Na Salum Vuai, MAELEZO
UONGOZI mpya wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), umeanza kupunguza changamoto za kiofisi zinazokikabili kwa miaka mingi baada ya kufanikiwa kununua gari mbili ili kurahisisha utendaji wake.
Gari hizo aina ya NOAH zilizonunuliwa nchini Dubai (U.A.E) zikiwa na thamani ya shilingi 19,900,000, zilikabidhiwa jana kwa uongozi wa chama hicho na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk, katika ofisi za ZFA zilizoko uwanja wa Amaan.
Akizungumza katika hafla hiyo kabla kukabidhi funguo za gari hizo, Waziri huyo alisifu hatua ya chama hicho kwa kuamua kufanya kazi kisasa, akisema vyombo vya usafiri ni nyenzo muhimu katika utendaji wa taasisi yoyote.
Aidha alisema kupatikana kwa gari hizo, kutasaidia kupunguza changamoto zinazokwamisha shughuli za ZFA, lakini akawasisitiza viongozi wa chama hicho waendeleee kufanya kazi kwa kushirikiana na wadau wengine ili kuleta maendeleo ya mpira wa miguu Zanzibar.
Alieleza kufarijika kwake na namna ZFA ilivyoanza kubadilika na kuondokana na migogoro aliyoirithi wakati akikabidhiwa wizara yake, na kutaka vyama vyengine vya mnicxezo viige mfano wa chama hicho kwa kubuni njia za kujitafutia mapato badala ya kupeta miguu na kusubiri ruzuku ya serikali.
"Hatutaki vyama vinavyojiendesha kwa ofisi za mifukoni, au kuishi kwa migogoro na malumbano kupitia vyombo vya habari. Vyama kama hivyo havitufai na nimemuelekeza Mrajis avifutilie mbali," alifafanua Waziri Mbarouk.
Mapema, Makamu wa Rais wa ZFA Pemba Ali Mohammed, alisema baada ya kununua gari hizo kwa ajili ya ofisi za chama hicho Unguja na Pemba, katika miezi michache ijayo, wanakusudia kununua gari nyengine kumi kwa ajili ya ofisi zote za ZFA wilayani.