Na Miza Kona -Maelezo Zanzibar
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeombwa kuipatia fedha Wizara ya Kilimo na Maliasili kwa ajili ya kulipa deni wanalodaiwa na wakulima wa mbegu za mpunga nchi
Akiwasilisha Ripoti ya Kamati ya Fedha Biashara na Kilimo katika Ukumbi wa Baraza La Wawakilishi Chukwani, Mwenyikiti wa Kamati hiyo Salmin Awadh Salmin amesema Wizara hiyo inadaiwa jumla ya sh milioni 240 na wakulima wanaozalisha mbegu za mpunga katika mabonde mbalimbali ya kilimo hicho.
Alifahamisha kuwa wakulima hao wanadai fedha hizo zaidi ya miezi minne hali inayopelea kurudisha nyuma maendeleo ya kilimo hicho na kukosa kujikimu kimaisha.
“Kamati ilielezwa kuwa wakulima wa mikataba wanaozalisha mbegu za mpunga katika mabonde mbali mbali wanaidai Wizara jumla ya Tsh milioni 240 baada ya Wizara kuchukua mpunga huo bila ya kuwalipa kwa zaidi ya miezi minne ambapo wakulima wa bonde la Mtwango pekee wanadai Tsh milioni 60,” aleleza Mwenyekiti huyo.
Ameeleza kuwa tatizo hilo linaweza kuathiri uzalishaji wa mbegu hizo za mpunga kitendo ambacho kinawavunja moyo wakulima na kuathiri kilimo hicho.
Aidha Mhe Salmin ameitaka Wizara hiyo ya Kilimo na Maliasili kukipatia mtaalam wa maabara ya Mifugo na ulinzi wa uhakika Chuo cha Kilimo kiliopo Kizimbani ili kiweze kufanya kazi zake kwa ufanisi.
Akichangia Ripoti ya Kamati hiyo Mwakilishi wa Viti maalum Asha Bakari Makame ameiomba Serikali kuweka Benki ya mikopo kwa wakulima kutokana na asilimia kubwa ya wazanzibari ni wakulima ili waweze kujikimu wakati wanapopata shida.