Ameir Khalid na Naima Hamza
WIZARA ya Mifugo na Uvuvi imeelezea kupata mafanikio makubwa katika sekta ya mifugo na uvuvi,katika kipindi cha mwaka wa fedha 2012- 2013.
Waziri wa wizara hiyo,Abdilahi Jihadi Hassan alieleza hayo jana wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa wizara hiyo kwa mwaka 2013/2014.
Alisema katika sekta ya mifungo wizara yake imeimarisha utoaji wa huduma za uzalishaji na utibabu wa mifungo, kutokana na kuongezeka kwa wajasiriamali wa mazao ya ya mifugo wanaozalisha samli, siagi, jibini, mtindi na maziwa ya kunywa.
sekta ya mifugo hivi sasa imetoa ajira kwa kaya 34,000 na kukua kwa asilimia 3.1 na kuchangia asilimia 3.8 ya pato la taifa katika mwaka 2012, ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu ya kuendeleza uzalishaji wa mifugo, ikiwemo vituo vya uzalishaji na utibabu wa mifugo, majosho na maeneo mapya ya karantini.
Kwa upande wa sekta ya uvuvi alisema umezidi kuimarika kutokana na kuongezeka kwa uvuvi wa baharini na pia wananchi wengi wameanza kufuga samaki na mazao mengine ya baharini.
Alisema hatua hiyo imewefanya wananchi wengi kuelimika na kuanza kufuga mazao ya baharini, ambapo kisiwa cha Pemba kimepata mafanikio makubwa.
Waziri Jihadi alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2012-2013 sekta ya uvuvi imepata mafanikio, ikiwemo kuongezeka kwa idadi ya samaki wanaovuliwa kutoka kilo 29,410,554 zenye thamani ya shilingi 103,180,991,590, ikiwa ni ongezeko la tani 651 sawa na asilimia 2.3.
Alisema shughuli za uvuvi zimekuwa kwa asilimia 2.3 na mchango wa sekta ya uvuvi katika pato la taifa umeongezeka kutoka asilimia 6.7 mwaka 2011 hadi kufikia asilimia 7.1 mwaka 2012, kuongezeka kwa ufugaji wa samaki na viumbe vyengine vya baharini.
Katika hutuba hiyo Waziri Jihadi alisema wizara hiyo inakusudia kutumia jumla ya shilingi 3,611,000,000 kwa kazi za kawaida, ambapo kati ya fedha hizo shilingi 2,326,000,000 ni kwa ajili ya mishahara na shilingi 1,285,000,000 ni kwa matumizi mengineyo ya kazi za kawaida.
Kwa upande wa kazi za maendeleo jumla ya shilingi 1,294,000,000 zimetengwa ambapo shilingi 664,000,000 ni fedha kutoka washirika wa maendeleo kwa kutekeleza miradi miwili, miradi ya kichaa cha mbwa na mradi wa kushajiisha ufugaji wa mazao ya baharini.
Wakati shilingi 630,000,000 ni kutoka serikalini katika kutekeleza miradi sita ya maendeleo, kuimarisha miuondo mbinu ya mifugo, kudhibiti maradhi ya mafua ya ndege na maradhi yasiyo kuwa na mipaka, kudhibiti kichaa cha mbwa, kupandisha ng'ombe kwa sindano, kuimarisha ufugaji wa samaki na kuimarisha uvuvi wa bahari kuu.