Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Hutuba ya Makamo wa Pili wa Rais ufungaji wa Baraza.

$
0
0
HOTUBA YA MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR, MHE. BALOZI SEIF ALI IDDI KATIKA UFUNGAJI WA MKUTANO WA
KUMI NA TANO WA BARAZA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR,
TAREHE 5 FEBRUARI, 2014

                       Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi. 



1.0         Utangulizi:

1.1         Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu na mwingi wa rehema, kwa kutujaalia uzima na afya njema na kutupa nguvu za kuweza kutimiza majukumu yetu yote tuliyojipangia katika kipindi hiki kwa salama na amani. Pili, nikushukuru wewe Mheshimiwa Spika pamoja na Wasaidizi wako kwa kuuongoza Mkutano wa 15 wa Baraza letu kwa umakini, busara, na hekima kubwa.   Nawashukuru Mhe. Naibu Spika na Wenyeviti wa Baraza la Wawakilishi kwa msaada mkubwa waliokupa katika kuliendesha Baraza hili tukufu kwa mafanikio makubwa na kumaliza shughuli zake salama.

1.2         Mheshimiwa Spika, pia nawashukuru kwa dhati Wenyeviti wote wa Kamati za Kudumu za Baraza kwa kuziongoza Kamati zao na kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa.

1.3         Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kumpongeza sana Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa uongozi wake imara ambao unaendelea kutupatia mafanikio makubwa ya kimaendeleo katika nchi yetu katika nyanja zote. Ushauri, maelekezo na miongozo yake inatusaidia sana katika kutekeleza majukumu yetu ya kuwatumikia wananchi.

1.4         Uchaguzi wa Jimbo la Kiembesamaki:
Mheshimiwa Spika, tarehe 2 Februari, 2014 wananchi wa Jimbo la Kiembesamaki walifanya uchaguzi na kupata Mwakilishi wao ambae anatokana na ridhaa ya wananchi wa Jimbo hilo. Katika uchaguzi huo Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo aliyegombea kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi aliibuka na ushindi mnono na kuwa Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki.

Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza kwa dhati Mhe. Mahmoud Thabit Kombo, kwa ushindi mnono alioupata kwa kuchaguliwa na wananchi wa Jimbo la Kiembesamaki kuwa Mwakilishi wao.  Wananchi wa Jimbo hilo wamefanya uamuzi wa busara wa kumchagua Mhe. Mahmoud Thabit Kombo. Hongera sana Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo.  Wewe siyo mgeni wa Baraza hili ingawa ni mgeni wa ukumbi huu, umekuwemo katika Baraza la Wawakilishi miaka kadha iliyopita na tunaikumbuka michango yako uliokuwa unaitoa ukiwa Mwakilishi wa Jimbo la Mpendae na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo.  Ni matumaini yetu kwamba Baraza hili litafaidika tena na michango yako katika kipindi hiki.

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii pia kuwapongeza wagombea wote pamoja na vyama vyao kwa kushiriki vyema katika uchaguzi huo ambao ulikuwa huru na wa haki na ulifanyika kwa salama, amani na utulivu mkubwa. Uchaguzi huo umekwisha na sasa ni wakati wa kushirikiana kwa pamoja katika kuendelea kuiletea maendeleo nchi yetu. Aidha, niwapongeze wananchi wa Jimbo la Kiembesamaki kwa kushiriki kwa wingi na kwa amani katika uchaguzi huu.

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kumpa pole   nyingi Mhe. Haroun Ali Suleiman, Waziri wa Nchi (OR), Kazi na Utumishi wa Umma ambaye kwa sasa yuko matibabuni Afrika Kusini na kumuombea Mungu ampe nafuu haraka ili aje kuungana nasi katika ujenzi wa nchi yetu.  Narudia tena kuwahakikishia wananchi na Baraza lako tukufu kwamba Mhe. Maalim Haroun yuko salama na hali ya afya yake inazidi kuimarika.  Ni jana tu nilizungumza na mwanawe Ali ambaye amenihakikishia kuwa hali ya Maalim Haroun alikuwa anaendelea vizuri na kwa mujibu wa maelezo ya Daktari wake huenda akaruhusiwa kurudi mnamo mwanzoni mwa mwezi ujao.

