Na Mwandishi wetu, Dodoma.
WAJUMBE wa Bunge la Katiba jana walishindwa kujadili kanuni zitakazoongoza mkutano wa bunge hilo, baada ya baadhi ya wajumbe kukosa nyaraka.
Wajumbe hao walikutana jana katika mkutano wa kawaida wa kazi, lakini wakati nyaraka hizo zikigawiwa ilibainika kuwa baadhi ya wajumbe wamekosa.
Hali hiyo ilimlazimu Mwenyekiti wa muda wa bunge hilo, Pandu Ameir Kificho, kutangaza kuahirisha mjadala huo hadi Jumatatu.
Wajumbe walikuwa wakutane jana na leo kujadili kanuni hizo kabla ya kuzipitisha katika mkutano wa Jumatatu.
Kutokana na hali hiyo shughuli za kupitisha kanuni ambazo zilipangwa kufanyika Jumatatu sasa zitasogezwa mbele hali ambayo pia itachelewesha uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo .
Spika wa zamani wa Bunge, Samuel Sitta, anapewa nafasi kubwa ya kushinda nafasi hiyo, hata hivyo alisema hatachukua fomu hadi atakapoziona kanuni zitakazomuongoza kuongoza bunge hilo .
Wakati huo huo, habari kutoka Dodoma zinasema kuna mipango ya chini kwa chini inaandaliwa na wajumbe kujiongezea posho, ingawa baadhi yao wanapinga.
Wanaotaka kujiongeza posho wanadai kiwango cha shilingi 300,000 kwa siku hakitoshi huku wanaopinga wakisema zinatosha na nyengine kubaki.
Katika hatua nyengine wakati zoezi la usajili wa wajumbe likiendelea ilibainika wajumbe wawili walijitokeza wakitumia majina ya aina moja.