Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Simanzi. JK aongoza mamia kuiaga miili

$
0
0
Na Juma Khamis
SIMANZI, huzuni na vilio vilitawala jana wakati miili ya wanajeshi wawili kutoka Zanzibar, ilipowasili uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Karume, ikitokea Dar es Salaam.

Miili ya wanajeshi hao Sajenti Shaib Shehe Othamn na Koplo Mohammed Juma Ali iliwasili majira ya saa 8:52 mchana kwa ndege ya kijeshi yenye namba JW 9034 na kupokelewa na Mkuu wa Brigedi ya Nyuki, Brigedia Sharif Sheikh Othman.

Wanajeshi walijaza eneo zima la uwanja wa ndege sehemu ya watu maarufu, wakionekana wenye huzuni kubwa.

Baada ya miili ya wanajeshi hao kutolewa ndani ya ndege ilibebwa na wapiganaji wa JWTZ na kupakiwa kwenye magari maalum.

Vilio vilianza baada ya wafiwa na vizuka na familia za marehemu hao kushuka kwenye ndege hiyo, ambapo ndugu zao waliokuja kuwapokea walishindwa kujizuia baada ya kushuhudia miili ya wapendwa wao kwa mara ya mwisho kabla ya kupelekwa katika safari ya milele.

Baba wa Sajenti Shaib, Sheikh Othman ambae alisafiri pamoja na mwili wa mtoto wake kutoka Dar es Salaam alishuka kwenye ndege akiwa amejikaza, lakini baada ya kukutana na ndugu zake alishindwa kujizuia na kujikuta akilia kwa uchungu mfululizo bila kunyamaza.

“Nimempoteza mtoto wangu, yeye alikuwa ndie msaidizi wangu, ahhhhhhhhhh,” alilalamika huku ndugu zake wakimpoza kwa kumpigapiga kwenye mabega, wakimwambia ‘nyamaza hii ndio safari ya kila kiumbe cha Mwenyezi Mungu, yeye ametangulia na sisi tuko nyuma yao, cha muhimu ni kumuomba Mwenyezi Mungu awape makazi mema.”

Vizuka, wakiongozana na watoto wao huku wakisaidiwa na wanawake wa kijeshi, walionekana wenye majonzi na huzuni wakikumbuka jinsi walivyokuwa pamoja na waume zao kabla ya vifo wakikumbuka mchango wao katika ujenzi wa familia.

“Mume wangu nilikuwa nampenda, ameniachia watoto, ameondoka bila taarifa, bila kumuona,” alilia kwa uchungu mmoja ya wanawake wa wanajeshi hao, huku wanajeshi wa kike wakiwapoza, kuwafariji na kuwaongoza hadi katika gari walilopangiwa kupanda.

Miili ya wanajeshi hao iliondoka uwanjani hapo majira ya saa 9:30 alasiri ikiongoza na msafara wa karibu magari 25 yaliyosheheni wanajeshi, ndugu, watendaji wa serikali ikipitia barabara ya uwanja wa ndege, kituo cha polisi Mazizini hadi Kilimani, ili kutoa nafasi kwa wananchi waliojazana barabarani kupata fursa kushuhudia miili ya mashujaa wao.

Baada ya kufikia chuo cha mafunzo Kilimani, msafara ulielekea barabara ya skuli ya Jang’ombe kuelekea barabara ya Kwamchina kuushusha mwili wa Sajenti Shaibu katika mtaa wa Mpendae ambako ndiko familia yake imeweka matanga.

Baadae msafara huo ulieleka Kwarara kuupeleka mwili wa Koplo Mohammed kwa taratibu za kuagwa na familia yake.

Mazishi ya wanajeshi hao yatafanyika leo majira ya saa 4:00 asubuhi katika makaburi ya Mwanakwerekwe na yatafanywa kwa taratibu zote za kijeshi.

Mbali ya miili ya wanajeshi kutoka Zanzibar, ndege iliyowaleta pia ilikuwa imebeba miili ya wanajeshi wengine ambao walisafirishwa katika mikoa mengine ya Tanzania kwa taratibu za mazishi.

Wanajeshi hao pamoja na wenzao watano waliuawa Jumamosi iliyopita katika jimbo la Darfur nchini Sudan baada ya kushambuliwa na waasi.

Katika tukio hilo wanajeshi wengine 14 walijeruhiwa na wanaendelea kupatiwa matibabu.

Nae Mwantanga Ame anaripoti kutoka Dar kuwa, Mapema jana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Rais Jakaya Kikwete aliwaongoza Watanzania kuiagia miili ya wanajeshi hao katika viwanja vya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Upanga jijini Dar es Salaam kabla ya kusafirishwa katika maeneo waliyotoka.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Kikwete alisema waliotekeleza mauaji hayo wana roho ngumu na kushangazwa na kitendo cha waasi hao kuwaua watu wanaowasaidia kupata utulivu, ili kunusuru maisha yao, kuwaondolea wasiwasi na kuwawezesha wafanye shughuli zenye tija kuendesha maisha yao.

Alisema tangu walinda amani wapelekwe Darfur mwaka 2007,walinzi wa amani 41 kutoka mataifa mbalimbali wameuawa na wengine 55 wamejeruhiwa.

“Kwa kweli idadi hii ni kubwa mno inayohitaji kutafakariwa vizuri na wadau wote. Pengine wakati umefika wa kuutazama upya mfumo wa kulinda amani Darfur hasa kuhusu uwezo wa kujilinda na wanajeshi wanaolinda amani. Hapana budi uwezo wao uongezwe ili kupunguza vifo na majeruhi. Narudia kuahidi kuwa rai hii tutaifikisha kwa mamlaka husika katika Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika,” alisema Rais Kikwete.

Rais Kikwete alitoa pole kwa familia na wafiwa wa marehemu na kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu aziweke roho zao mahala pema peponi, amiin.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi na viongozi wengine wa vyama na serikali.




Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>