STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 09 Februari, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein amewaambia wafanyabiashara wa viungo mjini Mumbai, kuwa Zanzibar haina pingamizi kuwauzia karafuu zake moja kwa moja na akawataka wafanye mazungumzo na Shirika la Biashara la Zanzibar-BIZANJE kuhusu jambo hilo.
Rais alikutana na wafanyabiashara hao baada ya kutembelea kiwanda kikubwa cha kutengeneza viungo cha Everest, kilichoko nje kidogo ya jiji la Mumbai.
Aliwaeleza wafanyabiashara hao kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hivi sasa inatekeleza mkakati wa kufufua zao la karafuu ambalo lilidumaa miaka iliyopita.
Alisema mkakati huo ambao unajumuisha kuongeza kasi ya upandaji wa mikarafuu mipya pamoja na kuwapa wakulima bei nzuri ya soko, uzalishaji umeanza kuongezeka na hata kuweza kutosheleza mahitaji ya wafanyabiashara hao ambayo tani 10,000 kwa mwaka.
Katika manasaba huo Dk. Shein alitoa mwaliko rasmi kwa wafanyabiashara hao kutembelea Zanzibar na kufanya mazungumzo na Shirika la ZSTC.
Awali, baadhi ya wafanyabiashara hao walieleza changamoto zilizowafanya kuacha kununua karafuu moja kwa moja toka Zanzibar kwa hiyo tamko hilo la Mheshimiwa Rais wa Zanzibar walieleza kuwa limewatia moyo na kuahidi kufanya biashara hiyo moja kwa moja na Zanzibar.
Walibainisha kuwa wao wanazihitaji sana karafuu za Zanzibar kutokana na bora wake na kuzisifia kwa kusema kuwa ndiyo “Mfalme wa Karafuu duniani”.
Akizungumzia historia ya biashara kati ya Zanzibar na India Dk. Shein alisema biashara kati ya nchi hizo imedumu kwa miaka karibu miaka 150 na kwamba Zanzibar ipo tayari kutiliana saini Makubaliano ya Ushirikiano na Kampuni ya viungo ya Everest ambayo inatumia karafuu na viungo vyengine kwa wingi.
Wakati huo huo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema ziara yake nchini humu imekuwa ya mafanikio na kufikia malengo yake.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea kiwanda cha kusindika viungo mjini hapa jana Dk. Shein aliwaeleza waandishi hao kuwa ziara yake hiyo imepata mafanikio katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kisiasa kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya India.
Kwa upande mwingine alifafanua kuwa ziara hiyo ya siku tisa iliyomuwezesha kuzuru miiji ya New Delhi, Jaipur, Hyderabad, Bangaluru na Mumbai imeziwezesha Zanzibar na India kuimarisha ushirikiano katika sekta za utalii, uwekezaji, afya, kilimo na uwezeshaji wananchi.
Aliongeza kuwa mbali ya kutia saini makubalinao ya ushirikiano katika baadhi ya sekta lakini pia wahusika wa sekta hizo wamealikwa kutembelea Zanzibar kwa mashauriano zaidi katika kuendeleza ushirikiano katika sekta zao.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwashukuru viongozi wa India hususan Makamu wa Rais wa nchi hiyo Mhe. Mohammad Hamid Ansari na Waziri Mkuu Manmohan Singh kwa kumualika kuzuru India rasmi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amemaliza ziara yake nchini humu na anatarajia kuondoka mjini Mumbai leo Jumapili kurejea nyumbani.
Katika ziara hiyo Dk. Shein amefuatana na Mke wake Mama Mwanamwema, Waziri wa Fedha Omar Yusuf Mzee, Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto Bibi Zainab Omar Mohamed, Waziri wa Biashara na Viwanda na Masoko Nassor Ahmed Marzui, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Dk. Mahadhi Juma Maalim na Balozi wa Tanzania nchini India Injinia John Kijazi.
Wengine katika msafara huo ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya Mohamed Saleh Jidawi na Katibu Mkuu Kilimo na Maliasili Affan Othman Maalim, Mshauri wa Rais Ushirikiano wa Kimataifa, Uwekezaji na Uchumi Balozi Mohamed Ramia na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar –ZIPA Salum Khamis Nassor.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822