Na Amina Omari,TANGA
UTAFITI wa awali wa mpango mkakati wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) wa 2012 hadi 2015, umeonesha kiwango cha uandishi unaozingatia maadili na uweledi katika vyombo vya habari hasa magazeti, umeongezeka.
Hayo yameelezwa na Meneja Maadili na Usuluhishi wa MCT, Allan Lawa, wakati wa mkutano na wahariri wa vyombo vya habari uliofanyika jijini Tanga.
Alisema licha ya mafanikio hayo bado kuna shida katika maeneo ya kuripoti habari za mahakamani, jinsia, katiba na kujitokeza kwa habari za uchochezi kwenye vyombo hivyo.
"Kumekuwepo na tatizo katika baadhi ya vyombo kuandika habari za uchochezi ambazo zinaweza kutufikisha kwenye machafuko jambo ambalo kama baraza hatutaki litokee,” alisema.
Pia alisema makosa ya habari za chuki yameongezeka kutoka makosa 11 katika kipindi cha miezi sita ya mwaka 2013,mpaka kufikia 53 kipindi cha Julai hadi Disemba.
Alisema utafiti huo utakapokamilika utawezesha MCT kuja na mpango madhubuti wa kuimarisha weledi ndani ya vyumba vya habari,waandishi wenyewe pamoja na vyuo vya tasnia hiyo.
Hata hivyo, aliwashauri wahariri wa vyombo vya habari kuhakikisha wanazisoma ripoti zinazotolewa na baraza ili kuongeza kiwango cha uweledi,kujirekebisha pale penye upungufu na kutoa taarifa sahihi.
Nae Meneja Machapisho, John Mireny, alisema lengo la mkutano huo ni kuwashirikisha wahariri katika kubaini upungufu ya kiutendaji uliopo katika utendaji wao na kutafuta mbinu ya kusuluhisha changamoto hizo.
Aliongeza kuwa michango hiyo ya kiutendaji itawezesha baraza kufanya tathimini ya kupata mwelekeo wa maeneo ambayo yamebainika kuna upungufu hayajafikiwa malengo hivyo kuyatafutua ufumbuzi.
Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga, alisema nia ya baraza ni kuhakikisha uhuru wa vyombo vya habari unapatikana pamoja na kuongeza uwajibikaji kwa jamiii kwa vyombo hivyo.