Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Wawakilishi: ZBC iangaliwe

$
0
0
Na Mwantanga Ame
KAMATI ya Mifugo Utalii, Uwezeshaji na Habari ya Baraza la Wawakilishi, imesema Shirika la Utangazaji (ZBC) inahitaji kuangaliwa kwani serikali imetumia kiasi kikubwa cha fedha kutekeleza miradi ya shirika hilo.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo,Mwakilishi wa Bumbwini, Mlinde Mbarouk Juma, alisema mradi wa digitali unahitaji umakini wa hali ya juu katika uendeshaji wake kwa kuhakikisha wafanyakazi wa ZBC wanabadilika.

“Kwa kutokuwa makini tutakuja kulaumiana na kuona ni bora tungelibaki katika mfumo wa analogia, na tukumbuke serikali imetumia fedha nyingi kuingia katika fumo huu,” alisema.

Wakichangia bajeti hiyo,Wawakilishi walianisha kasoro nyingi katika shirika hilo, wakisema utendaji wake si wa kuridhisha.

Baadhi ya wajumbe walisema hawataiunga mkono bajeti hiyo kwa kuwa kitabu cha bajeti hakijajibu mapungufu yaliyomo ndani ya wizara.

Wawakilishi Hija Hassan Hija (Kiwani), Viwe Khamis, Ismail Jussa Ladhu (Mji Mkongwe), Makame Mshimba Mbarouk (Kitope), Mussa Khamis (Koani) walisema bado kuna tatizo la upatikanaji wa matangazo ya katikia mfumo wa dijitali.

Walisema tangu kuanza mfumo huo kuna mafanikio kidogo, kutokana na baadhi ya maeneo hasa ya Pemba, kukosekana matangazo ya televisheni ya ZBC.

Walisema wanashangaa kuona hali hiyo inaendelea kutokana na serikali kuamua kutoa kazi hizo kwa kampuni ya AGAPE baada ya kuikubali kuwa ina sifa ya kufanikisha kazi hiyo, lakini la kushangaza kampuni hiyo inaonekana imeshindwa.

Walisema hali hiyo, imekuwa ikiwapa wasiwasi juu ya mradi huo na uendeshaji wa ZBC baada ya kuwepo taarifa za mgongano wa mara kwa mara kati ya watendaji wa Wizara na Shirika hilo.

Walisema hali hiyo, inaweza ikawa moja ya chanzo kikuu cha kuufanya mradi huo kushindwa kufanya kazi vizuri, na ni vyema wizara ikaweka wazi.

Wakichangia maeneo mengine, Wawakilisji walisema ipo haja ya taasisi nyengine kuangaliwa vizuri ikiwemo Shirika la Magazeti ya Serikali kwa kulipatia mitambo kwa kuwa hivi sasa magazeti yanayozalishwa na shirika hilo yanachapishwa Tanzania Bara.

Aidha, wajumbe waliitaka wizara kuendeleza kutoa elimu kwa watumishi wake ili waweze kutekeleza majukumu yao.

Wajumbe hao walilalamikia malipo ya posho za watumishi wa taasisi za habari wanaoripoti vikao vya Baraza la Wawakilishi.

Walisema wafanyakazi hao wanalipwa posho la shilingi 5000 kwa kikao, lakini pia hicho kidogo kinachelewa kutolewa.

Nae Mwakilishi wa Magomeni na Kwamtipura, Hamza Hassan Juma, alisema lawama zinazotupwa ZBC, hazikustahili kwani Wawakilishi ndio waliotoa wazo kwa serikali kubadili mfumo wa uendeshaji kutoka Idara kuwa shirika.

Alisema katika mapendekezo hayo, wajumbe walisahau kuishauri na kuisimamia serikali kufanya mabadiliko katika maeneo ambayo yataihusu serikali moja kwa moja katika kutafuta watendaji wa kuliendesha.

Alisema Shirika hilo kabla ya kuanza kazi zake ilitakiwa kupunguza wafanyakazi kwa kuacha wasio na tija na kubakisha watendaji bora lakini hilo halikufanyika.




Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles