Na Mwashamba Juma
CHINA inatarajia kuinufaisha Zanzibar katika sekta ya viwanda na utalii ili kuimarisha uchumi wake na kuinua uhusianao wakidugu baina ya nchi hizo mbili.
Kauli hiyo imetolewa na ujumbe wa watu 21 kutoka China uliokuja Zanzibar kwa ziara ya siku moja kwa lengo la kuanzisha uhusiano wa kibiashara baina ya nchini mbili hizo hasa katika sekta za maendeleo ikiwemo uvuvi na utalii.
Ujumbe huo ulikuwa ukizungumza na Waziri wa Fedha, Mhe. Omar Yussuf Mzee ofisini kwake Vuga mjini Zanzibar.
Kiongozi wa ujumbe huo, rais wa kampuni ya China Beobei International Investment Group, Bian Hongdeng, alisema ziara yao imewavutia zaidi katika uvuvi wa bahari kuu ya Zanzibar ambapo wataleta meli kubwa za uvuvi na kujenga kiwanda cha samaki ili kukuza sekta ya uvuvi nchini.
Akizungumzia sekta ya utalii, alisema Zanzinar ni kisiwa kizuri kwa utalii hivyo tayari wamezungumza na shirika la ndege la Hainan la China ili kuleta watalii wengi Zanzibar watakaoingia moja kwa moja wakitokea China.
Alisema pia wanatarajia kujenga hoteli kubwa yenye hadhi ya nyota tano itakayotoa huduma zinazolingana na utamaduni wa China, sambamba na kutoa nafasi 10 kwa Wazanzibari kwenda China kusoma kichina kwa ajili ya kufanyakazi na wachina wakiwa Zanzibar.
Ujumbe huo pia umezungumzia ujenzi wa chuo cha utalii kitakachotoa taaluma ya utalii kwa Wazanzibari ili kuimarisha sekta hiyo.
Wakizungumzia maendeleo mengine, walisema wanatarajia kujenga bandari ndogo katika kijiji cha Unguja Ukuu, ambako walipata tetesi ya kukaliwa na Wachina katika karne zilizopita.
Kujengwa kwa bandari hiyo kutarudisha hisroria zilizopita pamoja na kuimarisha uhusiano wa kirafiki baina ya Zanzibar na China.
Kwa upande wake Waziri wa Fedha, Mhe. Omar Yussuf Mzee, alisema miradi hiyo itakapotekelezwa Zanzibar itapiga hatua kubwa kimaendeleo na kukuza uchumi wake.
Alisema serikali itapunguza ushuru kwa sekta ya viwanda ili kuwapa nafasi wawekezaji wengi kuwekeza katika sekta hiyo.
Alisema ni wajibu wa serikali kutafuta nafasi za uwekezaji nchini kwa maendeleo na maslahi ya nchi na watu wake.
Ujumbe huo ulikuja kufuataia ziara ya Mhe. Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Muhamed Shein aliyoifanya China mwaka uliopita.