Diaspora ya Wazanzibari na Watanzania.
Katiba mpya itaonyesha!
Na Omar Ali.
Mwenyekiti wa ZADIA.
Jamhuri ya Muungano wa zilizokuwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika zilizoungana na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar; baadae kuitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wengi wanaijua kama Tanzania; imeamua kutengeneza katiba mpya.
Kwenye katiba hiyo, kuna makundi ya aina kwa aina, yanayotaka mambo tofauti yafanyike. Maarufu kati ya makundi hayo ni yale yanayotaka mabadiliko ya muundo wa Muungano wa hizo Jamhuri zilizokuwepo kabla, ambapo tume iliyokusanya maoni inasema zaidi ya asilimia 60 kwa Zanzibar na kwa Tanganyika asilimia 61 wanataka mfumo wa Muungano uliopo ubadilike. Lenye nguvu ni kundi la chama tawala CCM, wanaotaka mfumo wa Muungano na Serikali uliopo sasa hivi ubakie.
Kuna wengine wanaotaka mabadiliko ya ushiriki wa mambo ya nje kwa kila nchi. Wote wanakubaliana kwamba sheria za nchi za kikatiba zilizokuwepo kabla ambazo ni muafaka na matakwa ya wananchi ziendelee kuwepo kwenye katiba mpya.
Kuna kundi kubwa la raia waliokuwa raia wa hizo nchi mbili kabla ya Muungano na baadaae kwa sababu na awamu moja au nyengine, walihamia kwenye nchi tofauti, nje ya hizo nchi mbili za awali. Baadhi yao walilazimika kuchukua uraia wa nchi walizohamia.
Kwa mujibu wa sheria ambazo zinaaminika zilihofia enzi za vita baridi. Sheria za uraia za Tanzania zinasema kwamba, mtu yeyote akichukua uraia wa nchi nyengine anapoteza uraia wa Tanzania.
Kundi hilo la watu wapatao milioni mbili, linapiga kelele kujaribu kuwatanabahisha wahusika wote wanaotengeza katiba mpya kwamba, kwenye katiba hiyo kuwe na kifungu rasmi kinachoeleza wazi wazi kwamba, mtu yeyote mwenye asili ya Tanzania ama kwa upande wa baba, au wa mama, au pande zote, basi ana haki ya kuwa raia wa Tanzania hata kama amechukuwa uraia wa nchi nyengine.
Kwa maana nyengine, mtu akipenda kuwa na uraia wa nchi mbili au uraia pacha aruhusiwe.
Bahati mbaya mpaka sasa haijaonekana kwamba; suali hili ingawa linawaunganisha watu wa mirengo yote, kwenye Jamhuri zote za iliyokuwa ya Watu wa Zanzibar na Tanganyika. Watu hao wanajihisi kama kwamba hawatakiwi nchini kwao. Hapa nataka kutoa ufafanuzi wa hisia hizo kwa ufupi.
Tukiangalia hali ya wanaoishi nje ya Tanzania na kuamua kuchukua uraia wa nchi hizo utaona kwamba, walilazimika kufanya hivyo kwa lengo la kurahisisha maisha yao na ndugu zao waliowaacha huko nyuma. Ama wamechukua uraia mpya kwa kutaka kupata elimu, matibabu, huduma za jamii au kutosumbuliwa tu na sheria za nchi wanazoishi sasa hivi.
Kwa lugha ya mkato wengi husema tunatafuta maisha.
Kwa vile wengi wao wamehamia kwenye nchi zilizoendelea zaidi kuliko Tanzania, watu hao wamejiendeleza kielimu na kimaisha na wakati wote huo wanagawana faida ya hatua zao na ndugu zao na Taifa walilotoka.
Kama ambavyo Muungano ulivyoundwa kurahisisha baadhi ya mambo kwa wananchi wa nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar na nchi zenyewe, ndio vivyo hivyo watu hawa walivyoamua kutafuta mazingira bora ya maisha ili kurahisisha mambo kwa watu wao.
Muungano uliopo umewafanya Wazanzibari kuwa watu wa nchi mbili, Tanganyika na Zanzibar na Watanganyika kuwa watu wa nchi mbili, yaani Zanzibar na Tanganyika. Jambo hili liliwezekana kwa makubaliano tu ya aliyekuwa Raisi wa Jamhuri ya watu wa Zanzibar, sheikh Abeid Amani Karume na Raisi wa Jamhuri ya Tanganyika Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Kwenye kundi hilo la watu milioni mbili walioko ughaibuni, utaona kuna wengi wa watoto, ndugu jamaa na marafiki wa viongozi wakuu wa serikali zote mbili za Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano wa Tanzania.
Nitajie kiongozi yeyote maarufu wa Tanzania ambaye hana ndugu, jamaa au rafiki wa karibu sana ambae amehamia nchi nyengine, hasa ya mbali. Kuna pia watoto wa wavuja jasho ambao, wao ndio hasa waliohamia kwenye nchi zao za sasa hivi ili kupata manufaa na faida ya kuhamia kwenye nchi zilizoendelea ili kusaidia ndugu zao, lakini mioyoni mwao, siku zote wanajisikia na kuumiya kukosa kuwa makwao kwa wote Wazanzibari na Watanganyika.
Huo ni upande wa hisia na mahusiano.
