ikiwa pamoja na kuimarisha uwekaji wa kumbukumbu za mikopo. Mheshimiwa Spika kwakweli Idara hii ina kazi ngumu sana hasa katika upande wa kutunza kumbukumbu kwa vile vikundi vilivyowahi kuchukua mikopo vingi husambaratika na hatimae pesa hupotea na kutorudi tena Serikalini kwa lengo la kuwakopesha wananchi wengine ili na wao wafaidike na huduma hiyo.Kamati inaishauri Wizara ya Fedha kuwaingizia fedha zao kwa wakati ili Idara iweze kufanya kazi zake kwa umakini zaidi kwani pindi itakapokua inachelewa kuvipitia vikundi vyake na kukusanya marejesho yake ndio upotevu wa pesa utakapojitokeza.

Mheshimiwa Spika,Kamati imebaini kuwepo kwa tatizo la ukosefu wa taarifa za kutosha juu ya fursa za mikopo kwa vikundi mbali mbali vya ushirika.Hayo yamebainika wakati Kamati ilipokua ikifanya Kazi zake za ufuatiliaji ikabahatika kukutana na baadhi ya vikundi ambavyo vinaendesha shughuli zake katika mazingira magumu.Hali hii hupelekea vikundi vingi kubakia na umasikini wakati fursa zipo za kuwawezesha kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, Kamati inaishauri Wizara kwa kupitia Idara yake ya Mikopo  katika mipango yake ya mwaka 2013/2014 wajikite zaidi katika kutoa taarifa kwa kupitia vyombo vya habari mbali mbali ambavyo vina idadi kubwa ya wasikilizaji na watazamaji ili wananchi waweze kuzitambua fursa zinazopatikana katika Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, Idara ya Ushirika ilifanya tathmini juu ya uwezekano wa kuanzisha Benki ya Ushirika Zanzibar na kubaini kuwa upo umuhimu wa kuwa na Benki ya ushirikia Zanzibar.Mheshimiwa Spika, ingawa sekta ya  ushirika pekee haitoshi kugharamika mtaji wa uanzishwaji wake huo wa kuanzisha Banki, Kamati inaiomba Serikali kuhimiza agizo lake la kuwepo kwa  ushirikiano baina ya uanzishwaji wa Benki ya wanawake na Benki ya Ushirika lifanyiwe kazi haraka iwezekanavyo ili Bank ianze kutoa huduma zake kwa lengo la kutuletea Nchi yetu maendeleo kwani Wananchi watafaidika kwa uwepo wa Banki hiyo Zanzibar.

Mheshimiwa Spika,Kamati imeridhishwa na kazi inayofanywa naWizara ya Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika ya kuendeleza zoezi la kutoa mafunzo  maalum kwa kuwapatia taaluma watendaji wake inayohusiana na utekelezaji wa Mikataba ya kimataifa ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) ambayo yametolewa kwa lengo la kuwaelimisha watendaji juu ya wajibu wao wa kufanyakazi kwa mujibu wa miongozo ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) ambayo Nchi yetu imeridhia.

Mheshimiwa Spika, kutokana na hali mbaya wanayokumbana nayo wajasiriamali walioko katika masoko,Kamati inawashauri wajasiriamali  hao waliopo katika vikundi waunde ushirika au SACCOS katika maeneo yao ya kazi ili waweze kupata maendeleo zaidi ya kiuchumi kutokana na kufaidika na fursa za watakayopatiwa. Aidha, kupitia vyama hivyo wataweza kuyatatua matatizo mbalimbali yanayowakumba kwavile vyama hivyo vitakuwa na nguvu na sauti kutokana na kusajiliwa na kutambuliwa kisheria.Kufanya hayo pia kutachangia kwa kiasi kikubwa kufanikiwa kwa azma muhimu ya Serikali hii ya awamu ya saba ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi.

