Balozi Mteule wa Tanzania Nchini Malaysia Dr. Aziz Honari Mlima akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati alipofika kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Balozi Mteule wa Tanzania Nchini Malaysia Dr. Azizi Honari Mlima ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar. Balozi Aziz piakatika wadhifa huo ataiwakilisha Tanzania Katika Nchi za Thailand, Philippines, Cambodia, Brunei, Laos na Vietnam.
Waziri wa Sheria na Katiba wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Asha – Rose Migiro akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo yake na Waziri wa Sheria na Katiba wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Asha – Rose Migiro alipofika Ofisini kwake kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete kushika wadhifa huo.(Picha na Hassan Issa wa – OMPR)
Na Othman Ame OMPR.
Balozi Mteule wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Malaysia Dr. Aziz Honari Mlima ameagizwa kutumia nafasi yake ya Kidiplomasia kuyashawishi Mataifa ya Kati na Mashariki ya Bara la Asia ili Makampuni na Taasisi zake za Kiuchumi na Biashara zielekeze nguvu zao za uwekezaji hapa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Agizo hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar wakati wa mazungumzo yake na Balozi Mteule wa Tanzania Nchini Malaysia Dr. Aziz Honari Mlima aliyefika kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete kushika wadhifa huo.
Balozi Seif alimueleza Dr. Aziz Honar Mlima atakaye kuwa na Ofisi yake Nchini Malaysia akihudumia pia Nchi za Thailand, Philippines, Cambodia, Brunei, Laos na Vietnam kwamba Mataifa hayo tayari yameshapiga hatua kubwa kiuchumi kiasi kwamba Zanzibar inaweza kujifunza kutoka kwa Mataifa hayo.
Alifahamisha kwamba Zanzibar hivi sasa imeelekeza mtazamo wa nguvu zake katika uimarishaji wa miundo mbinu ya Viwanda vidogo vidogo na kuyakaribisha Makampuni na Taasisi za uwekezaji ndani na nje ya Nchi kuwekeza miradi yao hapa Nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimuomba Balozi Mteule wa Tanzania Nchini Malaysia Dr. Aziz Honari Mlima kuzungumza na Uongozi wa Taasisi na Makampuni ya Nchi hizo ili watumie fursa hizo kuwekeza Vitega uchumi vyao hapa Zanzibar hasa katika Biashara ya Mitandao ya Kisasa itakayotoa nafasi nyingi za Ajira.
“ Tumeweka milango wazi kwa wawekezaji wa kigeni kuja kuwekeza vitega uchumi vyao hapa Zanzibar na itakuwa vyema iwapo Viongozi wa Taasisi na Makampuni yenye shauku ya kuja Nchini wangeandaa ratiba maalum ya kutembelea Zanzibar ili kuona maeneo hayo ya uwekezaji “. Alisema Balozi Seif.
Akizungumzia suala la uimarishaji wa sekta ya Kilimo Balozi Seif aliziomba Nchi za Thailand na Malaysia kupitia Balozi huyo Mteule wa Tanzania kusaidia Taaluma katika sekta hiyo hasa kwenye Kilimo cha umwagiliaji.
Alisema Visiwa vya Zanzibar vimebarikiwa na kuwa na maji mengi kiasi kwamba yanashindwa kutumiwa vyema katika sekta ya kilimo kutokana na ufinyu wa Taaluma miongoni mwa Wakulima na wananchi.
Mapema Balozi Mteule wa Tanzania Nchini Malaysia Dr. Aziz Honar Mlima alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba atatumia hekima na nguvu zake zote katika kuona anaiwakilisha Vyema Tanzania kwenye Mataifa hayo ya Bara la Asia.
Dr. Aziz Honar alimuomba Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kuendelea kumsaidia kutokana na uzoefu wake wa Kidiplomasia pale atapohitaji nguvu za msaada.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikutana kwa mazungumzo na Waziri wa Sheria na Katiba wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Asha – Rose Migiro Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Mh. Asha – Rose Migiro amekuja Zanzibar kujitambulisha rasmi mara baada ya Kuteuliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete kushifa wadhifa huo.
Katika mazungumzo yao Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Viongozi na Watendaji wake itaendelea kumpa ushirkiano wa karibu ili kuona majukumu yake mazito ya Taifa anayatekeleza kwa ufanisi na makini zaidi.
Balozi Seif alisema ushirikiano huo hivi sasa ni muhimu hasa ikizingatiwa kwamba Taifa la Tanzania sasa linapita katika kipindi muhimu na kizito cha kuendelea na mchakato wa kupata katiba mpya ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba Bunge la Katiba haliko mbali kuanza mjadala wake Mjini Dodoma kwa vile mchakato wa kupata wajumbe wa Bunge hilo kupitia Taasisi, jumuia na kundi maalum unakaribia kukamilika kufuatia vikao vya pamoja kati ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa mujibu wa mfumo wa uteuzi wa nafasi hizo ulioainishwa ndani ya rasimu ya katiba hiyo.
Wajumbe hao 201 kutoka Taasisi, Jumuiya na Kundi maalum wanatarajiwa kuungana na wenzao Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Wabunge wa Bunge la Muungano kuunda Bunge lisilopunguwa Wajumbe 600 watakaojadili Rasimu ya Katiba Mpya na hatimae kurejeshwa kwa Wananchi ili kuipigia kura.