1.5         Mheshimiwa Spika, napenda pia kuwashukuru sana Waheshimiwa Wajumbe wote wa Baraza lako Tukufu kwa kujadili kwa kina miswada na ripoti mbali mbali ambazo ziliwasilishwa kwenye Mkutano huu wa Kumi na Tano. Ushauri uliotolewa na Waheshimiwa Wajumbe kupitia mijadala hiyo utasaidia sana katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali. Vile vile, niwashukuru sana Waheshimiwa Mawaziri kwa kujibu vizuri maswali yaliyoulizwa na Waheshimiwa Wajumbe na pia kutoa ufafanuzi wa kina kwa hoja mbali mbali zilizoibuka kwenye Mkutano huu.

2.0         Mambo yaliyojitokeza nchini:
2.1         Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar:
 Mheshimiwa Spika, tarehe 12 Januari, 2014 ilikuwa ni siku ya kilele cha  Maadhimisho ya Sherehe za Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar kutimiza miaka 50, maadhimisho ambayo yalizinduliwa rasmi tarehe 15 Agosti, 2013 na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi chote cha maadhimisho ya sherehe hizo tulishuhudia kufanyika mambo mbali mbali, ikiwemo uwekaji wa mawe ya msingi na ufunguzi wa miradi mbali mbali ya maendeleo, kulikuwa na matamasha mbali mbali ya michezo na muziki, maonesho na fensi, warsha na makongamano yaliyowashirikisha wananchi wengi. Jumla ya miradi 73 ilifunguliwa na miradi 41 iliwekewa mawe ya msingi.

Aidha, siku ya kilele tulishuhudia gwaride na maonesho ya kijeshi ya aina yake yaliyoandaliwa na Vikosi vyetu vya ulinzi na usalama, maandamano ya wananchi wa mikoa yote mitano ya Zanzibar na halaiki ya vijana wetu iliyopendeza sana.

Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua fursa hii kuwashukuru sana Wajumbe wa Baraza lako Tukufu na wananchi wote kwa jumla kwa kushiriki kikamilifu katika matukio mbali mbali wakati wa shamra shamra za miaka 50 ya Mapinduzi yetu. Pia, nachukua nafasi hii kuwapongeza sana Waheshimiwa Viongozi wote waliokuwa wageni rasmi katika matukio mbali mbali.

Aidha, naishukuru sana Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa na Kamati zake zote kwa kazi kubwa waliyoifanya hadi kufanikisha sherehe zetu ambazo zilikuwa za aina ya kipekee. Niwashukuru pia Vikosi vyetu vya Ulinzi na Usalama, wanafunzi wa halaiki, wasanii, wanahabari na wananchi wote ambao walishiriki kwa njia moja au nyengine katika kufanikisha maadhimisho haya.

2.2         Hali ya Amani, Utulivu na Usalama nchini:
Mheshimiwa Spika, amani, utulivu na usalama katika nchi ni nyenzo muhimu kwa maendeleo ya nchi yoyote duniani. Tanzania ni nchi inayoendelea kuheshimika katika Bara la Afrika na duniani kwa jumla kwa jinsi tunavyodumisha amani, utulivu na umoja katika nchi yetu. Hivyo, ni vyema kila mmoja wetu kuilinda na kuidumisha hali hii, ingawa katika siku za hivi karibuni kumejitokeza vikundi vya watu wachache wanaowasumbua wananchi kwa kuwavamia katika nyumba zao, kupora mali na kuwahatarishia maisha yao. Serikali haitavumilia kuona vitendo hivi vya uvunjifu wa amani vikifanyika katika nchi hii. Naliagiza Jeshi la Polisi kufanya kila linalowezekana kuwasaka na kuwakamata wote wanaohusika na vitendo hivyo na kuwafikisha katika vyombo vya sheria. Aidha, tunawaomba wananchi kuimarisha hali ya ulinzi katika maeneo yao na kutoa taarifa kwa vyombo husika mara moja wakigundua kuwepo dalili za uvunjifu wa amani na usalama katika maeneo yao.   Tunataka wananchi wetu wafanye shughuli zao za kuendesha maisha yao na ya familia yao kwa njia ya amani na utulivu bila ya kuwa na hofu yoyote.

