Na Anna Nkinda, Maelezo
VIONGOZI wa dini nchini wametakiwa kuhubiri amani katika majukwaa yao ili jamii ielewe umuhimu wa kuwepo kwa amani na kuendelea kuishi kwa upendo na ushirikiano.
Wito huo umetolewa jana na mke wa Rais, Mama Salma Kikwete wakati akiwafuturisha wanakijiji cha Hoyoyo wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.
Alisema viongozi wa dini wana jukumu kubwa la kuhakikisha waumini wao wanaelewa umuhimu wa amani katika nchi kwa kujenga mshikamano kama waasisi wa Tanzania walivyouanzisha.
“Katika shughuli yetu hii tumekusanyika watu wa dini mbalimbali wanaofunga mwezi huu na wengine mwezi mwingine lakini dua ni dua kupitia kwa mwanadamu yeyote Mwenyezi Mungu inamfikia, hivyo basi tuzidi kushikamana kwa kila jambo.”
Alisema amani inatafutwa kwa miaka mingi lakini inaweza kutoweka kwa muda mfupi hivyo basi kila mtu hasa viongozi wa dini watumie muda wao kuhubiri umuhimu wa amani.
Kwa upande wake Sheikh Athuman Kinyozi alimshukuru mama Kikwete kwa futari aliyoiandaa kwa ajili yao na kusema mtu anayejitoa kwa ajili ya kufuturisha wengine anapata thawabu kwa Mwenyezi Mungu.
Alisema kufanya kitendo cha kufuturasha si lazima uwe na uwezo mkubwa kifedha bali unaweza ukanunua hata tende au maji na kuwapa watu waliofunga.