Na Benedict Liwenga, Maelezo
WAZIRI wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amewaasa vijana kutoa maoni yao juu ya uundwaji wa katiba mpya ambayo haitajenga mifumo ya serikali ya udikteta, ubinafsi na ambayo haitaibebesha mzigo serikali.
Alitoa nasaha hizo jana wakati akifungua rasmi Baraza la Vijana la Taifa la Katiba lililoandaliwa na Taasisi ya Vijana ya Tanzania Youth Coalition (TYC) kwa kushirikiana na Restless Development, UNFPA na ILO lililojumuisha vijana 120 kutoka Wialaya 50 za mikoa yote Tanzania Bara na Zanzibar na ambao wanatoka mashirika mbalimbali, asasi, jumuiya na vikundi vya vijana.
Waziri Sitta aliwaasa vijana kuwa wana jukumu kubwa la mapambano kupinga ulafi katika mambo ya uongozi, udikteta na ubinafsi kwani vinailetea mzigo serikali.
“Mtu ajue kuwa kutumia madaraka kwa manufaa yake mwenyewe ni mwiko,” alisema.
Alisema vijana nchini wanatakiwa wawe wanaharakati katika kujali maadili mema na kusimama kwa dhati kupigania haki na usawa nchini.
Alivishukuru vyombo vya habari kwa mchango wake mkubwa wa kufanya kazi ya kuhabarisha umma.
Pia ameipongeza taasisi ya vijana kwa kuandaa baraza hilo kwa vijana wenzao kwani litawasaidia kutambua mabo ya msingi yanayohitajika kuwepo katika katiba mpya.
Waziri Sitta alisema kama vijana hawatakuwa makini watapata katiba yenye athari kwa maisha yao, hivyo akawataka watumie fursa hiyo vizuri.