Tukija kwenye upande wa mapato. Zaidi ya watu husika, Tanzania ndio inayofaidika zaidi kwa kuwa na watu wake nje ya nchi. Inafaidika kwa kukusanya fedha za kigeni ambazo wahajiri hao walioo nje wanatuma kwa ndugu na jamaa zao. Inafaidika wakati wahajiri hao wakitembelea Tanzania. Inafaidika kwa wahajiri hao, kutokana na uzalendo wao, kuwaunganisha watu wa nchi wanazoishi na Tanzania na hatimae watu hao kuwekeza nchini na inafaidika kwa mambo mengine mengi ambayo si moja kwa moja.
Ili kuelezea faida zinazopatikana na kuzitia sura, nitatoa mfano mmoja hapa. Kikawaida Watanzania na Wazanzibari wakiumwa na kukawa hakuna matibabu nchini wanapelekwa nchi za nje kutibiwa.
Bila shaka wengi wanaopata huduma hiyo ni wale walio kwenye tabaka la ama kuwa na kitu au kujua mtu wa juu kama sio mwenyewe kuwa kiongozi wa ngazi za juu.
Ikitokezea hivyo, Serikali ama ya Zanzibar au ya Muungano hulazimika kutowa zaidi ya Shillingi za kitanzania milioni 60 kwa kila mtu mmoja. Watanzania wenye ndugu zao nchini ambao wanaumwa na kuwa na uwezo, wanawapokea ndugu zao hao na kuwatafutia matibabu na serikali haigharimiki hata shilingi moja.
Hiyo ni faida ya moja kwa moja kwa Tanzania kwani wananchi waliokuwa wake, wamepata uraia wa nchi nyengine na wana haki ya kuwasaidia ndugu zao watibiwe.
Hivi karibuni niliangalia video moja ambamo Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambae kwa mujibu wa maelezo mengi niliyosoma, inaonyesha kwamba hana tatizo na suala la Watanzania kuwa na uraia pacha.
Alisema kumjibu Daktari wa fani ya urojo wa ndani ya mifupa aliyeuliza suali kuhusiana na uraia pacha. Dr, Kikwete alijibu kwa kusema kwamba suala hilo litaangaliwa. Na akatania kwa kusema kwamba yeye haoni tatizo na alimuamuru Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ndugu Membe alliweke hili suala hadharani.
Akasema lilipokewa, lakini watanzania wanasema “Sasa hawa mbona wanataka huku na huku. Si walihama kwa hiari yao?” Na akaongezea, “Profesa mmoja wa pale chuo kikuu alikuwa ni mmoja wa wapinzani hasa.” nilivyoelewa anamaanisha kwamba wasomi ndio wapinzani wa suala la uraia pacha. Kulikoni?
Nimefuatilia video hii kwenye Michuzi Blog, Kuna baadhi ya wachangiaji wanadiriki kusema eti “TANZANIA NI NCHI YA PASPOTI MOJA”. Huu ni ufinyu na mawazo mgando, kwani haulinganishi faida na hasara zilizopo kwa Tanzania kuwa na uraia pacha. Kwanza kwa kuanza kufikiria ni kuangalia, kwani hiyo Tanzania imekujaje? Jee kama waasisi wa Tanzania wangekuwa na mawazo mgando, ingekuwapo. Au tungekuwa bado tuna Tanganyika na Zanzibar kama zamani?
Kwa mujibu wa maelezo yanayopatikana kwenye mtandao, kuna nchi kama 23 za Afrika ambazo zinakuballi uraia pacha kwa njia moja au nyengine. Nchi hizo kwa majina ni: Angola, Benin, Burundi, Cote d’Ivoire (bila ya uwezo wa kushika vyeo vitatu vya juu kabisa), Djibouti,Egypt (kwa ruhusa maalum), Eritrea (kwa ruhusa na imetayarisha njia ya mpito), Gabon, Gambia, Ghana (Raia pacha hawezi kuwa na cheo cha juu ), Kenya, Lesotho, Morocco, Mozambique, Namibia, Nigeria, Rwanda, Sao tome & Principie , Sierra Leone, South Africa (kwa ruhusa maalum kwenye wizara ya mambo ya ndani), Togo, Tunisia, Uganda.
[Kutoka hapa]. Tanzania, Zambia na Zimbabwe zinatajwa kwamba utayarishaji wa sheria uko kikaangoni. Najiuliza suali hapa, kwa nini Tanzania inayokuwa mstari wa mbele kwenye ukombozi na masuali mengine yote iwe imeachwa nyuma na hizi nchi 23?
Natarajia pia kwamba haitabaki nyuma zaidi ya hapa na Uraia pacha utawekwa kwenye katiba kama Diaspora inavyopendekeza.
Makala hii fupi naiandika kama changamoto kwa jamii kuendeleza dialogue, ambayo kama ikieleweka na kutumia fursa hii ili kuwapatia wale wote waliozaliwa ama Tanganyika, au Zanzibar au Tanzania uwezo wa kuwa raia wa Nchi zaidi ya moja.
Kwa kufanya hivyo, Tanzania itakuwa tena imeshinda wengine kwa fikira endelevu kwa kuanzisha Muungano wa Nchi mbili zilizokuwa huru za Tanganyika na Zanzibar, baadae kwenye katiba mpya, baada ya kuyatafakari yale yote yenye uzito wa hali ya juu, wahusika hawakusahau kwamba, pamoja na watu milioni arubaini waliomo nchini, kuna ndugu zao milioni mbili, ambao kwa sasa wanajihisi kama “watu wasiotakiwa kwao”, lakini katiba mpya imewafungulia milango na kujiona na wao ni sehemu ya Jungu kuu liitwalo Tanzania.