2.3         Ununuzi na Uuzaji wa zao la karafuu:
Mheshimiwa Spika, karafuu ni zao muhimu katika uchumi wa nchi yetu na huchangia kwa kiasi kikubwa katika pato la Taifa na kuinua maisha ya wananchi wetu. Katika msimu wa karafuu wa mwaka 2013/2014, Serikali hadi kufikia tarehe 27 Januari, 2014 imeshanunua jumla ya tani 4995.4 za karafuu zenye thamani ya T.Shs. 69.89 bilioni. Kiasi hicho ni sawa na asilimia 119 ya lengo la kununua tani 4,200 kwa msimu wa mwaka huu. Aidha, Serikali tayari imeshauza karafuu nje ya nchi jumla ya tani 4,272 kwa thamani ya T.Shs. 73.03 bilioni.

Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa zao la karafuu nchini mwetu, Serikali imefanya jitihada za kuwainua wazalishaji wa zao hili kwa kutoa bei nzuri ya ununuzi wa karafuu zetu. Aidha, Serikali imewashajiisha wakulima wa karafuu kwa kuwapatia miche ya mikarafuu bure ili waweze kuotesha mikarafuu mengine mipya katika mashamba yao itakayozaa vizuri, tofauti na ile ya zamani ambayo kwa sasa mingi yao imechoka na kiwango cha uzalishaji ni mdogo.

Mheshimiwa Spika, huku Serikali ikifanya jitihada hizo kwa lengo la kuzalisha karafuu zaidi, kumeibuka watu wachache miongoni mwetu ambao hupita kwenye maeneo mbali mbali, kuwarubuni wakulima na kununua karafuu zao na baadae kuzisafirisha kwa njia za magendo na kwenda kuziuza nje ya nchi yetu. Watu hawa pia huwaibia wananchi kwa kutumia vipimo visivyo sahihi kwa ajili ya kujipatia manufaa zaidi.  Watu wa aina hii ni wahalifu na wahujumu wa uchumi wetu.  Natoa wito kwa wananchi kuwa macho na watu hawa na wasiwauzie karafuu zao wababaishaji wanaopita majumbani mwao na yeyote ambae atafanya hivyo pelekeni taarifa mara moja kwa viongozi wenu wa Shehia au Jeshi la Polisi ili waweze kuchukuliwa hatua zinazofaa. Serikali imeweka Taasisi maalum ya kununua na kuuza karafuu zetu ambayo ni ZSTC pekee, chombo ambacho kimeendelea kutekeleza majukumu yake kwa umakini na kutoa huduma bora za soko kwa wakulima wa zao la karafuu. Aidha, nakipongeza sana Kikosi chetu cha KMKM kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya ya kuwakamata wanaofanya biashara ya magendo. Nawapongeza raia wema wote wanaotoa taarifa kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama wanapobaini kuwepo kwa vitendo hivyo viovu, vyenye nia ya kuinyima Serikali mapato yake.

2.4         Mwenendo wa Bei za Bidhaa:
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2013 kumekuwa na utulivu wa bei za bidhaa kama vile mchele, sukari na unga wa ngano jambo ambalo linaleta faraja sana kwa wananchi wetu. Serikali inawapongeza sana wafanyabiashara wetu na inawataka waendelee kushirikiana na Serikali kwa kujadiliana na kushauriana masuala mbali mbali ya bei za bidhaa hasa mchele, sukari na unga wa ngano kwa lengo la kuwapunguzia wananchi wetu ukali wa maisha. Serikali inawaomba wafanyabiashara kuendelea kuagiza bidhaa hizo kwa wingi na kuuza kwa bei ambazo wananchi wanaweza kununua.

2.5         Usambazaji wa Huduma za Mkonga wa Mawasiliano:
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Kampuni ya Zantel inaendelea na kazi ya kusimamia usambazaji wa Mkonga katika taasisi za Serikali Unguja na Pemba. Hadi sasa zaidi ya taasisi 80 za Serikali tayari zimeshasogezewa Mkonga wa Mawasiliano na kufungwa kifaa maalum cha kusambazia huduma hiyo (Optical Distribution Frame). Serikali inaziomba taasisi zake zote kukamilisha uwekaji wa mtandao wa ndani (LAN) kwenye majengo yao ili waweze kufaidika na huduma za mtandao kupitia Mkonga huo.

2.6         Tatizo la Dawa za Kulevya:
Mheshimiwa Spika, suala la uingizaji, usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya bado linaendelea kuwa tatizo katika nchi yetu. Tatizo hili linatishia afya na maisha ya watu wetu, na hasa vijana na hivyo kuhatarisha uimara wa uchumi na maendeleo ya Taifa letu. Tukio la hivi karibuni la kukamatwa mabegi mawili yenye ujazo wa jumla ya kilo 30 za dawa za kulevya katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume ni la kusikitisha sana na kuifedhehesha nchi yetu. Serikali itawasaka kwa nguvu zote wale wote waliohusika na dawa zilizokamatwa na kufikishwa katika vyombo vya Sheria na mtandao wao wa udhalimu huu kudhibitiwa. 

