Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar
Jumuiya ya Wazamiaji na Uokozi Zanzibar imetakiwa kutanua wigo wa utendaji kazi zake ili pia ijishughulishe na uhifadhi wa mazingira badala ya kufanya kazi za uokozi baharini pekee.
Jumuiya ya Wazamiaji na Uokozi Zanzibar imetakiwa kutanua wigo wa utendaji kazi zake ili pia ijishughulishe na uhifadhi wa mazingira badala ya kufanya kazi za uokozi baharini pekee.
Mkuu wa Wilaya ya Mjini Kanali Mstaafu Abdi Mahmoud alitoa wito huo katika uzinduzi wa Jumuiya hiyo uliofanyika Ukumbi wa Hoteli ya Bwawani Mjini Unguja.
AMEsema maafa hayatokei upande wa baharini pekee bali yanaweza kutokea popote hivyo Jumuiya hiyo itanue wigo wake katika kukabiliana na mambo hayo.
Ameongeza kuwa kazi ya uokozi sio tu kufanywa wakati Maafa yanapotokea bali hata kutunza mazingira ya Baharini na Nchi kavu ni njia nzuri ya kujikinga na maafa mengi.
Katika kutekeleza hayo Mkuu huyo wa Wilaya amepanga kufanya harambee ya kujitolea na Wanajumuiya hiyo ili kufanya usafi wa kupigiwa mfano katika Manisapaa ya Mji wa Zanzibar.
Amewaasa Wanajumuiya hiyo kutokujihusisha na makundi ya kisiasa au dini katika kufanya mambo yao badala yake waangalie utu na Mustakabali wa Wananchi.
Kanali Mahmoud amewataka Wanajumuiya hiyo kuzidisha mashirikiano na upendo miongoni mwao ili Jumuiya iweze kusonga mbele.
Kwa upende wake Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Faki Bakar Faki amesema wameamua kuazisha Jumuiya hiyo ili kufanya shughuli za uokozi pale yanapotokea majanga bila kujali itikadi yoyote.
Faki amedai kuwa Uzoefu unaonesha kila panapotokea Majanga hasa ya baharini Asasi za kiraia na Watu binafsi ndio wanaokuwa wakwanza kufanya harakati za uokozi kabla ya Serikali kupitia Vikosi vyake kufika eneo la tukio na kuendelea na uokozi.
Ameiomba Idara ya Sayansi ya bahari kuwa karibu na Jumuiya hiyo na kuwawezesha kupata Kamera ambazo zitasaidia kupiga picha mambo mbalimbali wanayokutana nayo baharini.
Ameongezea kuwa Wamekuwa wakikutana na mambo mengi chini ya bahari wakati wa kufanya shughuli za uokozi au uvuvi na kwamba kama wangepiga picha zingesaidia kufanyiwa tafiti mbalimbali na kupatiwa majibu.
Kwa upande wake Afisa Tawala wa Wilaya ya Mjini Muhammed Abdallah ameisifia Jumuiya hiyo na kusema kuwa itasaidia sana katika kukabiliana na majanga ya baharini na hata nchi kavu.
Aidha ameongeza kuwa kwa muda mrefu Wavuvi wengi wamekuwa wakituhumiwa kwa kuvua Uvuvi haramu na kuongeza kuwa Jumuiya hiyo pia itumike katika kukabiliana na aina zote za uvuvi haramu
Baadhi ya Wanachama wa Jumuiya hiyo Walishiriki moja kwa moja katika Ajali za kuzama kwa Meli kadhaa Zanzibar ikiwemo Mv. Skirgit, Mv. Spice Islander1 na Mv. Fatih na hivyo kuamua kuunganisha nguvu kwa kuanzisha Jumuiya ili waweze kufanya kazi kwa pamoja.
Jumuiya ya Wazamiaji na Uokozi Zanzibar yenye Wanachama 200 Wazamiaji imeanzishwa kwa lengo la kusaidia Jamii pale yanapotokea maafa ambapo Makao makuu yake yapo Mtoni mjini Unguja.
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR