Na Kunze Mswanyama,Dar
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),imetoa onyo kali kwa vyama vya siasa vinavyoendelea na kampeni ya uchaguzi mdogo jimbo la Chalinze kwa kutumia lugha za chuki na zisizo za staha ambazo zinaweza kusababisha wananchi kujichukulia sheria mkononi.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Damian Lubuva, imesema kama tume wanafuatilia kwa karibu kampeni hizo.
Aliwasihi wanasiasa kuacha kutumia lugha mbya huku wakitakiwa kuzingatia ratiba waliyojipangia ili kuondoa migongano isiyokuwa ya lazima.
“Tume inasisitiza wagombea wote kufanya kampeni za kiungwana na kunadi sera za vyama vyao kwa kuzingatia sheria,kanuni na taratibu zote zilizoainishwa kwa mujibu wa sheria,” ilisema taarifa hiyo.
Alivitaka vyama kuacha kuhamasisha wanachama wao kujichukulia sheria mkononi na anayeshukiwa kuvunja sheria akabidhiwe kwenye vyombo vya vya sheria.
“Tume inatarajia kuona kila mwananchi mwenye sifa za kupiga kura katika jimbo la Chalinze anatumia haki yake ya kikatiba na kisheria kupiga kura kwa amani na utulivu,” ilisema.
Uchaguzi mdogo wa jimbo unaotarajiwa kufanyika Aprili 6,unafanyika kufuatia kifo cha aliekuwa mbunge jimbo hilo , Said Bwanamdogo ambapo Chama cha Mapinduzi kimemsimamisha Ridhiwani Kikwete.
Uteuzi wa wagombea ulifanyika Machi 12,kampeni zilianza Machi 13 na zinatarajiwa kuhitimishwa Aprili 5 mwaka huu ili kupisha uchaguzi mdogo Jumapili Aprili 6.