Na Kija Elias, MWANGA
SERIKALI inatarajia kuanzisha mradi mkubwa wa maji katika kijiji cha njia panda Kirya, wilaya ya Mwanga Mkoani Kilimanjaro, unaokadiriwa kugharimu shilingi bilioni 32.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe,wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha njia panda Kirya katika maadhimisho ya miaka 37 ya CCM, iliyofanyika kiwilaya katika kijiji cha Kirya na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho.
Alisema mradi huo unatekelezwa na wadau mbalimbali ikiwemo Benki ya Falme za Kiarabu (BADEA) na kwamba serikali kwa kutambua tatizo la maji inaboresha miundombinu katika vyanzo vya maji ili wananchi waweze kupata huduma hiyo, na kumaliza kero ya maji katika wilaya ya Mwanga, Same na Korogwe.
Alisema mradi huo ambao ni wa taifa, utahusisha ujenzi wa mtambo mkubwa wa maji katika kijiji cha Njia panda Kirya ambapo serikali imepanga kuleta kampuni ya kusambaza maji itakayofanya kazi ya kusukuma kutoka vyanzo vya maji hadi maeneo yanayokabiliwa na tatizo hilo.
"Serikali imedhamiria kumaliza matatizo ya maji, kwa hapa njia panda tunaleta kampuni ya kusambaza maji kijijini kwenu, kuna mradi mkubwa wa maji wa taifa ambao utaanzishwa hapa Mwanga na naamini tukifanikiwa tutakuwa tumetatua kero ya maji kabisa," alisema.
Aidha alisema maji hayo yatahifadhiwa katika tenki kubwa litakalofungwa mtambo wa kusafisha maji kabla ya kuyasambaza katika vijiji vyngine vyenye mahitaji ya maji.
Aliongeza kuwa mkondo mwengine utasukuma maji hayo kutoka katika kijiji cha Njia panda Kirya hadi Kisangara ambapo maji hayo yatapandishwa katika milima ya Kiverenge na wakati huo huo kukiwa na mkondo mrefu ambao utafanya kazi ya kusukuma maji hadi wilaya ya Same.
Alisema vijiji ambavyo vinatarajia kunufaika na maji safi na salama ni Handeni, Bora, Kagongo, Nyabinda Mvungu, Mangulai, Kirya, Kisangara, Makanya na Kisangara.
Aliwataka wananchi kuchukulia miradi yote inayoanzishwa na serikali kama urithi wao huku akihamasisha umuhimu wa kutunza mazingira kwa manufaa ya vizazi vya baadae.
Kwa upande wake, mjumbe wa kamati ya siasa ya mkoa wa Kilimanjaro, Paul Matemu, alisema vyama vya upinzani ni makundi ya wanaharakati na kamwe hayawezi kuingia ikulu mwaka 2015 kama ambavyo yamekuwa yakijinadi katika mikutano mbalimbali nchini.
Alisema vyama hivyo haviwezi kufikia hatua ziliyofikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutokana na vyama vingi kujihusisha na makundi ya wanaharakati ambayo yamekuwa yakiwashawishi vijana kuhamasisha machufuko.
Alisema katika sherehe za kuadhimisha miaka 37 ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi, kinajivunia misingi imara ambayo iliasisiwa tangu zamani na hayati Julius Kambarage Nyerere na hayati Abed Amani Karume.