Na Mwandishi wetu
MWANASIASA mkongwe, Kingunge Ngombalemwiru, ameendeleza shutuma kwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, akisema Tume yake haikufanya utafiti wa kina wakati ilipokusanya maoni kuhusu muundano wa Muungano wa serikali tatu.
Akizungumza katika semina kwa wanahabari jana, Kingunge alisema, alisema Tume haikuakisi mazingira ya uchumi wa Tanzania na umuhimu wa Muungano uliopo sasa.
Alisema ya kazi nzuri iliyofanywa na Warioba na jopo lake la wataalamu, lakini kazi waliyoifanya ina upungufu mkubwa huku akitilia mkazo Muungano wa sasa wa serikali mbili umesaidia kujenga umoja wa kitaifa Tanzania na Tanzania kuwa nchi ya mfano Afrika.
Alisema Muungano uliopendekezwa na Tume utajenga matabaka ingawa unawafurahisha watu wanaopenda madaraka.
Hata hivyo, alionya kwamba hazi kubwa iko mbele kupata katiba bora itakayokubalika na makundi yote, ikiwemo kuhakikisha hazi za makundi mbalimbali wakiwemo wakulima, wafugaji na jamii Wahazabe ambao alisema kama hawatakikishiwa maslahi yao ndani ya katiba watatoweka.
Alisema wao wakati wanapigania uhuru waliweka uzalendo mbele badala ya kugombania vyeo, lakini hali hiyo ilibadilika baada ya uhuru na Mapinduzi, ambapo sasa wanasiasa wapo kwa ajili ya kupigania maslahi yao binafsi.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ali, licha ya kutangaza kuwa ni muumini wa muungano wa serikali mbili, aliwataka wajumbe wa bunge la katiba kuondoa msuguano uliopo ili Watanzania wapate katiba bora.
Aliwashauri wajumbe kutumia hotuba ya Jaji Joseph Warioba, hotuba ya Rais Kikwete pamoja na sheria nyengine kama miongozo muhimu watakapojadili rasimu ya katiba.
Aidha, aliwasihi wanahabari wanaoripoti bunge la katiba kuhakikisha makundi yote yanayounda bunge hilo yanapewa nafasi sawa badala ya kuripoti misimamo ya makundi fulani pekee.
“Mkianza kuchagua kuwa hoja hii ina nguvu zaidi kuliko ile mtawapotosha wananchi,” alisema.
Dk. Ayoub Rioba, mtaalamu wa masuala ya habari na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam , aliwasihi wanahabari kuripoti sawa yale yanayotokea katika ukumbi wa bunge hilo .
Hata hivyo, baadhi ya wanahabari walionesha hofu na wawasilishaji wa mada kuzungumzia zaidi masuala ya siasa na mfumo wa serikali badala ya kuwaelimisha waandishi umhimu wa kuripoti masuala ya bunge.
Walisema walitarajia waandaaji wa mkutano huo wangewatafuta watoa mada walio huru ambao hawaungi mkono mifumo yoyote ya serikali tofauti na mmoja ya wasiliajaji (Bashiru Ali) ambae ameonesha msimamo wa kuunga mkono serikali mbili wakati hapo si pahala pake.