MAADHIMISHO YA MIAKA 50 YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR
MRADI WA KUTOA MIKOPO KWA WAJASIRIAMALI WADOGO (SELF) NA MKAKATI WA KUPUNGUZA UMASIKINI WA KIPATO:
Ø SELF ni Mradi wa kutoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo kupitia asasi ndogo na za kati za fedha.
Ø SELF yatimiza miaka 13 ya huduma ya kutokomeza umasikini nchini.
Ø SELF yaeleza mikakati yake, mafanikio na changamoto
Tangu mwaka 1961 Serikali ya Tanzania imekuwa inapambana dhidi ya maadui watatu wa maendeleo yaani; ujinga, maradhi na umasikini. Aidha, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, Malengo ya Maendeleo ya Milenia na MKUKUTA na MKUZA; inaainishwa changamoto za kuyapata maendeleo na haja ya kuweka vipaumbele. Wakati tukiadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar,12 January 2014, changamoto kubwa inayoikabili Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kama ilivyo kwa serikali nyingine katika nchi zinazoendelea, ni jinsi ya kutekeleza mipango ya kuwawezesha wananchi wengi zaidi kushiriki kikamilifu katika shughuli kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na hatimaye nchi nzima; ili waweze kuwa na maisha ya viwango vya kuridhisha na kustahimilika kama vilivyoanishwa katika Malengo ya Milenia.
Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA),umeandaliwa katika nguzo kuu tatu. Nguzo ya kwanza ni ‘’Ukuaji wa Uchumi na Kupunguza Umaskini wa Kipato.’’ Nguzo hii inaunganishwa kwa karibu na nguzo ya pili ya ‘’Kuimarisha Ubora wa Maisha na Ustawi wa Jamii’’, na nguzo ya tatu ni ‘’Utawala Bora na Uwajibikaji’’ ambayo ni msingi muhimu wa nguzo mbili zilizotangulia.
Serikali inatambua kwamba umasikini wa kipato ni chanzo na/au kichocheo cha maradhi na ujinga katika jamii, ndiyo maana juhudi za dhati zinahitajika ili kuhakikisha kuwa, sambamba na kupatikana kwa mahitaji ya msingi; chakula, mavazi na makazi, suala la kuwawezesha wananchi kijikwamua wao wenyewe kiuchumi, ni la msingi kabisa; hasa ikizingatiwa kwamba uwezo wa Serikali pia una ukomo kutokana na upungufu wa rasilimali. Hivyo Serikali inatakiwa iandae mazingira mazuri ya kutekeleza MKUKUTA na MKUZA; yanayoshirikisha jamii kubwa katika masuala ya kiuchumi. Ndani ya MKUKUTA na MKUZA, imeainishwa miradi na programu mbalimbali kusaidia Watanzania na hasa wale wa kipato cha chini mijini na vijijini waweze kujiajiri na kuongeza vipato. Mradi wa SELF ni miongoni mwa miradi iliyoanzishwa, kwa lengo hili.
Mradi wa kutoa Mikopo kwa wajasiriamali wadogo (SELF ), ni Mradi wa kutoa mikopo kwa Asasi ndogo za kifedha ili hatimaye asasi hizo ziweze kutoa mikopo hiyo kwa wananchi wajasiriamali wenye kipato kidogo waliopo mijini na vijijini.
