Na Mwandishi wetu
KAMATI ya Bunge ya Miundombinu imefanya ziara ya kutembelea barabara zinazotarajiwa kuanza kujengwa pembezoni mwa jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kupunguza msongamano.
Kamati hiyo ambayo ilifanya mazungumzo na Waziri wa Ujenzi na watendaji wa wizara, ilikuwa ilikagua miradi inayotekelezwa na wakala wa barabara Tanzania (Tanroads) katika mkoa wa Dar es Salaam.
Akizungumza na wajumbe wa kamati hiyo, Waziri wa Ujenzi, Mhe. Dk. John Magufuli, alisema mbali na utekelezaji wa miradi mbali mbali mikubwa ya maendeleo jijini Dar es Salaam, pia upo mradi maalum wa kupunguza msongamano kwa kuimarisha barabara zilizoko pembezoni mwa jiji ambazo ni viungo muhimu kwa barabara kuu zinazoingia na kutoka mjini.
Alisema katika awamu ya kwanza tayari jumla ya kilometa 22 kati ya kilometa 78.9 za barabara hizo zimejengwa.
Barabara hizo ni kuanzia kituo cha mabasi Ubungo kupitia Kigogo hadi barabara ya Kawawa (km 6.4) na kutoka makutano ya barabara ya Kigogo kupitia bonde la Msimbazi hadi makutano ya mtaa wa Jangwani na Twiga (km 2.72).
Alisema barabara nyingine ni Jet Corner–Vituka– Devis Corner (km 12) na Ubungo Maziwa-Mabibo External Mandela yenye urefu wa kilimota 0.64.
Alisema katika mwaka huu wa fedha 2013/2014 jumla ya kilometa 27.2 zitaanza kujengwa ikiwa ni awamu ya pili ya mpango huo.