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na juhudi zake za kupambana na wale wote wanaojihusisha na biashara hii haramu bila ya kujali nyadhifa zao, umaarufu wao na hali zao za maisha. Aidha, Serikali itaendelea kuelimisha jamii juu ya madhara ya utumiaji wa dawa hizi hatari kwa maisha ya binaadamu. Naomba kuwasihi wale wote wanaohusika na udhibiti wa uingiaji na usambazaji wa dawa za kulevya kuwa makini na utendaji wao wa kazi kwani kuanzia sasa Serikali itachukua hatua kali kwa watakaobainika kushiriki kwa namna yeyote katika biashara hii haramu.  Hata hivyo, vita hivyo siyo vya Serikali peke yake, bali ni vyetu sisi sote wananchi.  Wananchi wakitimiza wajibu wao wa kuwafichua wanaohusika na biashara hii, vita hivi vitakuwa rahisi kushinda.

2.7         Vyombo vya usafiri wa baharini:
Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 5 Januari, 2014 kulitokea ajali katika maeneo ya Nungwi wakati meli ya MV Kilimanjaro II ilipokuwa ikitoka Pemba kuelekea Unguja. Ajali hiyo ilisababishwa na upepo mkali na Nahodha alishindwa kuihimili na baadhi ya abiria waliokuwa wamekaa juu na pembezoni mwa meli hiyo walianguka na kutumbukia baharini. Serikali imeunda Tume ya Uchunguzi ili kujua chanzo na sababu za kutokea ajali hiyo na taarifa ya uchunguzi huo itatolewa kwa wananchi mara tu Tume hiyo itakapokamilisha na kuwasilisha ripoti yake.

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kuwapa mkono wa pole ndugu na jamaa wote ambao walipoteza ndugu zao kwenye ajali hiyo. Mungu awape moyo wa subira, na uvumilivi, Amin. Pia nawapa pole wale wote ambao kwa njia moja ama nyengine waliathirika na ajali hiyo. Mungu aendelee kuwapa afya njema.

Mheshimiwa Spika, Kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa yanayoendelea kuikumba dunia na katika sehemu za nchi yetu, ni muhimu kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri baharini, manahodha na wananchi kwa jumla kufuatilia maelekezo yanayotolewa na taasisi husika kuhusu mwenendo wa hali ya hewa na kuchukua hadhari wakati wanaposafiri kwa kutumia vyombo vya baharini.
Aidha, napenda kutoa pole nyingi na za dhati kwa wananchi wa Micheweni kwa maafa waliyoyapata ya kuunguliwa na nyumba zao.  Mimi mwenyewe nilikitembelea kijiji kilichoathirika na maafa hayo na kuiona hasara kubwa iliyopatikana.  Ninawaomba wananchi wa Micheweni wawasaidie wenzao walioathirika ili waweze kurejea katika hali zao za kawaida.  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwasaidia wananchi hao kadri itakavyoweza.

2.8         Bunge la Katiba:
Mheshimiwa Spika, sote tunaelewa kwamba nchi yetu imo kwenye hatua za kupata Katiba Mpya na tayari Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Mwenyekiti wake Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba imeshakabidhi Rasimu ya Pili ya Katiba hiyo kwa Serikali zote mbili. Hatua iliopo mbele yetu sasa ni kuwa na Bunge la Katiba litakalojadili na kupitisha Rasimu ya Katiba Mpya na baadae kupigiwa kura ya maoni na wananchi. Watendaji wetu wa Baraza la Wawakilishi kwa kushirikiana na watendaji wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaendelea kuandaa Kanuni pamoja na taratibu nyengine zitakazoongoza Bunge hilo linalotarajiwa kuanza hivi karibuni baada ya majina 201 ya Wajumbe watakaoingia katika Bunge hilo kutangazwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete   mnamo siku chache zijazo. Taratibu zote zitakapokamilika Waheshimiwa Wawakilishi pamoja na Wajumbe wengine wa Bunge hilo watajulishwa rasmi.

