Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif akikabidhi msaada wa Bati kwa ajili ya kusaidia uwezekaji wa Jengo la Klabu ya Soka ya Timu ya Kombora iliyopo Kitope.
Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Kirombero Mwalimu Juma Simai akipokea msaada wa vifaa vya kupikia chai vilivyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi kwa skuli zote za jimbo hilo.Hafla hiyo imefanyika katika uwanja wa michezo wa Kombora Kitope.
Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi akizindua na kukagua kisima cha maji safi kiliopo Kijiji cha Mgambo ambacho kimejengwa kutokana na Mfuko wa Jimbo la Kitope.
Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi msaada wa Magodoro, Juzuu na Mashaf Ustadhi wa Madrasat Qiyamu Islamia ya Mgambo Wilaya ya Kaskazini Unguja,akitekeleza ahadi aliyoipa Madrasa hiyo.
Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Mbunge wa Kitope Balozi Seif. Ali Iddi, akizungumza na Wanafunzi wa Madrasat Qiyamu Islamia ya Mgombo Unguja ili kufanya bidii katika kusoma na ili kuja kuwa Walimu Bora wa baadae wa Elimu ya Dini ya Kiislam,(Picha na Hassan Issa – OMPR)
Na Othman Ame OMPR.
Walimu wa Madrasa wameaswa kujiepusha na tabia ya kuwafundisha watoto ushabiki wa Kisiasa kwa kutumia mafundisho ya Dini jambo ambalo linaweza kuleta matabaka na ni hatari kwa watoto hao katika maisha yao ya baadaye.
Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi alitoa nasaha hizo wakati wa hafla fupi ya Kukabidhi msaada wa Magodoro, Misahafu, Juzuu pamoja na fedha taslimu kwa ajili ya ununuzi wa mpira wa kusambazia maji kwa Madrasat Qiyamu Islamia hafla iliyofanyika katika uwanja wa Skuli ya Mgambo Wilaya ya Kaskazini “ B “.
Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema jamii katika baadhi ya maeneo Nchini imekuwa ikikosa utulivu wa kimaisha na hatimae kuingia katika mgongano baina ya jamii kutokana na baadhi ya walimu kuendeleza hulka ya kushawishi wanafunzi wao kujihusisha na masuala ya Kisiasa.
Alisema wakati umefika kwa walimu hao kuhakikisha kwamba wanasimamia vyema ufundishaji sahihi uliosisitizwa katika Qurani pamoja na maamrisho yote yaliyomo ndani ya mfumo mzima wa Dini ya Kiislamu.
Aliwataka waalimu na wananchi kuendelea kuwa na subra hasa wakati wanapoomba nguvu za ziada za kupatiwa misaada katika miradi yao ya maendeleo na hata ile ya Kidini.
Balozi Seif aliahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za Wananachi hao kwa kuongeza misaada zaidi bila ya kujali itikadi za kisiasa kwani dhima ya Uongozi inabakia pale pale ya kuwahudumia wananchi wote.
Naye kwa upande wake Mke wa Mbunge wa Jimbo hilo la Kitope Mama Asha Suleiman Iddi aliwatanabahisha walimu na wanafunzi hao wa Madrasat Qiyamu Islamia kuelekeza nguvu zao zaidi katika Ibada ili kufanikiwa vyema katika maisha yao ya milele.
Mama Asha alisema mafundisho mema ya walimu watakayowapa watoto wao ndani ya Madrasa mbali mbali Nchini ndio kigezo pekee kitakachowapa nidhamu ya kuheshimika ndani ya jamii iliyowazunguuka.
Mapema Balozi Seif alikagua kisima cha maji safi na salama cha Kijiji cha Mgambo ambacho kimejengwa kwa kutumia mfuko wa Maendeleo ya Jimbo la Kitope ili kuwaondoshea usumbufu wa huduma hiyo muhimu kwa Binaadamu.
Msimamizi wa Ujenzi wa Kisima hicho Afisa Mipangowa Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini B Nd. Ahmada Juma Kheir alimueleza Balozi Seif kwamba ujenzi huo hadi kufikia hatua ya matumizi umegharimu jumla ya Shilingi 13,000,000/-.
Akiwapongeza Wananchi hao kwa ustahamilivu wao kutokana na kukosa huduma hiyo wa muda mrefu Balozi Seif aliahidi kuweka Mashine pamoja na Ujenzi wa Tangi la kuhifadhia maji wakati huduma za umeme zitakapofika katika eneo hilo.
Akikabidhi msaada wa Vifaa vya uwezekaji kwa Tawi la CCM Mbaleni Balozi Seif ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM aliwapongeza wanachama wa Tawi hilo kwa uamuzi wao wa kujenga Ofisi itakayokuwa na hadhi ya Chama chenyewe.
Balozi Seif alieleza kwamba juhudi za Uongozi wa Jimbo hilo zitaongezwa zaidi ili kukamilisha ujenzi wa matawi mawili yaliyobakia kati ya Matawi 20 yaliyomo ndani ya Jimbo la Kitope.
“ Ukweli lilikuwa Tawi lenye kusuasua ujenzi wake kwa muda mrefu lakini hivi sasa limefikia hatua nzuri kiasi cha kuelekea kwenye agizo la Chama cha Mapinduzi la kuwataka Wana CCM kujenga Matawi yenye hadhi ya Chama chenyewe “. Alisisitiza Balozi Seif.
Aliwaomba wanachama wa chama cha Mapinduzi wa Jimbo hilo kuendelea kuunga mkono sera na ilazi ya Chama chao iliyopata ridhaa ya kuongoza Taifa hili la Tanzania.
Katika Ziara hiyo Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope Balozi Seif pia alikabidhi Shilingi Milioni moja kwa ajili ya kusaidia upatikanaji wa huduma za umeme katika kijiji cha Fujoni, vifaa vya kupikia chai kwa Maskuli yaliyomo ndani ya Jimbo hilo pamoja na vifaa vya kuezeka Tawi la CCM Mbaleni vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi Milioni 4.6.