Balozi Seif akisalimiana na Balozi wa Israel Nchini Tanzania Bwana Gil Haskel wakijiandaa na mazungumzo ya kuimarisha uhusiano kati ya Israel na Zanzibar.
Balozi wa Israel Nchini Tanzania Bwana Gil Haskel akimpongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kufuatia Tanzania kuendeleza mchakato wa katiba Mapya ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika misingi ya amani na utulivu.(Picha na Hassan Issa wa – OMPR)
Na Othman Khamis Ame. OMPR.
Serikali ya Israel imekusudia kuunga mkono harakati za Kiuchumi na Maendeleo ya Zanzibar ili kuona ustawi wa maisha ya Wananchi wa Zanzibar katika dhana nzima ya kukabiliana na ukali wa maisha na kupunguza umaskini inafanikiwa.
Kauli hiyo imetolewa na Balozi wa Israel Nchini Tanzania Bwana Gil Haskeli aliyefika nyumbani kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Bara bara ya Haile Selassie Jijini Dar es salaam kwa mazungumzo ya kuimarisha uhusiano kati ya pande hizo mbili.
Balozi Gil Haskel alisema amemua kufanya ziara maalum ya kutembelea na kukutana na Viongozi wa juu na waandamizi wa Wizara zinazohusika na Sekta za Kilimo na Afya Zanzibar ili kuangalia mazingira ya namna ya kuanza kutekeleza mpango huo.
Alisema Israel tayari imeshajitolea kusaidia mafunzo ya muda mrefu na mfupi kwa watendaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa Wizara za Afya na Kilimo kwa lengo la kuwajengea uwezo wa Kitaaluma utakaowapa fursa na nguvu kubwa ya kutekeleza majukumu yao Kitaalamu zaidi.
“ Tumeamua uwezo wetu wa Kitaaluma katika sekta za Kilimo na Afya tulionao katika kipindi kirefu hasa suala la kilimo cha umwagiliaji { Drop Irrigation } tunaweza kuwasaidia wenzetu ili nao wapige hatua za maendeleo “. Alisema Balozi Gil Haskel.
Balozi Gil ameipongeza Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kutokana na hatua yake ya kuendelea na mchakato wa kuelekea kwenye Katiba Mpya ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema yapo matumaini yaliyo wazi kwa Watanzania kuvuka katika kipindi hichi cha Mpito na cha Kihistoria tokea Uhuru wa Tanganyika na Mapinduzi ya Zanzibar cha mabadiliko hayo ya Katiba katika misingi ya amani na Utulivu.
Alifahamisha kwamba mchakato huu wa mabadiliko ya Katiba umetoa somo kwa mataifa mbali mbali Duniani na hasa yale Mataifa yaliyo jirani na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuiga mfumo huo.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameipongeza Israel kwa hatua zake inazoendelea kuchukuwa za kutaka kusaidia mafunzo watendaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zzanzibar kwenye Sekta za Afya na Kilimo.
Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliikumbusha Nchi hiyo kuafuatia ziara yake aliyoifanya ya Mwaka 2012 Nchini Israel kufikiria kuongeza nguvu zake za kusaidia kitengo cha Maafa Zanzibar.
Alisema Zanzibar imekuwa ikikabiliwa na matukio ya maafa kama zilivyo nchi nyengine duniani lakini Kitengo chake cha kukabiliana na maafa bado hakijawa na nguvu za kiutendaji kukabiliana na majanga wakati yanayotokea.
“ Bado Serikali ya Israel ina nafasi ya kusaidia kitengo cha Maafa ili kipate nguvu ku bwa ya kupambana na athari zinapotokea katika sehemu mbali mbali ya Visiwa vyetu “. Alifafanua Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Alieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejipanga kujenga Vituo vya kukabiliana na Maafa katika maeneo muhimu Unguja na Pemba ili kusaidia mafunzo pamoja na kutoka huduma wakati yanapotokea maafa katika maeneo ya karibu na vituo hivyo.
Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kupambana na umaskini imeshauri na kusimamia uanzishwaji wa Vikundi vya Ushirika hasa vile vya Saccos katika maeneo mbali mbali Nchini.
“ Vikundi mbali mbali vya Saccos vinazidi kuimarishwa ili kufikia hatua ya kukabiliana na ukali wa maisha sambamba na kupambana na umaskini miongoni mwa Jamii Nchini “. Alifafanua Balozi Seif.
Akizungumzia suala la uimarishaji wa Sekta ya Utalii Nchini Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimueleza Balozi wa Israel Nchini Tanzania kwamba Zanzibar inatarajia kuongeza kupokea Idadi ya Watalii kutoka laki 240,000 katika kipindi hichi na kufikia idadi ya watalii Laki 255,000 kwenye kipindi kijacho.
Alifahamisha kwamba juhudi za Serikali kupitia taasisi na hasa sekta binafsi zinazojishughulisha na sekta hiyo ya Utalii zinaendelea kuchukuliwa kuitangaza zaidi Zanzibar Kiutalii katika Nyanja za Kimataifa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kupitia Balozi Huyo wa Israel Nchini Tanzania Bwana Gil Haskel aliipongeza Nchi hiyo Kufuatia ziara yake aliyoifanya Nchini Israel mwaka 2012 ambayo ilileta mafanikio makubwa katika sekta za Afya, Kilimo na Kitengo cha Kukabiliana na Maafa.
Alieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi waliowengi wameonyesha faraja yao kutoka na Nchi hiyo kuendelea kupokea na kusaidia huduma za Afya hasa kwa watoto wa Zanzibar wenye Maradhi ya Moyo wanaofanyiwa Operesheni ya maradhi hayo Nchini Israel.