Lengo kuu la Mradi ni kukuza na kuboresha upatikanaji wa huduma za kifedha, hivyo kuwapa fursa ya kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali kwa lengo la kujiongezea kipato ili kuondokana na umaskini. Ili kufikia lengo hili, Mradi wa SELF unatekeleza shughuli zifuatazo:
1. Utoaji wa mikopo kwa Asasi za kifedha kwa lengo la kuwakopesha walengwa wa mradi wa SELF: Ukiwa ni mradi uliojizatiti kikamilifu kuwapa watu masikini fursa ya kuwa na uchaguzi katika kujipangia maendeleo yao, kupambana na umasikini, na kujenga msingi bora na imara ya vyanzo vya mapato kwa ajili ya mahitaji yao ya kila siku; SELF – inatoa mikopo kwa Asasi za kifedha (Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGOs), Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS), Kampuni zinazotoa mikopo (Microfinance Companies), Jumuia za kijamii (CBOs), Benki za wananchi za maendeleo (Community Banks) ambazo nazo hutoa mikopo kwa walengwa ambao ni Wanawake,Vijana,Walemavu wake kwa waume, Wakulima na Wajasiriamali wadogo wadogo. Mikopo hii inatolewa katika kiwango cha riba nafuu; kiwango ambacho kitaziwezesha Asasi za kifedha kutoa mikopo kwa walengwa wanaofanya shughuli za uzalishaji mali katika sekta rasmi na isiyo rasmi huku wakimudu gharama zao za uendeshaji. Mikopo hii inatolewa tu kwa zile Asasi za kifedha zenye uwezo na sifa nzuri katika kusimamia utoaji wa mikopo kwa kufuata taratibu bora na sahihi za usimamizi wa fedha.
2. Kujenga Uwezo: Katika kuhakikisha kuwa yanakuwepo mazingira mazuri yanayo shajiisha kuwepo kwa huduma endelevu za kuweka na kukopa, SELF imetenga fedha kwa shughuli zifuatazo:
Ø Kuendeleza Kada ya Wafanyakazi: SELF imejizatiti katika kutoa mafunzo kwa mujibu wa tathmini ya mahitaji ya mafunzo kwa wafanyakazi na viongozi wa asasi wabia wa mradi kwa Kada zifuatazo:
· Wajumbe wa bodi, kamati za mikopo na usimamizi wa fedha, maafisa mikopo pamoja na makarani.
· Wajasiriamali wadogo walengwa wa mradi ambao ni wabia wa asasi za fedha zinazoshirikiana na Mradi.
· Maafisa ushirika.
Ø Kuandaa kada ya Wakufunzi na utayarishaji wa mitaala inayotumika kufundishia.
Ø Kusaidia ukarabati wa majengo ya ofisi na vitendea kazi pamoja na samani za ofisini kwa asasi wabia wa mradi
3. Uhamasishaji na Ufuataliaji: Ukiwa kama kielelezo cha jitihada za mwanadamu na matarajio yake katika mapambano dhidi ya umaskini uliokithiri, mradi wa SELF umeandaa kampeni mbalimbali kwa lengo la kuuelimisha umma kuhusu shughuli za mradi na kutoa hamasa kwa wananchi ili waweze kuelewa umuhimu wa kujiajiri, kujipatia mikopo na kuirejesha mikopo kwa wakati na kwa faida ya wote. Aidha ufuatiliaji na tathmini ya mara kwa mara ya shughuli za mradi ni nguzo kuu katika kujua maendeleo yake kwa ajili ya ufanisi.
Mradi huu ulianza kutekelezwa mwaka 1999/2000, ni Mradi uliobuniwa na Serikali na kufadhiliwa na Serikali ya Tanzania na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), ili kutoa huduma zilizo endelevu za kifedha kwa jamii ambayo ilikuwa haijafikiwa na huduma rasmi za kifedha hususani jamii za vijijini.
Serikali ilikusudia kutumia fedha hizi, kuanzisha mfuko ambao utatoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wananchi kupitia Asasi za Kifedha. Eneo la mwanzo la shughuli za Mradi wa SELF ilikuwa kwenye mikoa 6 yaTanzania bara, ambayo wakati huo ilibainika kuwa nyuma kimaendeleo na kwenye mikoa 5 ya Tanzania visiwani. Mikoa hiyo ilikuwa ni Mtwara, Lindi, Pwani, Dodoma , Singida na Dodoma . Mnamo mwaka 2004/05, Serikali iliongeza eneo la Mradi wa SELF kufikia mikoa 14 ya Tanzania Bara. Mikoa mipya iliyoongezwa ilikuwa Mwanza, Mara, Ruvuma , Mbeya, Iringa, Tanga, Kilimanjaro na Arusha.
