Na Joseph Ngilisho,ARUSHA
KANISA la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT), limewaonya wake wa watumishi wa kanisa hilo kuacha kuvaa nguo za kubana na zinazoacha wazi sehemu kubwa ya miili yao kwa sababu kitendo hicho ni ukiukaji wa maadili ya kanisa.
Kauli hiyo ilitolewa na Askofu wa Kanisa hilo, kanda ya kaskazini, Martin Shao, kwenye ibada maalumu ya kumtawaza mchungaji mpya wa kanisa hilo, Godlisten Wilison Mkenda, kuingia daraja la uchungaji,iliyofanyika kanisa la KKKT usharika wa Salei jimbo kuu la Arusha.
Alisema watumishi wa mungu wamekua na changamoto kubwa katika kutoa huduma kwa waumini na muda mwingine inasababishwa na wachungaji wasiokua na imani ya kutosha kwa kushindwa kuyakabili majaribu kutokana na vishawishi.
Alisema pamoja na changamoto hizo, wakati mwingine zinachangiwa na baadhi ya wake wa watumishi na waumini kwa kuvaa nguo zisizofaa na kuwaingiza watumishi katika majaribu.
Alisema wake wa watumishi wamekuwa wakishindana na mambo ya kidunia na kusahau kuwa wao ndio kioo cha jamii na wanapaswa kuwa na maadili mema.
Alisema Wakristo watambue kuwa majaribu yapo kwa kila binadamu lakini anayo nafasi ya kukabiliana nayo na kuyashinda,na kwamba yapo majaribu mengine ambayo umfanya mtu kukomaa na hatimaye kupata ushindi wa uzima.
Aidha aliwataka watumishi wa serikali na siasa kulifuata neno la Mungu kwani wanakumbana na majaribu makubwa maofisi na wakati mwengine yanawashinda.
Kwa upande wake, Mchungaji Godlisten Mkenda, aliseam anamshuku Mungu kwa tukio hilo kwani ni malengo yake ya siku nyingi kuwa mchungaji.