Tunawaomba Waheshimiwa wote watakaobahatika kushiriki katika Bunge hilo kutilia maanani maslahi ya nchi yetu, umoja na mshikamano wetu na uhai wa Taifa letu.  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haina mwongozo wa kutoa kwa washiriki wa Zanzibar ili kumfanya kila mshiriki awe huru kuichambua na kuijadili rasimu hiyo kadri atakavyoona inafaa.  Mwisho wa yote tungependa kuona nchi inapata Katiba mpya itakayokuwa nzuri na yenye maslahi kwa wote.

3.0         Migogoro ya ardhi: 
Mheshimiwa Spika, tangu Awamu ya Saba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuingia madarakani suala la kutatua migogoro ya ardhi limepewa kipaumbele kwa kufanya juhudi mbali mbali.

Kama hatua ya msingi tumeanza na mapitio ya Sera ya Ardhi kwa vile Sera ndio dira kuu ya kusimamia na kuendeleza matumizi bora na endelevu ya ardhi. Sera hiyo itakapokamilika ndio itakayotoa miongozo ya muda mfupi na ya muda mrefu juu ya mustakbali mzima wa ardhi, na kuondoa mianya ya uwezekano wa kutokea migogoro ya ardhi hapa Zanzibar.

Mheshimiwa Spika,
Katika kuendeleza jitihada za kupatia ufumbuzi wa kudumu migogoro yote ya ardhi, Serikali imechukua jitihada zifuatazo:-

a)    Mahakama za Ardhi zimeimarishwa kwa kuengezwa idadi ya Mahakama katika Mikoa yote ya Unguja na Pemba sambamba na uteuzi wa Mahakimu katika Mahakama hizo.  Aidha, idadi ya wazee wa Baraza imeongezwa ili kuharakisha maamuzi ya utatuzi wa migogoro ya ardhi.  Uimarishaji huo wa Mahakama umeleta matokeo mazuri.  Kwa mfano, katika kipindi cha miezi sita (6) iliyopita jumla ya kesi 187 zimeweza kutolewa maamuzi.

b)   Kufanywa Marekebisho ya Sheria ya Umiliki wa Ardhi Namba 12 ya 1992.

Mnamo mwaka 2013, Baraza la Wawakilishi lilipitisha marekebisho madogo madogo (Miscellaneous Ammendments) ya sheria ambayo yatarahisisha ulipaji wa fidia pindipo Serikali inapolichukua eneo la mwananchi kwa manufaa ya Taifa.

c)     Usajili wa Ardhi:
Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati inaendelea na kazi ya kumtambua na kumthibitisha kila mwenye haki ya matumizi ya ardhi katika maeneo mbali mbali Unguja na Pemba kwa lengo la kuondoa migogoro ya ardhi.  Utambuzi ni hatua ya awali katika kufikia lengo kuu la MKUZA II la kusajili asilimia hamsini ya ardhi yote ya Zanzibar ifikapo mwaka 2015.

d)    Uhaulishaji wa Ardhi:
Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati imepata mafanikio makubwa ya utendaji wa kazi za uhaulishaji wa ardhi kwa kuondoa athari za kutapeliwa na kudhulumiwa kutokana na umakini katika utendaji kazi wa Bodi ya Uhaulishaji.

e)    Kuchukua hatua za nidhamu:
Serikali imechukua hatua mbali mbali za kinidhamu kwa watendaji wote wanaobainika kwa namna moja au nyengine ni chanzo cha migogoro ya ardhi na uvunjaji wa sheria za ardhi.

Utaratibu wa upimaji na ugawaji wa ardhi:
Mheshimiwa Spika,
Serikali kupitia Wizara husika imeanzisha mfumo wa kuwashirikisha Viongozi wa Mikoa, Wilaya, Masheha na Madiwani katika taratibu zote za upangaji na upimaji wa ardhi.  Aidha, mpango mkuuu wa matumizi ya ardhi Zanzibar (National Land Use Plan) kwa mara ya kwanza umeshirikisha wadau wote waliotajwa hapo juu ili kila mdau aweze kujiona kama ni mshiriki kamili wa maendeleo ya eneo lake na mlinzi dhidi ya ujenzi holela.

Pia, ningependa kutoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu kwenye zoezi la usajili wa ardhi ambalo kwa sasa linagharamiwa na mradi wa Smole na mpango wa MKURABITA.  Hivyo, ni vyema wananchi waitumie kikamilifu fursa hii adimu na adhimu.