Awamu ya kwanza ya utekelezaji wa Mradi wa SELF ilikwisha mwaka 2007. Hata hivyo kutokana na mahitaji makubwa ya huduma za kifedha yaliyoibuliwa na Mradi, Serikali bila ufadhili wa nje iliendelea kugharamia shughuli za Mradi, husasani uendeshaji. Mchango huu toka Serkalini pamoja na mapato ya ndani ya Mradi yaliwezesha SELF kuendelea kutekeleza shughuli zake kwa ufanisi mkubwa na mwaka 2009 mikoa 7 iliyokuwa imebaki kwa upande wa Tanzania Bara iliongezwa kwenye eneo la Mradi. Mikoa iliyoongezwa ilikuwa ni Manyara, Shinyanga, Tabora, Kagera, Kigoma, Rukwa na Dar es Salaam . Hivyo Mradi wa SELF ukawa unatekelezwa, mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani.
Mradi wa SELF umekuwa makini kutekeleza kwa vitendo majukumu yake kwa ufanisi mkubwa ili kutimiza malengo ya kuanzishwa kwake. Hali hii imechangiwa na jitihada za makusudi za SELF zilizofanywa katika kuutangaza Mradi, kuzihamasisha Asasi ndogo na za Kati za Fedha kuchukua mikopo yenye masharti nafuuu na kuzifanya ziwe na fikira ya kutoa huduma iliyo endelevu kwa kujenga uwezo wa kiutendaji kupitia mafunzo yanayotolewa na wataalamu waliobobea katika masuala ya uendeshaji na usimamizi wa fedha. Aidha vitendea kazi vinavyotolewa na Mradi vimekuwa ni motisha kwao ya kutoa huduma vizuri na kuboresha utendaji.
Leo hii SELF sio tu kwamba imekuwa ya kupigiwa mfano kutokana na sera zake zinazolenga kuleta maendeleo kwa watu maskini, bali pia kwa mafanikio iliyoyapata ambayo yanaifanya iwe mfano wa kuigwa miongoni mwa miradi inayosimamiwa na Serikali inayojishughulisha na utoaji wa huduma za Kifedha, pale ambapo taasisi rasmi, yaani Benki za biashara zimeshindwa kukidhi mahitaji kutokana na sera, sheria na taratibu za kibenki. Kimataifa SELF imejijengea umaarufu kutokana na kushika nafasi ya juu miongoni mwa miradi ya aina hii, inayofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Uzoefu na mafanikio yaliyopatikana katika awamu ya kwanza ya mradi yameiwezesha SELF kuingia katika awamu ya pili ya utekelezaji iliyoanza Julai 2010 na itamalizika Juni 2015. Katika awamu hii ya pili ya utekelezaji, Serikali inakusudia kuibadilisha SELF kutoka kuwa Mradi na kuwa taasisi inayojitegemea.
Katika kipindi cha miaka kumi na mitatu iliyopita, utoaji mikopo unaofanywa na SELF kwa Asasi za Fedha umepanda kwa kasi na kuweza kuwafikia wananchi wengi wa kipato cha chini waliopo mjini na vijijini kama inavyoonyeshwa kwenye jedwali hapo chini.
