STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 21 Februari, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameihakikishia Serikali ya Uholanzi kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ina dhamira ya kweli ya kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wake na Uholanzi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alitoa kauli hiyo jana wakati alipokuwa akizungumza na Waziri wa Biashara za Nje wa nchi hiyo Bibi Lilianne Ploumen aliyemtembelea Ikulu.
“Ningependa kurejea tena dhamira yetu ya kuendeleza kushirikiana na serikali ya Uholanzi katika nyanja mbalimbali za maendeleo kwa faida za nchi zetu na watu wake” Dk. Shein alimueleza Bibi Ploumen.
Aliongeza kuwa Serikali na wananchi wa Zanzibar wanasubiri kwa hamu kuanza ujenzi wa wodi mpya ya kinama wajawazito na watoto katika hospitali ya Mnazi Mmoja ambayo itajengwa kwa ufadhili wa Serikali ya nchi hiyo kupitia Mpango wa ORIO.
Dk. Shein aliueleza msaada wa nchi hiyo katika sekta ya afya kuwa muhimu sana kwa ustawi wa wananchi wa Zanzibar na hiyo inaonesha jinsi Zanzibar na Uholanzi zilivyo marafiki.
Alimueleza Waziri huyo kuwa amepata faraja kusikia kuwa Serikali ya Uholanzi tayari imeleta timu ya wataalamu humu nchini kufanya utafiti wa uwezekano wa ujenzi wa bandari Zanzibar.
“Tunahitaji bandari ya kisasa hivi sasa iwe kwa ajili ya shughuili za abiria na mizigo au hata bandari ya mafuta na gesi zote ni muhimu kwa mazingira ya uchumi wa Zanzibar hivi sasa” alisisitiza Dk. Shein.
Halikadhalika Dk. Shein alimueleza Bibi Ploumen kuwa Serikali ya Zanzibar imefurahishwa na taarifa kuwa Uholanzi imetenga fedha maalum kwa ajili ya kuijengea uwezo Zanzibar katika kuendeleza rasilimali zake ikiwemo mafuta na gesi.
Kwa hivyo aliishukuru Serikali na wananchi wa Uholanzi kwa misaada yake hiyo na mengine ambayo imekuwa ikichangia na kuharakisha ufanikishaji wa malengo mbalimbali ya maendeleo nchini.
Dk. Shein alimshukuru waziri huyo kwa kutembelea Zanzibar kufuatia mazungumzo yake waliyofanya akiwa nchini Uholanzi mwenzi Agosti mwaka jana wakati alipofanya ziara rasmi nchini humo.
“Nilifurahi kusikia utafanya ziara nchini na leo nimerafijika zaidi kuona ujio wako umeambatana na ujumbe mzito wa makampuni kutoka nchini Uholanzi ”alieleza Dk. Shein na kuongeza kuwa hatua hiyo inafungua ukurasa mpya wa matumaini na ushirikiano wa miaka mingi ijayo kati ya Serikali na sekta binafsi.
Wakati huo huo Waziri wa Biashara za Nje wa Uholanzi bibi Lilianne Ploumen alisema kuwa Serikali ya nchi yake imeainisha maeneo ya ushirikiano na Zanzibar kufuatia ziara ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliyoifanya nchini Uholanzi mwezi Agosti mwaka jana.
“tangu ulipofanya ziara yako nchini kwetu Serikali yetu imekuwa ikiangalia namna bora ya kuisaidia Zanzibar katika kuendeleza rasilimali zake ikiwemo mafuta, gesi pamoja na miundombinu ya usafari wa baharini ikiwemo ujenzi wa bandari”alieleza Bibi Ploumen.
Katika kufanya hivyo alieleza kuwa Serikali ya nchi yake imetenga fedha maalum kwa ajili ya mafunzo ya kuijengea uwezo Zanzibar kuendeleza rasilimali zake ikiwemo sekta ya mafuta na gesi.
“Tumebaini (Serikali ya Uholanzi)maeneo ya kushirikiana na makampuni utakayoonana na leo(jana) yana weledi mkubwa katika maeneo hayo ambayo ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya usafiri wa baharini, ujenzi wa bandari, mafuta na gesi, mapato na kodi katika rasilimali na taasisi ya mafunzo”alifafanua Bibi Ploumen.
Alieleza kuwa ujio wa makampuni hayo kutoka nchini kwake ni sehemu ya jitihada za serikali ya nchi yake na Zanzibar ya kuimarisha uhusiano baina ya serikali zao na ushirikiano baina ya sekta binafsi za nchi mbili hizo.
Mazungumzo hayo yalihudhuria pia na baadhi ya mawaziri na Mkatibu wakuu pamoja na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822