BAADA ya kupotea kwa miaka mingi, hatimaye ligi ya mpira wa miguu kwa timu za wachezaji wanawake Zanzibar inatarajiwa kurudi viwanjani leo.
Katiba wa soka la wanawake Zanzibar Laila Said, amewaambia waandishi wa habari kuwa pazia la ligi hiyo inayoshirikisha jumla ya timu sita, litafunguliwa katika uwanja wa Amaan mnamo saa 10:00 jioni.
Alisema timu zinazotarajiwa kufungua dimba ni New Generation Queens ya mtaa wa Kwahani, itakayorushana roho na Mwenge Sisters kutoka Makunduchi.
Timu nyengine zinazoshiriki ligi hiyo ni Women Fighters, Bungi Sisters, Kidimni Sisters pamoja na Mkoani Stars kutoka kisiwani Pemba, ambayo hata hivyo haitakuwepo kwenye sherehe za ufunguzi kwa kuwa itachelewa kufika Unguja.
Hata hivyo, Laila alisema mechi nyengine zote zitakuwa zikichezwa uwanja wa Mao Tse Tung wakati wa saa 8:00 na saa 10:00 jioni.
Katika ligi hiyo iliyopangwa kumalizika Januari 26, mwaka huu, mgeni rasmi anatarajiwa kuwa mke wa Makamu wa Pili wa Rais, Asha Suleiman Iddi.