Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Wafuasi wa CCM, CHADEMA wapigana mapanga

$
0
0
Na Kadama Malunde,KAHAMA
ZIKIWA zimesalia  siku chache kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa kiti cha udiwani katika kata Ubagwe wilayani Kahama mkoani Shinyanga,kampeni za uchaguzi huo zimeingia doasari baada ya watu wanaodhaniwa kuwa ni wafuasi CHADEMA kuwavamia na kuwajeruhi vibaya kwa mapanga   wafuasi watano wa CCM.
Akizungumza katika hospitali ya wilaya ya Kahama alikolazwa kufuatia kupata majeraha ya mapanga, Katibu mwenezi wa CCM wilaya ya Kahama, Masood Melimeli, alisema tukio hilolilitokea juzi majira ya saa 1:30 usiku wakati wakitokea kijiji cha Ihata kwenda Itobola kwenye kampeni.
Alisema walipofika katikati ya pori walikutana na gari la CHADEMA aina ya Toyota land Cruser ikiongozwa na Mbunge wa jimbo la Maswa Mashariki, Sylivester Kasulumbayi na kuanza kuwashambulia kwa kutumia mapanga, nondo na marungu.
Alisema waliojeruhiwa katika vurugu hizo ni Katibu mwenezi wa CCM, Masood Melimeli aliyeumia sehemu ya mkono na bega, Ramadhani Salumu aliyepigwa panga la mguu na mkono, Sebastian Masonga aliyevunjwa mkono wa kushoto, dereva Charles Muhiga aliyejeruhiwa sehemu za kichwani na Mtendaji wa kata ya Ubagwe, Stephen Kimario, aliyepigwa vibaya sehemu za kichwani.

Alisema katika tukio hilowafuasi wawili wa CCM waliofahamika kwa jina moja moja la Ismail na Samweli walipotea kusikojulikana baada ya kukimbia kujinusuru na kifo.
Katibu mwenezi wa CCM mkoa wa Shinyanga, Emanuel Mlimandago, amelaani kitendo hicho na kusema hiyo  sio demokrasia ya kweli na kuongeza kuwa Watanzania wote hawana budi kulaani kitendo hicho.
Mwenyekiti wa TADEA wilaya ya Kahama, Charles Lubala, akizungumzia tukio hilo, alisema mfuasi mmoja wa CHADEMA alivamia mkutano wa CCM na ndipo walipomkamata na kumuweka katika gari lao kwa lengo la kumpeleka kituo cha polisi Bulungwa.
Alisema  baada ya kumuweka garini,wafuasi wa CHADEMA walitangulia mbele na kuweka vizuizi barabarani  kabla ya kuanza kushambuliana.
“Kwa kweli hizi kampeni zimekuwa kama  vita kwa sasa ni hatari na tunapaswa kujihami kikamilifu kwani unaweza kupoteza maisha kwa sababu ya kampeni tu,” alisema.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Kahama, Juma Protas, alikanusha wafuasi wa chama hicho kuhusika katika tukio hilo.
“Siyo kweli,vijana watatu wa CHADEMA ndiyo waliotekwa na CCM katika eneo la makao makuu ya kata ya Ubagwe, baada ya kutekwa wakafungwa kamba na kuingizwa kwenye gari, ndipo wananchi wananchi walipoamua kwenda kuwasaidia na purukushani ndipo zilipoanza,” alisema.
“Baada ya purukushani hizo,CCM wakapiga simu polisi, polisi wakaenda kwenye kambi ya CHADEMA na kupiga risasi juu kisha kuwakamata wafuasi 13 wa akiwemo Mbunge wa Maswa Mashariki, Sylivester Kasulumbayi, na sasa wanapelekwa mahakamani,CCM ndiyo waliteka vijana watatu  wa CHADEMA na vijana hawa hadi sasa hawajulikani walipo,” alisema.
Mganga mkuu wa hospitali ya wilaya ya Kahama, Dk. Hellen Membe, alisema siku ya tukio  majira ya saa sita usiku alipokea majeruhi watano na wanaendelea kupatiwa matibabu.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu, Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga, ACP Evarist Mangala, alithibitisha kutokea tukio hilo na kuongeza kuwa jeshi la polisi linawashikilia watu 13.

Kampeni za uchaguzi katika kata ya Ubagwe wilayani Kahama zinafanyika kufuatia aliyekuwa diwani wa kata hiyo, Richard Mndula kufariki dunia mwaka jana huku kinyang’anyiro hicho kikiwahusisha wagombea watatu  kutoka vyama vya CCM, TADEA na CHADEMA.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>