4.0         Mambo yaliyojitokeza Barazani:
Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu wa Kumi na Tano jumla ya maswali 40 ya msingi na maswali 92 ya nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu na kupatiwa majibu na ufafanuzi na Waheshimiwa Mawaziri. Pia, Waheshimiwa Wajumbe walijadili na kupitisha Miswada miwili: Mswada wa Sheria ya Kuanzisha Sheria ya Hakimiliki za Wagunduzi wa Aina Mpya za Mbegu za Mimea na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo na Mswada wa Sheria ya Kufuta Sheria ya Karafuu Nam. 11 ya mwaka 1985 na Kuweka Sheria Mpya ya Maendeleo ya Karafuu na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo.


4.2       Maelezo ya Miswada iliyowasilishwa:
Mheshimiwa Spika, Mswada wa Kwanza ambao uliwasilishwa na Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako kupata nafasi ya kuujadili ni Mswada wa Sheria ya Kuanzisha Sheria ya Hakimiliki za Wagunduzi wa Aina Mpya za Mbegu za Mimea na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo. Madhumuni ya Mswada huu ni pamoja na kuweka mfumo utakaowatambua na kuwalinda wagunduzi wa aina mpya ya mbegu za mimea waliopo na watakaokuja nchini na kulinda hakimiliki zao. Pia Mswada huu una lengo la kuongeza na kuvutia uwekezaji kwenye sekta ya kilimo kwa kuongeza hamasa katika ugunduzi wa mbegu mpya zinazokidhi mahitaji ya wakulima na masoko pamoja na upatikanaji wa taarifa muhimu ikiwa ni pamoja na matokeo ya majaribio ya kitaalamu na upatikanaji wa teknolojia mpya za utafiti na ugunduzi wa mbegu mpya.

Aidha, kupatikana kwa Sheria hii hapa Zanzibar kutaiwezesha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutimiza masharti ya kujiunga na Shirika la Kimataifa la Hakimiliki za Wagunduzi wa Aina Mpya za Mbegu za Mimea (International Union for the Protection of New Varietees of Plants – UPOV). Kwa kujiunga na Shirika hilo, Tanzania itapata faida nyingi zinazohusiana na masuala ya maendeleo ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, Mswada wa Sheria ya Kufuta Sheria ya Karafuu Nam. 11 ya mwaka 1985 na Kuweka Sheria Mpya ya Maendeleo ya Karafuu na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo nao uliwasilishwa ndani ya Baraza lako Tukufu na kujadiliwa na Waheshimiwa Wajumbe. Mswada huu umeanzishwa kutokana na mapungufu mengi yaliyokuwemo kwenye Sheria ya Karafuu ya mwaka 1985. Sheria hii mpya pamoja na mambo mengine pia itahusisha masuala yote yanayohusu karafuu kama vile ukulima wa zao la karafuu, uvunaji, uanikaji, uhifadhi wa mikarafuu na maeneo ya maendeleo ya mikarafuu.

Mheshimiwa Spika, aidha, Sheria hii itaanzisha Mfuko Maalum wa Maendeleo ya Karafuu kwa lengo la kuliendeleza zao la karafuu na kuwaendeleza wakulima wa zao hilo kifedha. Vile vile, Mfuko una lengo la kusaidia uendeshaji wa tafiti kwa ajili ya maendeleo ya karafuu na kusaidia huduma za matibabu kwa wakulima na watu watakaopata madhara wakati wa shughuli za uchumaji wa karafuu. Kwa ujumla Mswada huu ni mzuri kwani utasaidia sana masuala mbali mbali ya maendeleo ya zao letu la karafuu kuhusu ukulima bora, utunzaji na uuzaji wake.

Mheshimiwa Spika, nawashukuru Waheshimiwa Wajumbe kwa kuzikubali na kuzipitisha Sheria hizi muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu. Naziagiza taasisi husika mara baada ya kukamilika kwa taratibu za kuanzisha Sheria hizi, kuchukua hatua za makusudi za kuielimisha jamii kuhusiana na matakwa ya Sheria hizi ili kurahisisha utekelezaji wake.  

