Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

‘Usasa unaongeza magonjwa yasiyoambukiza’

$
0
0
Na Salum Vuai, MAELEZO
MIFUMO ya kisasa ya kuishi ambapo watu wengi wanaiga mila za kimagharibi, imeelezewa kuwa inachangia sanaongezeko la magonjwa yasiyoambukiza hapa Zanzibar.

Akitoa mada katika warsha ya siku mbili ya kujadili mpango kazi unaojadili namna na kupambana na magonjwa hayo inayofanyika hoteli ya Zanzibar Ocean View iliyoko Kilimani mjini Zanzibar, Meneja wa kitengo cha maradhi yasiyoambukiza-‘NCD’ Dk. Omar Mwalimu alisema, njia pekee inayoweza kufanikisha kupunguza magonjwa hayo, ni kwa jamii kufuata mfumo wa asili wa kuishi.

Alifahamisha kuwa, miongoni mwa mambo yanayowaathiri sana watu, ni matumizi ya tumbaku na sigara, kunywa pombe na kutokuishughulisha miili yaokwa kufanya mazoezi.

Dk. Mwalimu alisema, utafiti uliofanywa mwaka 2011 kubaini chanzo cha magonjwa yasiyoambukiza, umegundua kuwa asilimia 7.3 ya wananchi wa Zanzibar wanatumia bidhaa za tumbaku, asilimia 1.7 wanakunywa pombe, na asilimia 18 tu ndio wanaofanya mazoezi.

Aidha alisema, utafiti huo umeonesha asilimia 33 ya wananchi, wanakabiliwa na ugonjwa wa presha.
Alieleza kuwa, katika kila watu watatu, mmoja kati yao anaugua presha, ambapo asilimia 3.7, (watu 48,000 hadi 50,000) hapa 
Zanzibar wanaishi na ugonjwa wa kisukari.

Hata hivyo, alisema ongezeko hilo limeanza kubainika kwenye miaka ya 90, baada ya jamii na serikali kutanabahi, ambapo hapo kabla mkazo mkubwa ulikuwa umeelekezwa katika  maradhi mengine, ikiwemo malaria na baadae UKIMWI.   

Aidha, alifahamisha kuwa, asilimia kubwa ya wananchi wa Zanzibar hawana utamaduni wa kula mbogamboga na matunda katika milo yao, jambo ambalo linawakosesha virutubisho muhimu miilini mwao ambavyo vina nafasi kubwa ya kujenga afya na kuwaepusha na maradhi mbalimbali.

“Watu wengi wanadhani kula chakula kingi ndio muhimu, lakini hawajali ubora na umuhimu wa vyakula vinavyohitajika kwa afya zao,” alisema.


Alisema umefika wakati sasa serikali kupitia sekta na wizara zake mbalimbali, zichukue nafasi yao katika kuielimsha jamii juu ya haja ya kuzingatia taratibu nzuri za kuishi, na kupunguza vyakula vya kisasa ambavyo madhara yake ni makubwa kuliko manufaa.

Baadhi ya washiriki wa warsha hiyo, walishauri hatua mbalimbali zichukuliwe, ikiwa pamoja na kupiga marufuku uingizaji wa sigara na pombe, ili kuinusuru jamii na janga la magonjwa yasiyoambukiza.

Wengine walipendekeza kukatazwa uuzaji wa baadhi ya vyakula maskulini hasa vinavyoweza kuwaathiri watoto kiafya, na badala yake wafanyabiashara wa maskulini wahamasishwe kuuza vyakula  vya asili pamoja na matunda.

Aidha, walisema suala la kufanya mazoezi na la mtu binafsi lakini anahitaji kuelimishwa ili asiuendekeze mwili, na badala yake wafanye mazoezi japo ya kutembea na kupunguza kupanda gari hata kwa safari ya masafa mafupi.

Akizungumza katika warsha hiyo iliyokuwa na mada mbalimbali, Mwakilishi wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) Neema Kileo, alisema wananchi wa Zanzibarwanapaswa kutumia vyema neema ya mazao ya matunda yanayopishana kila baada ya kipindi kifupi badala ya kukumbatia vyakula vya kizungu.

Aidha aliwataka wataalamu wa sekta ya afya, kuwa na mikakati maalumu ya kusambaza elimu kwa wananchi ili wahamasike kutumia vyakula vya asili zikiwemo mbogamboga na matunda, badala ya kukimbilia kuviuza huku wenyewe wakipuuza kuvila.

Warsha hiyo inatarajiwa kufungwa leo.   

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>