Na Mohammed Muhina
Maafisa na Askari wa Jeshi la Polisi hapa nchini wametakiwa kuendelea kuainisha kero na changamoto zinazowakabili ili zichukuliwe hatua kwa lengo la kuboresha na kuimarisha utendaji kazi wa Jeshi hilo.
Agizo hilo limetaolewa jana na Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Hamdani Omari Makame, wakati akizungumza na Maafisa na Askari Polisi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Kamishna Hamdani alikuwa katika ziara ya kujitambulisha kwa Askari na viongozi wa Kiserikali tangu alipoteuliwa na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Rais Jakaya Kikwete, kushika wadhifa huo.
Kamishna Hamdani amesema kazi yake ya kwanza ni kukusanya taarifa, malalamiko na kero mbalimbali za Askari na maafisa ili kuangalia jinsi ya kuzitatua.
Amesema hadi sasa tayari ameshayapatia ufumbuzi matatizo kadhaa yakiwemo ya Askari kukosa mishahara kwa kipindi kirefu.
Hata hivyo Kamishna Hamdani amewataka Maafisa na Askari kuweka mbele uzalendo na kuangalia masuala ya msingi ikiwa ni pamoja na kuimarisha usalama katika miundombinu ya Utalii kwa kuzingatia taratibu na sheria za nchi.
Amesema Utalii kwa upande wa Zanzibar ni moja ya sekta inayoiingizia serikali zaidi ya Aslimia 80 ya fedha za kigeni na hivyo ni muhimu kuhakikisha kuwa maeneo ya utalii na watalii wanaoingia visiwani humo wanakuwa salama.
Nao baadhi ya Askari wameshauri kuwepo na mabadiliko ya kimfumo na kwamba askari wapya wanapomaliza mafunzo yao ya awali katika chuo cha Taaluma ya Polisi Moshi, wasipangiwe kufanyia kazi katika maeneo walikozaliwa kwani kwa kufanya hivyo ni kuzorotesha utendaji wa kazi za Polisi.
Konstebo Marwa Range, wa FFU Finya na Koplo Hamisi Shoka, wa Wete, wamesema kama askari wanapohitimu mafunzo yao ya awali watapangiwa mikoa pasipo kujali mkoa ama wilaya alikozaliwa, kutasaidia kuimarisha utendaji wa kazi za Polisi na kudumiasha nidhami.
Awali akitoa taarifa ya hali ya Usalama, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba ACP Mohammed Shahani, alisema matukio ya uhalifu yamepungua kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na siku za nyumba.
Kamanda Shahani amesema kupungua kwa makosa katika mkoa huo kunatokana na juhudi zinazofanywa na Askari wake kwa kushirikiana na Wananchi kupitia mpango wa Ulinzi Shirikishi.
Amesema kupitia mpango huo, Jeshi la Polisi limekuwa likipata taarifa nyingi za kihalifu na kuchukuliwa hatua kabla ya kutokea na hivyo kuongeza kuimarika kwa hali ya Ulinzi na Usalama katika mkoa huo.