Na Denis Mlowe, IRINGA
ASILIMIA 25 ya wanawake wako katika hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa saratani ya shingo ya uzazi na kusababisha vifo kwa wanawake nchini.
Kwa mujibu wa takwimu, asilimia 80 ya wagonjwa wanaobainika na aina hiyo ya saratani, hugundulika wakati ugonjwa huo ukiwa tayari umeshasababisha athari kubwa na kushindwa kutibika.
Hayo yamebainishwa na Katibu tawala wa mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu, wakati wa uzinduzi wa mradi wa kuhamasisha jamii kuhusu huduma za uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi, uliondaliwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya T-Marc Tanzania .
Alisema asilimia kubwa ya wanawake hawajitokezi kuangalia afya zao na kupima saratani, hali inayosababisha ugonjwa huo kuongezeka.
Alisema takwimu kutoka taasisi ya saratani ya Ocean Road, inaonyesha kati ya wagonjwa wa saratani wanaopelekwa katika taasisi hiyo kila mwaka, zaidi ya wagonjwa 5,000 wana tatizo la saratani ya shingo ya kizazi.
Alisema wataalamu wa mambo ya saratani wamegundua kuwa kuna uhusiano mkubwa kati ya saratani ya mlango wa kizazi na maambukizi ya virusi vya Ukimwi.
Alisema kutokana na tatizo hilo mkoani Iringa, serikali imewataka wadau kujitokeza kuunga mkono ili kuhakikisha wanawake wanakuwa salama.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa T- Marc Tanzania,Diana Kisaka, alisema kila mwaka wanawake 6,000 hugundulika na saratani ya mlango wa kizazi.
Alisema wanawake 4,000 hufa kila mwaka nchini kutokana na saratani hiyo sawa na wanawake 11 wanaofariki kila siku.
Alisema takwimu za hospitali ya Ocean Road zinaonesha asilimia 40 ya vifo
vinatokana na matatizo ya saratani ni wagonjwa saratani ya mlango wa kizazi.
Alisema ugonjwa huo ni tatizo kubwa ulimwenguni na hasa katika nchi zinazoendelea ambapo takwimu za kimataifa zinaonesha kila mwaka zaidi ya watu milioni 5 hugundulika na saratani na kufanya tatizo hilo kufikia asilimia 29.