    4.3       Ripoti za Kamati za Kudumu za Baraza la Wawakilishi:
Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu, Waheshimiwa Mawaziri waliwasilisha taarifa za utekelezaji wa maagizo ya Kamati za Kudumu za Baraza la Wawakilishi kwa mwaka 2012/2013. Aidha, Waheshimiwa Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Baraza lako Tukufu waliwasilisha taarifa za Kamati zao kwa mwaka 2013/2014. Kutokana na taarifa hizo, Waheshimiwa Wajumbe walipata nafasi ya kujadili, kuibua hoja mbali mbali za msingi pamoja na kutoa ushauri utakaosaidia kuimarisha utendaji kazi wa Serikali. Serikali itaendelea kushirikiana na Waheshimiwa Wawakilishi pamoja na kuzifanyia kazi hoja za msingi zinazoibuliwa na Wajumbe. Dhamira ya Serikali ni kuwa na uwajibikaji utakaoleta ufanisi, tija na maslahi kwa Taifa letu.  Napenda kuliahidi Baraza lako Tukufu kwamba maagizo na maelekezo yote yaliyotolewa katika Ripoti za Kamati kwa mwaka 2013/14 yatafanyiwa kazi na Serikali kwa ukamilifu.

Nawapongeza sana, Mhe. Spika, Wajumbe wa Baraza hili namna walivyokuwa makini katika kutekeleza wajibu wao wa kuisimamia Serikali na kuibua ubadhirifu wa mali na fedha za umma unaofanywa Serikalini.  Serikali itafanya kila juhudi kuirekebisha hali hiyo.

Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kuzipongeza Kamati zote za Kudumu za Baraza hili kwa kazi wanazozifanya za kuisaidia Serikali yetu kuimarisha utendaji na uwajibikaji. Naomba tuendelee kushirikiana katika kuiletea maendeleo nchi yetu kwa faida yetu na vizazi vijavyo.

Mheshimiwa spika, napenda kuwahakikishia Wajumbe wa Baraza lako tukufu kuwa Serikali haidharau na wala haitodharau maagizo yanayotolewa na Kamati za Kudumu ila maagizo yote hufanyiwa kazi kikamilifu na kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha kuwa ubadhirifu huo haufanyiki na itaendelea kufanya hivyo.  Serikali haitamvumilia yoyote atakaye thibitika kufanya ubadhirifu huo.

5.0         Uwasilishaji wa Bajeti ya Serikali na bajeti za Mawizara kwa mwaka wa fedha 2014/2015:
Mheshimiwa Spika, kabla sijamaliza hotuba yangu napenda kuliarifu Baraza lako Tukufu kwamba Serikali inakusudia kubadilisha mfumo wa kuwasilisha Barazani mapendekezo ya bajeti kuwa katikati au mwishoni mwa mwezi wa Mei badala ya mwezi wa Juni. Kwa mwaka ujao wa fedha (2014/2015) bajeti itawasilishwa katika mwezi wa Mei na kumalizika mwishoni mwa mwezi wa Juni kabla ya kuanza Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan. Hivyo, ni vyema kwa Mawizara kuanza maandalizi ya mapema ya hotuba zao za bajeti na pia Kamati za Baraza na Wajumbe wa Baraza kujipanga kuendana na mabadiliko hayo.  

6.0         Hitimisho:
Mheshimiwa Spika, kwa mara nyengine tena nichukue nafasi hii kukupongeza tena wewe binafsi, wasaidizi wako pamoja na watendaji wote wa Baraza kwa kutekeleza majukumu yenu kwa uadilifu na ufanisi mkubwa.

Mheshimiwa Spika, pia niwashukuru sana Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako kwa ushauri wao wenye lengo la kuimarisha utekelezaji wa Majukumu ya Serikali. Ni imani yangu kwamba, Waheshimiwa Wawakilishi wanapoibua hoja mbali mbali ndani ya Baraza hili wana lengo la kuisaidia Serikali yetu ili iwe makini zaidi katika utendaji kazi wake. 

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa niwashukuru waandishi wa habari, wakalimani wa alama kwa kazi zao nzuri za kuipasha habari jamii. Nawashukuru wananchi wote kwa kufuatilia mijadala ya Baraza kupitia vyombo vyetu vya habari na kuendelea kuiamini serikali yao na kudumisha amani, utulivu na mshikamano katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, nawatakia Waheshimiwa Wawakilishi wote kurudi vituoni mwao salama kwenda kuwahudumia wananchi Majimboni mwao.

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa naomba kutoa hoja ya kuliakhirisha Baraza lako Tukufu hadi tarehe 14 Mei, 2014, Saa 3 kamili za asubuhi.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>