Mheshimiwa Spika,Kamati yetu imetiwa moyo na utekelezaji wa majukumu ya Kamisheni ya Kazi kwa kufanikisha na kuanza kazi kwa  kanuni mbili za Sheria ya Ajira nambar 11 ya mwaka 2005 zinazohusu maslahi ya wafanyakazi katika sekta binafsi na Kanuni ya Usajili na utendaji kazi wa Vyama vya Wafanyakazi. Mheshimiwa Spika, adhma ya Serikali yetu tukufu ni kuhakikisha wananchi wake wanapata haki zao za msingi kama inavyoelekeza Katiba ya Zanzibar kifungu cha 21(4)toleo la 2010. Hivyo kwa kutumia kanuni hizi ambazo zinatoa miongozo juu ya maslahi kwa wafanyakazi katika sekta binafsi nina imani zile kero ambazo kila siku zilikua zikifikishwa hapa Barazani juu ya maslahi ya Wafanyakazi wa sekta binafsi pamoja na mambo ya mikataba kwa wafanyakazi kwa sasa zimepata mkombozi.

Mheshimiwa Spika,shukurani za dhati tunazitoa kwa fungu lililotengwa kwa ajili ya Kamisheni ya Kazi.Ni dhahiri kuwa mgao huo umefanywa kutokana na majukumu makubwa inayobeba Kamisheni .

Mheshimiwa Spika, Kamati inaiomba Wizara ifanyejitihada za kuwawezesha na kuwapa elimu kina Mama hususan walioko vijijini kupata miradi watakaweza kuimudu kwani kuna baadhi ya miradi ya kinamama hao inaonekana kuwatesa kama vile mradi wa mwani ambapo faida inayopatikana haiendani na nguvu zinazotumika.Vilevile kutokana na kutokua na elimu ya kuuhifadhi mwani huo hupelekea mwani huo kushuka kiwango kinachohitajika katika soko la kimataifa.

Mheshimiwa Spika, Kamati ilipata nafasi ya kutembelea Ofisi kuu Pemba  na Idara zake inazoziratibu na kujionea hali halisi ya mazingira magumu ya utendaji kazi kwa watumishi wake na hata Afisa Mdhamin. Kamati inaishauri Serikali kuona haja ya kutafutiwa jengo la Ofisi pamoja na vitendea kazi ambavyo kamati iliishauri Wizara vipatikane kwa haraka ili kuweza kuratibu kazi zao kwa ufanisi zaidi,Pia Kamati imeridhika baadhi ya  malengo ya Ofisi hii iliyojipangia kwa mwaka mpya wa fedha kama vile kuongeza upatikanaji wa fursa za ajira za heshima kwa wananchi ,kuimarisha na kuongoza program za uwezeshaji wananchi kiuchumi na kusimamia utekelezaji wa sheria za kazi.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka milango wazi kwa wawekezaji wa ndani na nje kuanzisha miradi yao mbalimbali hapa nchini kwa lengo la kuinua uchumi wa Nchi yetu ikiwa ni pamoja na kupatikana kwa fursa mbali mbali za ajira kwa vijana wetu.Kamati imefurahishwa kuona mawakala binafsi wa Ajira za nje wamesajiliwa rasmi na wamepewa mikataba maalumu kwa lengo la kuwalinda Wazanzibari.Pia Kamati imeridhika kusikia kua Balozi zetu zilizokua nchi mbali mbali duniani zinahusika katika kupitia mikataba  ya kazi kabla haijafika huku Zanzibar ili wananchi wetu wasipate mashaka pindi watakapokuwepo huko ugenini .Mheshimiwa Spika ,kimsingi Kamati inaishauri  Wizara itafute kwa kina upatikanaji wa kazi nje na sio kuwaachia mawakala pekeyao.

Hitimisho.

Mheshimiwa Spika, napenda sasa kuwashukuru Wajumbe wote kwa kunisikiliza kwa makini na utulivu,pia napenda kukushukuru kwa mara nyengine tena wewe binafsi kwa kuniruhusu kutoa maoni ya Kamati ya Mifugo, Utalii,Uwezeshaji na Habari.

Mheshimiwa Spika,baada ya maelezo hayo napenda kutamka kwa niaba ya kamati ya Mifugo, Utalii,Uwezeshaji na Habari na kwa niaba ya wananchi wa jimbo langu la  Bumbwini ninaunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Wizara ya Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika .Aidha nawaomba Wajumbe wote wachangie na kuunga mkono Makadirio ya Bajeti ya Wizara hii kwa ajili ya utekelezaji bora wa majukumu na malengo waliyojipangia.

Mheshimiwa Spika ,naomba kuwasilisha.

Ahsante,

………………

(Mlinde Mabrouk Juma )

Mwenyekiti,

Mifugo, Utalii,Uwezeshaji na Habar



Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>