Hafsa Golo na Haroub Hussein
WATU 24 wakiwemo wanajeshi watatu wamejeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuelekea kwenye maziko ya wanajeshi waliouawa katika jimbo la Darfur nchini Sudan, kupinduka katika maeneo ya Mwanakwerekwe, mita 100 tu kutoka yalipo makaburi.
Ajali hiyo ililihusisha gari linalomilikiwa na jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) aina ya Defender namba 2953JW04, lililokuwa kwenye msafara uliowahusisha wanajeshi na raia waliokuwa wakielekea kwenye mazishi hayo.
Baada ya ajali hiyo, wanajeshi waligawana ambapo wengine walishughulikia mazishi ya wenzao na wengine kushungulikia majeruhi na kuwakimbiza hospitali kuu ya Mnazimmoja.
Majeruhi 17 wakiwemo wanajeshi wawili wametibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani na wengine saba akiwemo mwanajeshi mmoja wamelezwa kwa matibabu kutokana na kupata majeraha makubwa.
Mwandishi wa habari hizi aliefika katika eneo la ajali alishuhudia gari hilo likiwa limelala ubavu kabla ya wanajeshi kwa kushirikiana na raia hawajaliinua.
Kulikuwa na idadi kubwa ya watu katika makaburi ya Mwanakwere, eneo lililotokea ajali na katika hospitali ya Mnazimmoja, kila mmoja akitaka kufahamu kama ndugu zao hawamo kwenye ajali hiyo.
Daktari Mkuu kitengo cha mapokezi, Dk. Juma Mambi, ameliambia gazeti hili kwamba majeruhi waliolazwa wanaendelea na matibabu na hali zao zinaendelea vizuri.
Alisema majeruhi wengi wameumia sehemu za kichwa na uso.
Miongoni mwa waliojeruhiwa zaidi ni Said Ali Sheha, Hafidh Omar Ali, Jafar Ali Jafar, Salum Kassim Mansour, Seif Ali Mbaruok na Shuwaib Yussouf Abdi.
Hakukuwa na majeruhi wanawake kwakuwa dini ya kiislamu haiwaruhusu wanawake kwenda makaburini kuzika.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadamu Khamis Mkadamu,amethibitisha ajali hiyo na kusema gari hilo lilikuwa likiendeshwa na mwanajeshi aliemtaja kwa jina la Salum Kassim Mansour, ambae nae amejeruhiwa na kulazwa hospitali.
Aidha alisema gari kama hilo kwa kawaida lilitakiwa kubeba abiria 10-12 lakini ilibeba watu wengi na kusababisha kuyumba na hatimae kupinduka.
Mmoja wa majeruhi, Kassim Ali Mohammed mkazi wa Darajabovu akisimuliwa ajali hiyo alisema baada ya kupinda makutano ya barabara ya Mwanakwerekwe, Amani na Mombasa, gari hilo liliyumba na kutulia lakini lilipofika eneo la Asha Fatuma ilipinduka.
Hata hivyo alisema gari hiyo ilikuwa katika mwendo wa kawaida kwani likuwa kwenye msafara kuelekea makaburini.
Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein aliwaongoza mamia ya wananchi katika maziko ya Sajenti Shaib Shehe Othman na Koplo Mohamed Juma Ally yaliyofanyika jana asubuhi katika makaburi ya Mwanakwerekwe.
Viongozi wengine waliohudhuria ni Mkuu wa Brigedi ya Nyuki, Brigedia Jenerali Sharif Sheikh Othman, Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, Mawaziri wa SMZ na SMT, ndugu,wananchi, wanajeshi, polisi, askari wa vikosi vya SMZ na viongozi mbali mbali wa vyama na serikali.
Wanajeshi hao walizikwa kwa heshima zote za kijeshi ikitangulia maiti ya Sajenti Shaibu na kufuatia Koplo Mohamed.
Kabla ya kuzikwa, maiti za wanajeshi hao zilisaliwa katika msikiti wa Noor Muhammad ulioko Kwa Mchina ambapo sala iliongozwa na Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Khamis Haji.
Viongozi wengine waliohudhuria ibada hiyo ni Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad, Mawaziri wa SMZ, SMT na Waislamu.
Wanajeshi hao ni miongoni mwa wanajeshi saba waliouawa Julai 13 katika jimbo la Darfur baada ya kushambuliwa na waasi.
Mungu azilaze roho za marehemu mahala pema peponi na majeruhu wapone haraka.