Kupanuka kwa Huduma za Kifedha Vijijini na Mjini
Mwaka | 02/03 | 03/04 | 04/05 | 05/06 | 06/07 | 07/08 | 08/09 | 09/10 | 10/11 | 11/12 | 12/13 |
1.Idadi ya Asasi za Kifedha | 21 | 39 | 70 | 71 | 56 | 186 | 155 | 203 | 301 | 323 | 364 |
2. Thamani ya mikopo kwa Asasi ‘’Tshs 000’’) | 665,450 | 1,513 | 3,465 | 2,733 | 3,769 | 3,283 | 5,752 | 6,859 | 9,014 | 10,248 | 9,843 |
3. Idadi ya wananchi waliokopeshwa | 7,083 | 12,325 | 20,526 | 37,364 | 54,058 | 60,016 | 65,809 | 73,025 | 80,454 | 88,083 | 93,364 |
4. Jamii iliyonufaika | 28,332 | 49,300 | 82,104 | 149,456 | 216,232 | 240,064 | 263,236 | 292,100 | 321,816 | 352,332 | 374,560 |
Hadi kufikia Juni 2013 tayari SELF ilikuwa imeshatoa mikopo yenye thamani ya bilioni 52.3 kwa asasi za kifedha zipatazo 364 (asilimia 60 kati ya hizo ni za vijijini). Mikopo hii imesaidia kukuza shughuli ndogo za kiuchumi na kunufaisha zaidi ya wateja wapatao 93,372 ambao kati ya hao 58% ni wanawake. Aidha, watu wapatao 374,560 kwa njia moja au nyingine wamenufaika na mikopo hii.
Mafunzo yanayotolewa na Mradi wa SELF kwa viongozi na watendaji wa asasi ndogo na za kati za fedha yanalenga kuwajengea uwezo juu ya utawala bora,usimamizi wa shughli za fedha na mikopo. Wajasiriamali wadogo wanaokopa toka asasi wabia wa SELF nao pia hupatiwa mafunzo ya ujasiriamali na stadi za biashara. Mafunzo haya yanalenga kuwaongezea ujasiri wa kuthubutu na kuongeza ubunifu katika biashara zao ili waweze kuwekeza vizuri kwenye mikopo wanayoipata kwa kuifanyia biashara kwa njia za kitaalamu zitakazo waongezea tija kwenye biashara zao.
Jedwali lifuatalo linaonyesha idadi ya wabia wa mradi walionufaika na mafunzo toka Mradi mradi ulipoanza hadi kufikia Juni 2013.
Idadi ya Viongozi, Watendaji wa Asasi za kifedha, Wajasiriamali wadogo na Watoa Huduma walionufaika na Mafunzo toka SELF.
Kundi | 2000 - 2009 | 2010 - 2013 | Jumla |
Viongozi na Watendaji wa Asasi za kifedha | 2,486 | 1,042 | 2,551 |
Wajasiriamali wadogo | 3,175 | 4,558 | 5,649 |
Watoa huduma (Maafisa Ushirika ngazi ya wilaya) | 208 | 180 | 240 |
Mradi wa SELF umekuwa ukihakikisha huduma za fedha zinazotolewa zinakuwa endelevu kwa wabia wake, ili wananchi wengi zaidi hasa maeneo ya vijijini waweze kunufaika na huduma za kifedha. Mradi wa SELF umekuwa ukihamasisha wabia wake kutoa huduma katika mazingira yaliyo bora, salama na yenye mvuto, ili wananchi wengi waweze kuhamasika na kujiunga kwenye huduma za kifedha.
Hadi kufikia mwezi June 2013, Mradi wa SELF tayari ulikuwa umetoa jumla ya T.sh. 75,374 milioni kwa asasi za fedha 68 inazoshirikiana nazo katika kuhakikisha huduma za kifedha zinawafikia wananchi kwa wingi zaidi, katika mazingira yaliyo salama na kisasa zaidi. Kiasi hicho kimeziwezesha asasi hizo kununua samani za ofisi, vitendea kazi kama vile kompyuta, mashine za kudurufu na kusikani karatasi, pikipiki, kasiki, baiskeli, kukarabati majengo pamoja na kuandaa mikutanao kwa ajili ya wanachama wao.
Mikopo inayotolewa kwa wabia wake pamoja na vitendea kazi vya ofisi wanavyopewa wabia wa SELF, umezifanya asasi hizi kuongeza ufanisi na kuimarisha utoaji huduma kawa katika viwango bora kabisa, na kuzifanya asasi hizo ziweze kukua toka kwenye kiwango cha chini cha utoaji huduma hadi kwenye kiwango cha kati, na zile asasi za fedha zilizo kuwa kwenye kiwango cha kati kukua na kufikia kiwango cha juu cha utoaji huduma.
Hadi kufikia mwezi June 2013, asilimia 12 ya wadau wanaoshirikiana na Mradi, wameweza kukua toka kiwango cha chini kabisa cha utoaji huduma hadi kiwango cha kati, wakati asilimia 3.4 ya asasi za fedha zilizo kwenye kiwango cha kati zimeweza kufikia kiwango cha juu kabisa cha utoaji huduma za mikopo. Asilimia 31 ya wadau wa kiwango cha chini, waliweza kuimarisha huduma zao ndani ya kiwango hicho na kuanza kutoa huduma bora zaidi kwa wanachama wake. Kukua huku ni muhimu, ili kuibua Asasi za kifedha endelelevu ambazo zitaendelea kutoa huduma bora za kifedha kwa jamii na hivyo kukuza uchumi na kuboresha maendeleo ya jamii nzima.
Akizungumza katika moja ya mafunzo ya kuwajengea uwezo Warajisi Wasaidizi na Maafisa Ushirika wa Mikoa ya Tanzania bara na visiwani, Katibu tawala wa Mkoa wa Pwani Ms. Beatha Swai, aliwataka Maafisa ushirika wa mikoa yote waongeze bidii katika kuwaelimisha viongozi wa SACCOS ili waweze kuzifahamu sheria za ushirika vizuri, hivyo kuweza kuimarisha utendaji na usimamizi wao wa kazi. “ Mnatakiwa msimamie vizuri Sheria ya Ushirika kwa viongozi wa SACCOS kwa kufuata misingi na kanuni za ushirika, ili kuongeza uelewa kwa viongozi wa SACCOs ili waweze kusimamia shughuli zao vizuri”
Bw. Abdulhaman Mohamed Hassani, ambaye ni Katibu Mkuu wa taasisi ya kutoa mikopo ya Jumuiya ya Changamoto ya Unguja (Changamoto Life Preservation Fund), iliyoanzishwa kwa lengo la kutoa huduma mbalimbali kwa jamii ya Saateni na maeneo yanayozunguka; anasema kwamba; awali taasisi ilisajiliwa kama chama cha kuweka akiba na kukopa (SACCOS). Lakini kufuatia utendaji mzuri na uhitaji mkubwa wa huduma za kifedha uliokuwepo , uongozi uliamua kuongeza wigo wa kutoa huduma na kuamua kubadilisha usajili wa SACCOS, na kuwa chama cha kijamii mwaka 2007. Anasema Mradi wa SELF umeweza kukidhi mahitaji ya asasi yao kwa kuongeza mtaji kupitia mikopo wanayoichukua SELF. Anaendelea “…..kutokana na kuongozeka kwa mtaji tumekuwa tukitoa mikopo kwa wakati kwa wanachama wengi zaidi tofauti na hapo awali, hivyo kuwafanya wanachama wetu kufanya biashara kwa uhakika zaidi kwa kujiamini. Ajira 2,700 zimeweza kupatikana baada ya wajasiriamali kuweza kupanua biashara zao”
Bw. Abdulhaman Mohamed Hassani anaelezea jinsi mafunzo yaliyotolewa na Mradi wa SELF kwa viongozi, na wajasiriamali wa asasi yao, yalivyoboresha na kuongeza ufanisi wa utendaji kwa viongozi na kuwafanya kuongeza nidhamu ya fedha, kitu kilichokuwakikwazo kikubwa katika usimamizi wa asasi yao hapo awali, “……kwa upande wa wajasiriamali, mafunzo ya ujasiriamali kuhusu stadi za biashara, usimamizi wa biashara na elimu ya ujasiriamali, yamewaongezea ujasiri mkubwa wa kuthubutu na kuwa wabunifu katika biashara, hali inayowafanya waweze kusimamia biashara zao kwa kujiamini”
“Vile vile SELF imetusaidia kukarabati ofisi yetu, imekuwa ya kisasa na kuvutia zaidi; hali inayotufanya tuaminike na kutambulika kwa wadau wengi zaidi. Nawashauri wananchi wajiunge kwa wingi kwenye taasisi za kifedha, ili waweze kunufaika na mikopo ya masharti nafuu, ni vigumu kufikiwa na huduma za kifedha kwa mtu mmoja mmoja’’, anasema Bw. Abdulhaman Mohamed Hassani.
