Na Kauthar Abdalla
BODI ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar, imesema uhaba wa fedha umesababisha wanafunzi wanaosoma vyuo vya ndani kuchelewa kupata mikopo na badala yake kipaumbele kimetolewa kwa wanafunzi walioko nje ya nchi.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake Majestik, Mkurugenzi bodi hiyo, Iddi Khamis Haji, alisema si kweli kwamba bodi ya mikopo imekataa kuwapa fedha wanafunzi wa vyuo vya ndani, isipokuwa kikwazo ni upatikanaji mdogo wa fedha kutoka wizara ya fedha.
Hata hivyo, alisema wapo baadhi ya wanafunzi wanaosoma vyuo vya ndani wameshalipiwa baadhi ya fedha.
Alisema bodi ilibaini kwamba kama ingechelewesha fedha kwa wanafunzi walioko ugenini, wangepata shida na kushindwa kumudu mahitaji yao, ikiwemo gharama za malazi.
Alisema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2013/2014, bodi ilitengewa shilingi bilioni 9.1 lakini hadi kufikia Januari 2014, fedha zilizoingizwa zilikuwa shilingi bilioni 2.1 pekee.
Hata hivyo, alisema bodi itawalipia wanafunzi hao mara fedha zitakapopatikana na kwamba hatarajii chuo chochote kuwafukuza wanafunzi.
Aidha aliwataka wanafunzi na wazazi kuwa wastahamilivu katika kipindi hichi ambacho bodi inasubiri fedha kutoka hazina.
Akizungumzia deni la bodi kwa wahitimu, alisema ni wahitimu 300 pekee kati ya 2800 ndio walioanza kulipa mikopo yao.