Kauthar Abdalla na Salum Simba, MUM
WAZIRI wa Katiba na Sheria, Mhe. Aboubakary Khamis Bakary, amesema kumekuwa na migogoro mingi misikitini inayosababishwa na michango inayoingia kutoka vyanzo mbali mbali, ikiwemo vitega uchumi.
Aidha alisema migogoro mengine inasababisha na tofauti za kifikra, elimu na mitazamo.
Akiwasilsha ripoti ya utekelezaji wa maagizo ya kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ya Baraza la Wawakilishi ya mwaka 2012/2013, Waziri huyo alisema, hata hivyo wamechukua juhudi kuonana na viongozi wa misikiti kwa kushirikiana na taasisi ya World Islamic Call Society kutoka Libya.
Kuhusu uajiri katika ofisi ya Msajili wa Hakimiliki, alisema wizara imeajiri watendaji watatu na tayari wameshaanza kazi katika mwaka wa fedha 2013/2014.
Aidha alisema wizara bado inaendelea na juhudi za kupata hakimiliki za jengo la taasisi hiyo kisiwani Pemba kwa sababu haipo na hata baada ya kufuatilia wizara inayoshughulika na ujenzi imekosekana.
Akiwasilisha ripoti ya Kamati hiyo, Mwenyekiti wake, Mhe.Ussi Jecha Simai, alisema kamati imepata taarifa za kusikitisha kuhusu wizi wa nyaraka muhimu uliotokea katia idara ya nyaraka.
Alisema wizi huo umekuja kutokana na kutokuwepo kamera za usalama (CCTV) ambayo licha ya kupigiwa kelele muda mrefu wizara imeshindwa kuweka kamera hizo hadi wizi huo ulipotokea.
Akigusia Tume ya Kurekebisha Sheria, Mwenyekiti huyo aliitaka serikali kutilia mkazo suala la upatikanajai wa jengo la ofisi pamoja, ufinyu wa bajeti na kuongeza maslahi ya watumishi wa tume hii kwa sababu wanafanya kazi ngumu.
Kwa upande wa ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, alisema watumishi wanne wameshakimbia ambao wamehamia taasisi nyengine kufuata maslahi bora.
Aidha aliishauri serikali kuyafanyia ukarabati majengo ya Idara ya mahakama ambayo yanaonekana kuchakaa na kujipanga kujenga mengine mapya.
Kamati hiyo ilisikitishwa na vitendo vya baadhi ya majaji kupuuza taratibu zilizopo kwenye sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai, ambapo baadhi yao ni wale waliolalamikiwa na Jumuiya ya Wanasheria Zanzibar (ZLS) baada ya kuteuliwa na Rais mwaka 2010.
Alisema hoja kuwa ni uwezo wao mdogo na wengineuadilifu wao katika kuendesha mashauri mbali mbali ni wa mashaka.
Alisema yapo mashauri mengi katika mahakama za watoto ambayo yalipelekwa muda mrefu bila kusikilizwa na mengine kufutwa kutokana na wazee kuchoka kusubiri.
« Lipo shauri limefutwa kwa sababu mtoto aliyefanyiwa udhalilishaji ameshafikia umri ambao ni zaidi ya umri aliokuwa nao wakati akifanyiwa udhalilishaji na mzee wake kuamua kutoendelea na kesi hiyo, » alisema.
Alisema pia yapo makosa ya ubakaji na udhalilishaji kijinsia yaliyopewa hukumu ambazo zipo kinyume na sheria, ikiwemo mshitakiwa kulipishwa faini ya shilingi 400,000 ambapo muathirika alipewa shilingi 100,000.
Wakichangia, wajumbe wa baraza la Wawakilishi wameiomba serikali kuweka mahakama maalum za kusikiliza kesi zinazohusiana na migogoro ya wawekezaji ili kutoa uhuru zaidi wa kuendesha kesi hizo.
Aidha walisema idara ya mahakama inategemewa zaidi kutoa haki hivyo mahakimu na majaji watoe hukumu kwa mujibu wa sheria.
Mwakilishi wa Kitope, Mhe. Makame Mshimba Mbarouk, alisema kumekuwa na malalamiko mengi kwamba mahakama hazitekelezi majukumu yake ipasavyo hali inayosababisha kuongezeka migogoro.