Na Othman Khamis, OMPR
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amesema jamii inapaswa kuendelea kuheshimu jukumu la walimu waliopewa jukumu la kuwafinyanga watoto.
Balozi Seif alieleza hayo ofisini kwake Vuga katika hafla fupi ya kuukabidhi uongozi wa skuli ya msingi ya Uzini ya Wilaya ya Kati mashine ya kudurufu (photocopy), meza pamoja na wino zake ili kusaidia machapisho ya kazi za skuli hiyo.
Makabidhiano hayo ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa mwaka 2011 wakati akiwa mgeni rasmi kwenye sherehe za kuwazawadia wanafunzi bora wa skuli hiyo.
Alisema ufinyanzi wa watoto kitabia, kimaadili na kitaaluma ni kazi ya wito na ni ngumu ambayo inahitaji kuungwa mkono na jamii ili iweze kutoa matunda bora.
Aliuomba uongozi wa skuli hiyo kuhakikisha mashine hiyo ambayo ni hazina kwao wanaitumia vizuri kwa lengo lililokusudiwa.
Aliwapongeza walimu na wanafunzi wa skuli hiyo kwa ustahamilivu wao wa muda mrefu tokea kutolewa ahadi hiyo ambayo ilichelewa kutokana na mawazo yaliyochanganya kufikiria kwamba kilichokuwa kikihitajiwa katika maombi ya skuli hiyo ni kompyuta badala ya mashine hiyo.
Akitoa shukrani kwa niaba ya walimu na wanafunzi wa skuli hiyo, Mwalimu Mkuu Msaidizi,Tatu Ame Suleiman alisema msaada huo umeleta ukombozi kwao.
Alisema eneo kubwa la Uzini hadi Mchangani lilikuwa likikosa huduma hizo jambo ambalo lilileta usumbufu hasa kwa walimu na wanafunzi wakati wa vipindi vya mitihani ya majaribio sambamba na kazi za kila siku ya kiutawala.
Mwakilishi wa jimbo la Uzini, Mohamed Raza Hassan alisema msaada huo utaongeza ujirani mwema kati ya wananchi wa jimbo la Uzini na wale wa Kitope.
Aliushauri uongozi wa skuli hiyo kuandaa utaratibu maalum utakaowezesha matumizi bora ya mashine hiyo na kutoa huduma kwa wananachi wengine wa kawaida katika eneo hilo.
Vifaa hivyo vina thamani ya shilingi milioni 1.5.