Na Fatuma Kitima, DSM
TAKWIMU zinaonesha kumekuwa na ongezeko la matukio 264 ya ajali za barabarani kwa mwaka jana ambapo ni sawa na asilimia 1.1, ikilinganishwa na mwaka 2012 ambapo matukio yalikuwa 23,578.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga, alitaja maeneo aliyoongoza kwa ajali ni Kinondoni,Ilala, Temeke Kilimanjaro na Pwani.
Alisema ajali zilizosababisha vifo kwa mwaka 2013 ni 3,427 sawa na ongezeko la asilimia 3.0 ikilinganishwa na mwaka 2012 ambapo kulikuwa na vifo 3,328.
Alisema kuwa ajali zilizosababisha majeruhi kwa kipindi hicho ni 11,307 sawa na ongezeko la asilimia 2.6 ikilinganishwa na mwaka 2012 ambapo kulikuwa na majeruhi 11,021.
Alianisha kuwa kumekuwa na ongezeko la vifo 33 sawa na asilimia 0.8 kwa mwaka jana ikilinganishwa na idadi ya mwaka 2012 ambapo kulikuwa na vifo 3,969, hata hivyo kumekuwa na ongezeko la majeruhi 578 kwa mwaka 2013 sawa na asilimia 2.9 tofauti na mwaka 2012 ambapo kulikuwa na majeruhi 20, 111.
Alisema kuna baadhi ya mikoa ambayo imepunguza idadi ya ajali ikiwa ni Arusha, Mwanza,Mbeya na Morogoro.
Alibanisha kati ya makundi hayo, ajali za pikipiki zimeongoza kwa ajali nyingi ambapo takwimu zinaonesha idadi ya ajali kwa mwaka 2013 ni 6,831 sawa na asilimia 18.5 tofauti na mwaka 2012 ambapo kulikuwa na ajali 5,763.
Alisema idadi ya ongezeko la vifo vilivyotokana na pikipiki kwa mwaka 2013 ni 168 sawa na asilimia 18.1 ambapo mwaka 2012 kulikuwa na vifo 930, hata hivyo kwa mwaka 2013 kumekuwa na ongezeko la majeruhi 1,046 sawa na asilimia 19 ambapo mwaka 2012 kulikuwa na majeruhi 5,532.
Kutokana na ongezeko hilo polisi imepanga mikakati mbalimbali ya kupunguza ajali za barabarani kwa mwaka 2014 ambazo ni ushirikishwaji kwa jamii na elimu kwa umma ambapo watapanua wigo wa utoaji elimu kwa umma ikiwa ni pamoja na kuboresha mipango katika vipindi vya redio na televisheni.
Aidha alisema kutakuwa na uthibiti wa makosa ikiwa ni pamoja na kuongeza ukamataji wa madereva wasiopenda kutii sheria bila shuruti, matumizi ya liseni mpya kudhibiti mienendo ya madereva na kuongeza matumizi ya teknolojia na mawasiliano.