Na Haji Nassor, PEMBA
WATU nane wakiwemo mabaharia wanne, wamenusurika kifo baada ya jahazi walilokuwa wakisafiria kutoka Tanga kwenda Wete Pemba, kukumbwa na upepo mkali na kulazimika kumwaga mzigo waliokua wamepakia.
Kadhia hiyo iliwakumba jana majira ya saa 8:50 jioni, wakati jahazi hiyo ikiwa imebeba bidhaa za aina mbali mbali za wafanyabiashara wa miji ya Pemba.
Baadhi ya mabaharia waliokuwemo kwenye chombo hicho, walisema waliondoka bandari ya Tanga wakiwa salama na kwamba mzigo waliobeba ulikuwa wa kawaida, lakini hali ilibadilika kadiri safari ilivyoendelea.
Walisema walibeba matenga ya tungule 300, viazi mbatata gunia 30, vituguu maji gunia 40, magodoro 30 pamoja na vitu vyengine vidogo vidogo kama mafuta ya kupikia, madumu, misumari na mapipa matupu.
Mmoja kati ya mabaharia hao aliejitambulisha kwa jina moja la Mohamed (Mudi) alisema, wakati wako nusu ya safari yao, ulitokezea upepo usio wa kawaida na kuliyumbisha jahazi lao.
Alisema baada ya kuona jahazi linayumba mara tatu mfululizo, nahodha alitoa agizo kali la kuwataka mabaharia wamwage mzigo kupunguza uzito.
Nae abiria aliekuwemo kwenye chombo hicho, Nd. Ali Khamis Juma, akizungumza kwa njia ya simu alisema, zaidi ya matenga 25 ya tungule, madumu ya mafuta, baadhi ya viroba vya misumari vilitupwa baharini.
“Taharuki haikuwa ndogo, lakini kutokana na tuliokuwemo kwenye jahazi ni watu wa bahari, tulijua nini tufanye, na tukaanza kumwaga mzigo taratibu hadi utulivu ulipopatikana,’’ alisema.
Baadhi ya mashuda wengine waliokuwemo kwenye jahazi hilo walidai kuwa, mzigo ulikuwa umezidi uwezo wa jahazi hilo na ndio maana, baada ya kubakia mzigo wake wa kawaida safari iliendelea.
Kamanda wa Polisi mkoa wa kaskazini Pemba,Sheikhan Mohamed Sheikhan, alisema taarifa za tukio hilo bado hazijafika ofisini kwake.
Hivi karibuni watu watano walihofiwa kufa, baada ya boti ya Mv. Kilimanjaro II waliokuwa wakisafiria, kukumbwa na dhoruba ilioambatana na upepo mkali, katika eneo la mkondo wa bahari ya Nungwi, wakati ilipokuwa ikitokea bandari ya Mkoani kwenda Unguja.
Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania (TMA) na Mamlaka ya usafiri baharini Zanzibar ZMA, katika kipindi cha miezi miwili mfululizo sasa, imekua kikitoa taarifa za tahadhari kila siku kupitia vyombo vya habari juu ya kuwepo kwa upepo mkali katika bahari ya Hindi.