Na Kija Elias, MOSHI
ABIRIA wanaosafiri katika wilaya sita za mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, wamekwama kusafiri kwa saa 10, baada ya wamiliki wa mabasi na madereva kugoma kutoa huduma,wakililalamikia jeshi la polisi kikosi cha usalama barabarani, kuwadai rushwa kwa lengo la kuficha makosa.
Katika hali ambayo haikuwa ya kawaida vurugu kubwa ziliibuka katika kituo kikuu cha mabasi ya mjini Moshi, kati ya watu wanaodaiwa kuwa wafanyakazi wa mabasi hayo na wapiga bede na kusababisha gari lililowabeba askari kanzu wa jeshi la Polisi mkoa wa Kilimanjaro, kupigwa mawe na kisha kuvunjwa vioo.
Vurugu hizo zilijitokeza baada ya askari kujaribu kumkamata mmoja wa madereva wa mabasi yaliyogoma kufanya safari zake katika kituo cha abiria wanaokwenda mpaka wa Holili uliopo kati ya Tanzania na Kenya pamoja na mji wa Himo na Marangu.
Pia katika vurugu hizo, kituo cha mabasi kiligeuzwa uwanja wa mpira wa miguu, kwa takribani dakika 75, huku pembeni askari hao wakishuhudia.
Hali hiyo ilisababisha Mkuu wa kituo cha polisi Moshi kuomba nguvu za ziada kwa ajili ya kukabiliana na nguvu kubwa ya wananchi hao, ambapo kikosi cha kutuliza ghasia kilifika.
Akizungumzia mgomo huo, Mwenyekiti wa Chama cha Wasafirishaji wa mabasi kanda ya kaskazini (AKIBOA), Hussein Mrindoko na Mwenyekiti wa (AKIBOA) mkoa, Mohamed Nkya, walisema wameamua kugoma kutokana na baadhi ya askari kugeuza stakabadhi za malipo yanayotokana na faini kuwa mtaji wa kibiashara kwa kuwa wanatoza gari moja faini ya shilingi 30,000 hadi mara tatu kwa siku.
Kwa upande wake, Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani, alikiri kumpiga makonde mmoja wa wamiliki wa mabasi wa wilaya ya Hai, Abdulrazack Mtoro, akidai sheria inamruhusu kufanya hivyo.
Naye, Mkuu wa kituo kidogo cha polisi kituo kikuu, Hendry Nguvumali, alisema madereva na wamiliki wa mabasi hayo wanasema uongo na kumdanganya Mkuu wa Mkoa kwamba yeye ni mlevi wa kupindukia na amekuwa akijisaidia ovyo nyuma ya mabasi ya abiria, jambo ambalo haliwezi kumzuia kutimiza wajibu wake.
Akizungumzia tuhuma zilizotolewa na wamiliki wa mabasi hayo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, alisema kuhusu malalamiko yaliyotolewa dhidi ya askari hatua zitachukuliwa dhidi yao .
Hata hivyo, alisema wananachi na madereva wa mabasi wanatakiwa kutii sheria za usalama barabarani.
"Askari kuwa mlevi na kushindwa kusimamia sheria za barabarani, tutamchukulia hatua mara moja, ulevi wa kupindukia kwa kweli umelifedhehesha jeshi la polisi lakini pia suala la kupiga watu makonde siyo utaratibu kwa sababu ofisa anatakiwa kufuata taratibu na kwa kuwa amekiri mwenyewe,nitalitazama kwa kufanya uchunguzi," alisema.
Akizungumzia mgomo huo, Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, alisema mgomo wa mabasi ukiachwa uendelee utasababisha kuporomoka uchumi wa mkoa huo na kutoa amri kwa Mamlaka ya Usafirishaji wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) kutengeneza ratiba ya kukutana mara kwa mara na wadau wa usafirishaji.