Bw. Ally Adam Ally ni Mwenyekiti wa Serena SACCOS, ambayo imekuwa miongoni mwa wanufaikaji wa huduma za fedha toka Mradi wa SELF. Yeye anasema, katika maeneo yote ambako SELF imewafikia wananchi, imekuwa mkombozi mkubwa kwao hasa kutokana na kutoa mikopo yenye masharti na riba nafuu inayowawezesha watu wa kipato cha chini kuimudu.
Anasema tofauti na asasi nyingine za kifedha kama benki na kampuni binafsi ambazo huweka masharti magumu yanayohitaji dhamana, SELF imejidhirisha kuwa tofauti kabisa na asasi hizo.
“Tumeweza kuboresha maisha yetu tofauti na awali, kupitia mikopo ya SACCOS yetu, tumeweza kuboresha maisha yetu, tumenunua vyombo vya moto kama pikipiki, magari na kuboresha makazi yetu kwa kupitia mikopo, vilevile ada za watoto na zetu sisi wenyewe zimekuwa zinapatika kwa urahisi sana tofauti na awali”, anasema Mwenyekiti Ally Adam Ally.
Akizungumza na Majira katika mahojiano maalum, Meneja wa Mradi wa SELF Bw. Abiah Kaaya, anasema pamoja na mafanikio ambayo SELF imeyapata katika kipindi cha takribani miaka kumi na tatu tangu kuanza huduma zake, bado kumekuwa na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa kikwazo katika kutekeleza na kutimiza malengo ya Mradi wa SELF.
‘’Utoaji wa huduma za Kifedha kwa wananchi wa kipato cha chini ni dhana iliyoshamiri miaka ya karibuni hapa Tanzania; Asasi zinazofanya shughuli hii zimejikita zaidi mijini na kwenye maeneo yenye shughuli kubwa za kipato. Aidha upatikanaji wa huduma hizi katika maeneo ya vijijini umekuwa bado uko katika kiwango cha chini, ambapo huwa ukifanyika kwa utaratibu ambao si rasmi kutokana na kutokuwepo kwa Asasi zinazotambulika kisheria.
Aidha, kwenye maeneo ambayo kuna Asasi za kifedha zinazotoa huduma, kutokana na udhaifu wa kiutendaji, hususan upungufu wa wafanyakazi wenye ujuzi utoaji wa huduma ni duni na hazikidhi matakwa ya walengwa. Wafanyakazi wenye ujuzi mdogo wamelazimika kuwa na majukumu mengi kwa wakati mmoja tofauti kabisa na uwezo wao, utawakuta wakati mwingine wakifanya kazi kama Mameneja, Maafisa Mikopo na Wahasibu. Katika utendaji kazi wa aina hii, udhibiti na utunzaji wa fedha umekuwa tatizo kubwa; ni dhahiri kabisa kwa asasi za aina hii kukabiliwa na hatari kubwa ya kushindwa kutoa huduma zilizo endelevu kwa sababu ya zisizoridhisha zitolewazo na wafanyakazi wasio na uzoefu, hali hii inapelekea kupoteza pesa’’, anaeleza Meneja wa Mradi.
