Na Miza Kona- Maelezo
Wizara ya Fedha imesema inaendelea kutoa taaluma ya uwekezaji kwa wananchi na kuhakikisha kuwa migogoro ya ardhi kati ya wawekezaji na wananchi inaondoka nchini.
Akiwasilisha Ripoti ya Utekelezaji wa Maagizo ya Kamati ya Fedha Biashara na Kilimo katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Waziri wa Fedha Omar Yussuf Mzee amesema kuwa serikali tayari imeanza kufanya utafiti kwa lengo la kufahamu kiini cha migogoro hiyo.
Amesema serikali kupitia Mamlaka ya Ukuzaji na Uendelezaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) inatoa taaluma ya uwekezaji na kuhakikisha utaratibu wa kuwalipa fidia wananchi unakuwa wazi na wenye kueleweka.
Aidha amewahimiza wananchi kutunza mazingira kwa lengo la kuhifadhi mandhari ya mji wa Zanzibar na kuwa kivutio kikubwa cha watalii.
Hata hivyo Waziri huyo amesema Wizara yake imo katika hatua za mwisho za kukamilisha marekebisho ya sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kuhakikisha kuwa Mfuko huo unamwezesha mwanachama kutumia mchango wake kama dhamana kwa lengo la kumpatia mkopo.
Aidha amefahamisha kuwa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) inafanya mawasiliano na Mamlaka ya Mapato Kenya (KRA) ili kupata taarifa sahihi za viwango vya mafuta kutoka Mombasa kinachoingizwa nchini pamoja na kushirikiana na Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo KMKM kufaya doria katika sehemu mbali mbali za bahari kwa lengo la kudhibiti magendo ya mafuta.
Ameeleza kuwa serikali kwa kushirikana na wamiliki wa hoteli tayari imeanza maandalizi ya ulinzi katika maeneo mbali mbali kwa lengo la kuondosha uhalifu katika maeneo ya utalii.