Anaeleza kuwa changamoto nyingine inayozikabili Asasi za kifedha ni wananchi kuwa na uelewa mdogo juu ya masuala kifedha, yahusuyo mikopo, akiba, riba n.k.; hivyo kushindwa kutoa maamuzi sahihi kuhusu dhana nzima ya matumizi ya akiba na mikopo, ili kuongezea kipato na hivyo kujikwamua kiuchumi. Aidha, mapungufu ya elimu hii, inafanya wananchi kushindwa kufanya tathmini ya fursa zilizopo ili kuzitumia vizuri kwa manufaa yao. Kuondokana na changomoto hii, Meneja wa Mradi wa SELF anashauri asasi za fedha ziwe zinatoa elimu kwa wateja, wanachama na wananchi, ili waweze kuwa na uelewa mkubwa wa namna ya kutumia mikopo hiyo vizuri na kuwafanya wafanye shughuli kwa malengo na mitizamo iliyo endelevu. Kwa upande wa viongozi wa asasi za fedha, baadhi yao wamekuwa na uelewa mdogo wa masula ya kifedha, hali inayowafanya washindwe kubuni vyanzo vingine vya mapato vilivyo imara na kutegemea zaidi vyanzo vilivyopo tu. Viongozi na watendaji hawana budi kuelewa kuwa kuendelea kuwepo kwa asasi zao kutategemea zaidi uwezo wao wa kubuni mikakati itakayoziwezesha Asasi za fedha kuwa endelevu. Mikakati hiyo ni pamoja na kupanua wigo wa eneo na huduma wanazotoa, kubuni vyanzo vipya vya mapato, kudhibiti gharama za uendeshaji, kuboresha urejeshwaji wa mikopo na kudumisha uongozi bora.
Anaendelea kueleza kuwa, tabia na mawazo potovu yatokanayo na mila na desturi kuhusu mikopo, hasa ile itolewayo na Serikali imekuwa changamoto kubwa inayofanya viwango vilichokusudiwa na Serikali, vya kuifikishia mikopo jamii pale ilipo hasa sehemu za vijijini, visifikiwe. Vilevile kuna desturi kwa baadhi ya jamii kuona mikopo kama chombo kinachodhalilisha au chombo kinachotumika kuwakandamiza na kuwarudisha nyuma kimaendeleo, pindi wanaposhindwa kulipa mikopo kwa wakati.
Utawala mbovu wa baadhi ya viongozi wa Asasi za kifedha, ambao umekuwa hauzingatii misingi ya utawala bora, usiofuata utaratibu uliowekwa wakati wa uchaguzi na usio zingatia huru na haki kwa viongozi wengine umekuwa changamoto kubwa ya kuhakikisha huduma za kifedha zinatolewa katika mzingira huru na ya haki. Viongozi wamekuwa wakiingilia kazi za meneja na kuwafanya wafanye kazi katika mazingira magumu, yasio huru hivyo kushindwa kusimamia majukumu yao vizuri, hiyo ni mojawapo ya changomoto zinazoelezwa na Meneja, kwa asasi za fedha.
Anataja changamoto nyingine inayozikabili Asasi za kifedha kuwa ni kutumiwa vibaya fursa ya kuwepo kwa taasisi mbalimbali zinazotoa mikopo. ‘Lipo tatizo kwa baadhi ya Asasi za fedha kutumia vibaya fursa ya kuwepo kwa taasisi nyingi zinazotoa mikopo kwa kuchukua mikopo mingi kwa wakati mmoja toka kwa wakopeshaji tofauti kuliko uwezo wake wa kuitumia na kuisimamia, hivyo kuwa na mikopo mingi isiyolipika hali ambayo inapunguza ufanisi na uendelevu wa asasi hizo’’. Anasema juhudi za Serikali za kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapewa kitambulisho cha utaifa, ambazo zinaendelea sasa, pamoja na kuanzishwa chombo kitakachokusanya taarifa za wakopaji (credit bureau), vitatoa ufumbuzi wa tatizo hili; kwa sehemu kubwa.
Meneja wa Mradi wa SELF, anawashauri wananchi waache kuwa na mawazo potofu, na wajiunge kwa wingi kwenye asisi za fedha zinazotoa mikopo yenye riba nafuu, ili waweze kunufaike na mikopo hiyo kuwafanya washiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishajimali, na kuongeza vipato miongoni mwao na kutengeneza ajira nyingi zaidi kwa wananchi.